December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkulima Mbunifu yawafikia wakulima 100,000 Tanzania

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma

WAKULIMA wadogo zaidi ya 100,000 nchini Tanzania wamefikiwa na jarida la Mkulima Mbunifu ambalo huwapa elimu ya ukulima wenye tija na ufugaji bora.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Meneja Mradi wa Mkulima Mbunifu, Erica Rugabandana wakati wa warsha ya siku mbili iliyowakutanisha wawakilishi wa wakulima wadogo, maofisa ugani, maofisa wa serikalini, waandishi wa habari na wadau wa kilimo kutoka taasisi mbalimbali.

Akizungumzia Mradi mpya wa Mawasiliano ya Wakulima (FCP), Rugabandana amesema mradi huo umeongeza idadi ya wakulima wanaofikiwa na jarida la Mkulima Mbunifu linalotoa elimu sahihi ya kilimo chenye tija, kilimo ikolojia na ufugaji bora wa aina tofauti za wanyama na ndege.

Amesema jumla ya wakulima 63,832 wamefikiwa na nakala sita za jarida la Mkulima Mbunifu kwa njia tofauti ya mtandao tangu kuanza kwa wa Mawasiliano ya Wakulima (FCP), mwaka 2023.

Meneja Mradi huyo amesema Mkulima Mbunifu chini ya Shirika la Biovision Africa Trust (BVAT) kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT) wameandaa warsha hiyo ili kuendelea kupata mrejesho na kuongeza mtandao wa Mawasiliano kati ya wakulima, maofisa ugani kutoka serikalini na wadau wa kilimo ikolojia wa mashirika mengine.

Rugabandana ameitaja mikoa yenye vikundi vya wakulima na wafugaji vinavyopata huduma na mafunzo kupitia jarida la Mkulima Mbunifu makala ngumu kuwa ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Manyara na Singida.

Amesema kabla ya kuanza kwa Mradi wa Mawasiliano ya Wakulima mwaka 2023 zaidi ya wakulima 75,000 kutoka mikoa tajwa walipata nakala ngumu ya jarida la Mkulima Mbunifu kuanzia mwaka 2011.

“Mradi huu wa Mawasiliano ya Wakulima umeongeza tija ya ufikiwaji wa jarida letu la Mkulima Mbunifu kwa sababu wakulima wanapata huduma zetu kwa njia tofauti za kiteknolojia.

“…Uwepo wetu hapa leo ni kupata mrejesho hili jarida linatoka kila baada ya miezi miwili sasa tumefunga mwaka na majarida sita ninyi ni mashahidi idadi ya wakulima na wafugaji wanaopata jarida letu imeongezeka.

“Sio idadi tu mmesikia shuhuda za wasomaji wetu namna wanavyotumia jarida hili kuongeza tija kwenye shughuli zao za kiuchumi kwa hiyo lengo letu la kutaka kuwafikia wakulima wote wadogo Tanzania lipo mbioni kufikiwa,” amesema Rugabandana.

Mtendaji Mkuu wa Shirika la SAT, Janet Maro amesema lengo la warsha hiyo ni kuongeza wigo wa wasomaji wa jarida la Mkulima Mbunifu tukiamini kwa dhati kwamba elimu wanayoipata itawasogeza kwenye ukulima bora unaotunza mazingira na kuepuka madawa ya viwandani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wawakilishi wa wakulima hao waliohudhuria warsha hiyo, walisema elimu wanayoipata ya kutunza shamba, kutengeneza viwatilifu na ufugaji wa kisasa inawaongezea kipato.

Mama Shujaa wa Chakula kutoka Lushoto mkoani Tanga amesema elimu kubwa ya kilimo na ufugaji bora wanayoipata kwa kusoma majarida ya kila mwezi ya Mkulima Mbunifu yamewaongezea tija na kipato kwenye kilimo na ufugaji wao.

“Ukisoma Mkulima Mbunifu unakuwa ofisa ugani… Sisi kwenye kikundi chetu tunalima, tunapalia, tunatengeneza mbolea na dawa za kufukuzia wadudu Kwa kufuata maelekezo ya jarida la Mkulima Mbunifu.

“Tija ipo kubwa sana, kwanza gharama za kununua viatilifu na kikubwa zaidi tunafanya kilimo hai tunauhakika wa chakula kisichokuwa na madawa ya viwandani huku tukitinza mazingira,” amesema mama Shujaa wa Chakula.

Ofisa Kilimo Idara ya Maendeleo ya Mazao sehemu ya Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Kilimo, Matungwa Bagwerwa, ameupongeza Mradi wa Mkulima Mbunifu na kuahidi kuwahamasisha maofisa ugani kulipata jarida hilo kwa wingi na kulipeleka kwa wakulima wanaowahudumia.

Amesema serikali imefuangua milango ya ushirikiano kwa wadau wa kilimo na kuahidi kuwatumia maofsa wake kuhakikisha kila mkulima anafikiwa na kuhudumiwa.

Baadhi ya wakulima wakiwa kwenye vikundi kujadili baadhi ya mada zinazohusu kilimo ikolojia na ufugaji bora.
Washiriki wa warsha ya siku mbili iliyoandaliwa na Mkulima Mbunifu wakiwa kwenye picha ya pamoja jijini Dodoma.