January 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkonge kuuzwa soko la utalii Zanzibar

Na Mwandishi wetu

Katika mwendelezo wake wa kuhamasisha matumizi ya bidhaa za Mkonge nchini, Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), imedhamiria kulifanya zao la Mkonge kuwa zao la kitalii ambapo inatarajia kuingiza bidhaa zinazotokana na zao hilo katika Soko la Kitalii kupitia vijana kutoka visiwani humo.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TSB, Saddy Kambona alipokuwa akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo maalumu kwa vijana kutoka katika Chuo cha Mafunzo Zanzibar na Wanachama wa Klabu ya Mkonge ya Coastal ya Shule ya Sekondari ya Coastal ya jijini Tanga kuhusu sekta ya Mkonge.

Mkurugenzi Kambona amesema wamekuwa na kikao nao kuwaelezea fursa mbalimbali zilizopo katika mnyororo wa thamani wa zao la Mkonge na kwamba wanaweza kutumia au kushirikiana baina ya bodi na chuo hicho kuona ni namna gani tunaweza wapakatiwa mafunzo maalumu kupitia vituo hivyo viwili ambavyo vitaanishwa Tanga na Zanzibar.

Aidha, pamoja na mambo mengine, wamehitimisha mafunzo ya ndani ya kujadiliana juu ya fursa mbalimbali zinazotokana na Mkonge ambazo Wazanzibar wanaweza wakazitumia ambapo lengo ni kuhakikisha wanamsaidia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuondoa changamoto ya ajira hususani kwa vijana na kina mama.

“Tumekuwa na wakati mzuri kuwafundisha vijana ujuzi mbalimbali katika kutengenezeza zana za kutumia mikono (handcraft) kwa kutumia zao la Mkonge kwa ajili ya soko la utalii la Zanzibar.

“Kwa kuwa Zanzibar ni ardhi ya karafuu si rahisi kulima mkonge hivyo tunaweza tukatumia Mkonge kutoka Tanzania Bara kwa kutumia Soko la Utalii la Zanzibar kuzalisha bidhaa mbalimbali za mikono pia tunaweza tukatumia soko hilo kukuza hizo bidhaa za kutumia nyuzi asilia.

“Kwa hiyo leo walikuja wamepata mwongozo katika sura ile ya awali kujua tu Mkonge unalimwa vipi, unaandaliwaje, mashine za uchakataji zinafanyaje kazi na bidhaa zinazalishwaje,” amesema Mkurugenzi Kambona.

Pamoja na mambo mengine, amesema kwa sasa bodi imeona inaweza kuwapelekea bidhaa za Mkonge huko huko Zanzibar ili watumie Mkonge badala ya makumbi ya nazi ambayo wanayatumia sasa kutengenezea vitu lakini yanaweza kuharibika ili sasa wabuni bidhaa mbalimbali kwa kutumia nyuzi za mkonge na kuwafundisha vijana wengine zaidi.

“Sasa kwa kuanzia tumeanza na tutawapelekea malighafi ili waanze kubuni bidhaa mbalimbali ili baadaye utaalamu ukishapatikana usambae kwa vijana wengine wa Zanzibar na pia tunaweza kupitia hiyo njia vijana wengi wakajiajiri kwenye mnyororo mzima wa thamani wa zao la Mkonge,” amesema.