Na Suleiman Abeid,
Shinyanga.
UGOMVI wa fedha ya matumizi kiasi cha shilingi 10,000 kati ya mume na mke umesababisha madhara kwa mmoja wa wana ndoa hao kwa kujeruhiwa vibaya sehemu zake za siri.
Tukio hilo limetokea juzi katika Kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga likiwahusisha wakazi wa kata hiyo waliotajwa kwa majina ya Shaibu Manila (36) na mkewe aliyetambuliwa kwa jina moja la Mwajuma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Debora Magiligimba chanzo cha ugomvi huo ni Mwajuma kushinikiza kupewa fedha ya matumizi ambapo mumewe aligoma kutoa fedha hiyo hali iliyomuudhi mwanamke.
“Chanzo cha tukio hili ni mwanaume kumnyima mke wake fedha ya matumizi kiasi cha shilingi 10,000, ndipo ukaibuka ugomvi na kusababisha waanze kupigana ambapo mwanaume alikatwa sehemu zake za siri eneo la Korodani la kulia,” alieleza Magiligimba.
Aliendeleakufafanua kuwa mara baada ya mwanaume huyo kujeruhiwa na mke wake, Manila alikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mkoani Shinyanga kupatiwa matibabu na amesharuhusiwa ambapo mkewe mwanamke amekimbia na kwenda kusikojulikana na hivi sasa anatafutwa na polisi.
Kamanda hiyo ametoa wito kwa wanandoa au watu wenye mahusiano ya kimapenzi, wanapokuwa na mgogoro waache kuchukuliana sheria za mkononi, bali wapeleke matatizo yao kwa wazee wenye busara au wafike kwenye ofisi za ustawi wa jamii na dawati la jinsia ili waweze kuwatafuta suluhu ya tofauti zao.
Katika hatua nyingine alisema Jeshi hilo limefanya msako na doria mbalimbali katika kipindi cha kuanzia Decemba 2019 hadi Marchi 2020, na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 48 wakiwa na mali mbalimbali zinazohisiwa ni za wizi, ambapo 28 kati yao wameshafikishwa mahakamani na wengine 20 upelelezi bado unaendelea.
Kamanda Magiligimba ametoa wito kwa wananchi mkoani Shinyanga katika kusheherekea siku kuu ya Pasaka, wakae majumbani mwao na kuepuka misongamano ili kuendelea kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, huku akiwataka madereva wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima.
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya