Na Esther Macha, Timesmajira Online Rungwe
MKIMBIZA Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi, amepongeza utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma ya maji safi katika Mji wa Tukuyu, wilayani Rungwe mkoani Mbeya, akisema ni miongoni mwa miradi mikubwa nchini inayotekelezwa kwa ufanisi na tija kubwa kwa wananchi.
Akizungumza Oktoba 12, 2025, wakati wa uzinduzi na ukaguzi wa mradi huo uliopo Kata ya Msasani, Ussi amesema Mwenge wa Uhuru umeendelea kushuhudia mafanikio makubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini, ikiwemo sekta ya maji, ambayo imekuwa kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Yote haya ni matokeo ya kuwa na Rais mwenye weledi, mchapakazi na mwenye kujali wananchi. Tangu alipoteuliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia aliweka bayana dhamira ya kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji vijijini na mijini,” amesema Ussi.
Ameongeza kuwa uanzishwaji wa mamlaka maalum za maji mijini na vijijini, ikiwemo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (UWSA) na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa watanzania wengi.
“Nimetembelea mikoa 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa hakika mameneja wa mamlaka za maji wamekuwa wakitekeleza wajibu wao ipasavyo. Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa maeneo yanayofanya vizuri zaidi,” amesisitiza Ussi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uzalishaji Maji na Usafi wa Mazingira Mbeya (UWSA), Mhandisi Barnabas Konga, ameema mradi huo una uwezo wa kuzalisha lita milioni 19 za maji kwa siku, ambazo ni sawa na asilimia 127 ya mahitaji ya sasa ya Mji wa Tukuyu.
“Awali tulikuwa na uzalishaji wa tani milioni 11 kwa siku, lakini baada ya kuboresha mtandao wa maji kutoka Mto Mbaka, sasa tunazalisha lita milioni 8 zaidi, na hivyo jumla kufikia milioni 19,” amesema Konga.
Amefafanua kuwa mradi huo umegharimu shilingi bilioni 3.9, fedha zilizotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Maji. Kati ya fedha hizo, bilioni 3.6 tayari zimepokelewa na kulipwa kwa wakandarasi, huku gharama halisi ikiwa chini ya makadirio ya awali ya shilingi bilioni 4.5.
Konga amesema mradi huo unatekelezwa na UWSA kwa ushirikiano na Serikali Kuu, ambapo tenki kuu la kuhifadhia maji lina ujazo wa lita milioni 1.5.
Aidha, ameibainisha kuwa wananchi wa Kata ya Msasani walishirikishwa kikamilifu katika hatua zote za utekelezaji wa mradi, ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi na usimikaji wa miundombinu ya maji.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Elizabeth Fulahini, amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuondoa adha ya upatikanaji wa maji safi ambayo imekuwa changamoto kwa muda mrefu.
“Tunamshukuru sana Rais Samia na Serikali kwa kutuletea mradi huu. Awali tulikuwa tunatembea umbali mrefu kutafuta maji, lakini sasa tutapata huduma karibu,” amesema fulahini kwa furaha.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama