April 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi HGWT aitaka jamii kukemea mila zinazokwamisha elimu kwa wasichana 

Fresha Kinasa, TimesMajiraOnline ,Mara.

MKURUGENZI  wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali linalojishughulisha na kupambana na Ukatili wa Kijinsia Mkoa wa Mara  la ‘Hope for Girls and Women in Tanzania’ (HGWT) Rhobi Samwelly amesema Jamii inao wajibu wa  kuhakikisha mila na desturi zisizofaa ambazo  zimekuwa zinakwamisha Watoto wa kike kushindwa kuendelea na masomo  zinapigwa vita.

Amesema, serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri na kufanya Uwekezaji mkubwa katika sekta ya Elimu ikiwemo kujenga vyumba vya madarasa vya kutosha,  kuajiri Walimu  na kuondoa ada ili Watoto wote wapate fursa ya elimu bila vikwazo.  

Hivyo, mila ambazo zinawafanya Watoto wa kike wasisome lazima zikemewe na kila mmoja  kwa nafasi yake na juhudi za pamoja  ziendelee  kuchukuliwa baina ya wazazi, Mashirika binafsi na Serikali   ili zisikwamishe ndoto zao hasa maeneo ya Vijijini ambako elimu inahitajika zaidi kutolewa.
 
Rhobi ameyasema hayo  Machi 29, 2025  katika Mahafali ya Wahitimu wa  kidato cha sita  ya  Wanafunzi Vijana Wakatoliki Tanzania    (TYCS) wa Tarime Sekondari na Ingwe Sekondari  yaliyofanyika kwa pamoja  shuleni hapo. Ambapo pia  amewataka Wahitimu hao baada ya kufanya mitihani ya kidato cha sita, wasijiunge na makundi maovu ama kushiriki matukio ya kihalifu.

“Tuendelee kukemea ukeketaji kwa Watoto wa kike na  ndoa za utotoni ambazo zimekuwa zikiwafanya wasitimize masomo yao. Tuwasomeshe Watoto wa kike kwa juhudi zote, tuwalinde na kuwawekea mazingira wezeshi ili  wasipate vikwazo. Serikali inataka kuona kila mtoto Mtanzania anasoma tusiwaozeshe watoto wa kike kwa lengo la kupata ng’ombe, tuwapeni urithi wa kudumu ambao ni elimu.” amesema Rhobi. 

Pia, ametoa wito kwa Watanzania, kuendelea kudumisha amani, umoja, upendo na mshikamano na kutoshiriki kuvuruga amani iliyopo nchini kwani ndio Msingi wa Maendeleo ambayo yanafanywa na Serikali na kupelekea Taifa kupiga hatua.

Akisoma risala  ya Wahitimu hao wa kidato cha sita wa  (TYCS) Johnson Joseph amesema kuwa, wanamshukuru Mungu kwani wameweza kushirikiana kitaaluma na wanafunzi wengine katika masuala ya kitaaluma na kuimarisha Umoja.

“Mafanikio mengine tumeweza  kununua Vitendea kaz vya kiroho,kuhudhuria makongamano ya kiimani, kujenga ushirikiano kati yetu  na Jamii, kuwa na kwaya imara katika tawi letu,  kusaidiana kitaaluma,  kukuza ufaulu wa wanachama, kufanya matendo mbalimbali ya huruma kwa Jamii ikiwemo,”amesema na kuongeza kuwa.

Mkuu wa shule ya Tarime Sekondari Mwalimu Chenge Marwa ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanya Uwekezaji mkubwa wa  miundombinu katika shule hiyo, hali ambayo  amesema imeendelea kuwafanya wanafunzi kufanya vizuri sana katika mitihani ya kuhitimu kidato cha sita.