April 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkazi wa Mbagala ajishindia gari kupitia Promosheni ya Yas Magift

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPENI ya Magift ya Kugift kutoka YAS na Mixx by YAS imeendelea kubadilisha maisha ya Watanzania, ambapo Machi 28, 2025, ilibadili maisha ya Ramadhani Abdallah Mwinchande, mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam.

Abdallah amekabidhiwa rasmi gari jipya-zero kilomita, aina ya KIA Sorento na anakuwa mtanzania wa pili kushinda zawadi hiyo kabambe kupitia promosheni ya YAS ya Magift ya kugift.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi hiyo, Mkurugenzi wa YAS-Kanda ya Dar Kusini, Robert Kasulwa amesema promosheni hiyo ni sehemu ya shukrani kwa wateja wa YAS na Mixx by YAS kwa uaminifu wao.

“Leo tunaandika historia nyingine kwa kumkabidhi mshindi wetu, Ramadhani Abdallah Mwinchande zawadi ya gari jipya aina ya KIA Sorento. Huu sio tu ushindi wa mtu mmoja bali ni ushindi wa wateja wetu wote ambao wanaendelea kutumia huduma zetu kila siku.

Mkurugenzi wa YAS-Kanda ya Dar Kusini, Robert Kasulwa (katikati), akimkabidhi funguo za gari jipya mshindi wa promosheni ya Magift ya Kugift, Ramadhani Abdallah Mwinchande (aliyevaa kanzu) mkazi wa Mbagala. Hafla ya makabidhiano ilifanyika Mbagala Zakhem, Machi 28, 2025, jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia kutokea kushoto ni Mkurugenzi wa YAS-Kanda ya Dar Kaskazini, Aidan Komba, Meneja wa Yas-Kanda ya Temeke Mashariki Stella Kikwa, Meneja Biashara Mixx by Yas Phoebe Gaula, Meneja wa Yas-Kanda ya Ilala, Macbeth Manene na Meneja wa Yas-Kanda ya Temeke Kusini, Dorah Nyamko.

“YAS na Mixx by YAS tunaamini kuwa wateja wetu ndio msingi wa kila tunachofanya, na ndio maana tunajitahidi kutoa huduma bora na promosheni zenye thamani halisi,” amesema Kasulwa.

Tangu kuzinduliwa kwa kampeni ya Magift ya Kugift, zaidi ya Watanzania 1,300 wamenufaika na zawadi mbalimbali, zikiwemo magari mawili mapya, fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 840, na simu janja zaidi ya 540.

Akizungumzia mafanikio ya Kampuni ndani ya siku 100 tangu kufanyika kwa mabadiliko ya chapa kutoka Tigo na Tigopesa kwenda YAS na Mixx by YAS, Kasulwa amebainisha kuwa kampuni hiyo imepokea tuzo mbalimbali zikiwemo kutoka Ookla, TEHAMA Awards na TRA kama mlipaji mkubwa wa kodi kupitia ushuru wa forodha.

Mshindi wa gari hiyo, Ramadhani Abdallah Mwinchande ameishukuru YAS na Mixx by YAS kwa zawadi hiyo na kusisitiza kuwa ushindi wake ni uthibitisho kuwa kila mteja ana nafasi ya kushinda kupitia promosheni hiyo.

“Nina furaha kubwa kupokea zawadi hii. Nilipopigiwa simu kuambiwa nimeshinda gari mara ya kwanza sikuamini. Lakini YAS walinihakikishia ushindi wangu na kweli leo naondoka na gari jipya. Nawashukuru YAS na Mixx by YAS kwa kutambua na kuthamini wateja wake,” amesema Mwinchande.

Kwa upande wake, Kasulwa aliwahimiza wateja kuendelea kushiriki katika promosheni mbalimbali zinazoendelea na kutumia huduma za YAS na Mixx by YAS, huku akisisitiza kuwa kampuni hiyo itaendelea kuwa karibu na wateja wake kwa kutoa huduma bora na kuwapa fursa zaidi za kushinda.