January 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkenge ashangazwa timu nne kushiriki Ligi ya Wilaya

Na Omary Mngindo, TimesMajira Online, Bagamoyo

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani Muharami Mkenge, ameshangazwa na uchache wa timu zizoshiriki michuano ya kusaka timu zitakazoiwakilisha Pwani katika mashindano ya Ligi Daraja la Tatu.

Katika mashindano ni timu nne pakee ndizo zilizojitokeza ambapo timu za Kiembeni FC ilitwaa ubingwa Ligi Daraja la nne huku King Stone wakishika nafasi ya pili na Msata United nafasi ya tatu.

Akizungumza baada kumalizika kwa mashindano hayo yaliyofanyika kweye uwanja wa Mwanakalenge ambapo washindi hao watatu wataiwakilisha wilaya hiyo kushiriki Ligi Daraja la tatu Mkoa iliyo chini ya Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa COREFA, Mkenge amesema kuwa, ameshangazwa kuona timu zizoshiriki ligi hiyo inayowezesha washindi kushiriki ligi ngazi ya Mkoa mpaka Taifa, ikishirikisha timu chache huku michuano ya mitaa inayoandaliwa na wadau yakiwa na timu nyingi.

Amesema, Wilaya ya Bagamoyo ina klabu nyingi lakini zilizoshiriki ligi hiyo kubwa ngazi husika chache jambo ambalo halileti picha nzuri.

“Kuna haja ya kukaa na viongozi wa Chama Cha Mpira wa Miguu wilaya ya Bagamoyo (BFA) na wadau wanaosaidia mchezo huu, kwa pamoja tuone kitu gani kifanyike ili kuhakikisha klabu zetu kwa wingi wao zinashiriki ligi hiyo kwani lengo ni kuongeza ushindani katika ligi yetu, haiwezekani Bagamoyo yenye klabu zaidi ya 20, ligi ichezwe na timu nne tu,” amesema Mkenge.

Lakini pia kiongozi huyo aliipongeza Kiembeni FC kwa kutwaa ubingwa, King Stone na Msata zikishika nafasi ya pili na tatu huku Kerege ikishika nafasi ya nne kushiriki ligi hiyo kwani zimetimiza wajibu wao wa kikatiba wa kushiriki ligi kuanzia ngazi hiyo mpaka ya juu.

“Nawapongeza Chama ba soka Bagamoyo kwa kufanikisha ligi yake wilayani kwetu na kuwapata wawakilishi watatu wanaokwenda kucheza Ligi ya Mkoa, itayotoa timu za kushiriki ligi ya Mabingwa wa Mikoa,” amesema Mkenge.

Aidha kiongozi huyo amesme, mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu na atakaposhinda na kurejea madarakani, mbali na shughuli mbalimbali pia atakutana na wadau hao wa michezo ili kuzungumzia suala hilo.