Na Ashura Jumapili, Timesmajira Online,Karagwe
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu Abdallah Kaim,amempongeza Mwekezaji mzawa wa kiwanda cha kuchakata maziwa wilayani Karagwe mkoani Kagera,Jossam Ntangeki kwa jitihada kubwa aliyofanya kwa uwekezaji huo wenye thamani ya bilioni 8.6.
Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge Kitaifa ametoa pongezi hizo wakati Mwenge wa Uhuru ulipotembelea kiwanda hicho, Agousti 13, mwaka huu ambapo amesema mradi huo una viwango vyenye ubora unaotakiwa kwa biashara ya kisasa.
Kaim, amesema Mwenge wa Uhuru ,umepokea taarifa inayohusiana na mradi wa kiwanda hicho ambapo umetembelea ,kukagua na kujionea maendeleo yaliyopo ambayo ni mazuri.
“Kiwanda hiki ni cha kisasa chenye ubora wenye viwango vya juu katika uwekezaji wa kisayansi,”amesema Kaim.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ,ameendelea kuweka mazingira bora na rafiki ili wawekezaji wa ndani na nje ya nchi waweze kufanya uwekezaji wenye tija kwa maslahi mapana ya taifa.
Pia amesema serikali imefanya kazi kubwa katika mradi huo ikiwemo kusamehe kodi za mitambo iliyofungwa kiwandani hapo ili kuhakikisha muwekezaji anatoa fursa mbalimbali za ajira
Awali Mkurugenzi wa kiwanda cha Kahama Fresh Jossam Ntangeki, amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata lita elfu ishirini za maziwa kwa siku na gharama ya mradi huo wa kiwanda ni biilioni 8.6.
Ntangeki, anasema wanategemea kupata maziwa kutoka maeneo yanayozunguka Mkoa wa Kagera huku lengo kuu la mradi huo ni kuwa na soko la uhakika kwa wafugaji wa Mkoa huo.
Amesema licha ya Mkoa wa Kagera kuwa na maziwa mengi na wafugaji wengi lakini haukuwa ma kiwanda cha kuchakata maziwa huku wafugaji wengi wanashindwa kufanya ufugaji wa kisasa kwa sababu hawakuwa na soko la kuuza maziwa yao .
Ambapo kiwanda kinatarajia kuanza kufanya kazi mwezi Octoba mwaka huu na wanatarajia kutoa ajira zisizopungua 300 za wataalam na wasiokuwa wataalam ambazo tayari zimetangazwa.
Hata hivyo katika kuboresha soko hilo la maziwa kiwanda hicho kimeanzisha utaratibu wa kukopa ng’ombe na kulipa maziwa yaani mfugaji anakopesha ngo’mbe yeye analipa kwa kuuza maziwa kwa muda wa miaka miwili.
“Ng’ombe wanaokopeshwa ni mtamba wanakuwa na mimba ya miezi sita hadi saba na mwenyewe thamani ya milioni 3 akijifungua ndama pia anakuwa mali ya mfugaji,hadi sasa
kiwanda kimeishawakopesha wafugaji ng’ombe mtamba 300 kuanzia mwaka jana hadi sasa,”.
Kadhalika amesema ufugaji wa kisasa unaongeza uzalishaji na ng’ombe mmoja mtamba anakamuliwa kwa siku 200 na kila siku anatoa lota 15 hadi 25.
Robert Rwenkome,ni mfugaji ameieleza TimesMajira kuwa yeye alikuwa mfugaji wa ng’ombe wa nyama lakini alipopewa somo la ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na faida zake alianza kufuga.
Rwenkome, anasema ufugaji huo wa kopa ng’ombe lipa maziwa unafaida kubwa kwake kwa sababu alikopa ng’ombe 25 sasa anakaribia kumaliza deni lake huku akiwa na faida ya ng’ombe wengine 25 na jumla kuwa mmiliki wa ng’ombe 50 wa maziwa.
“Nina washauri wananchi wengine kuanza kuwekeza katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ambao ni dili zuri kwa kutumia mradi wa kopa ng’ombe lipa maziwa,”amesema .
Hata hivyo amesema wanakumbana na changamoto kubwa ya kukabiliana na watu wanaochoma moto maeneo ya malisho hasa nyakati za kiangazi.
More Stories
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania