January 29, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkapa,Rais aliyeamini katika Ushirika kutokomeza umaskini

“USHIRIKA ni mbinu sahihi ya kuondokana na kunyanyaswa kwa wananchi wenye kipato cha chini, wakiwemo wakulima wadogo na kuwapa chombo cha kumiliki uchumi wao kwa pamoja.

Ili vijana waanze kuhamasika na kuelimika juu ya ushirika na baadaye wajiunge na kuendeleza ushirika kwa uchumi endelevu, Elimu ya ushirika ianze kufundishwa mashuleni,”

Hayati Benjamin Mkapa,akizindua Mdahalo wa Kitaifa juu ya Maendeleo ya Watanzania, kwenye Uwanja wa Nyamagana Mwanza, 26 Machi, 1999.

Kauli hii ya Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu wa Tanzania aliyefariki Julai 24, 2020 Jijini Dar es Salam, inadhihirisha kuwa aliamini kuwa Vyama vya Ushirika vina mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi na kwa Wanachama wa vyama hivyo kutokana na manufaa na faida zinazopatikana kutokana na uwezekezaji wa aina mbalimbali kupitia Ushirika.

Mchango wa vyama vya ushirika kwenye uchumi unazaa ajira ambapo Ushirika hapa nchini umekuwa ukitoa mchango mkubwa kwenye huduma za jamii kama vile elimu na afya ambapo vyama vimekuwa vikichangia elimu na kujenga hospitali jambo ambalo lina uhusiano mkubwa na ukuzaji wa uchumi na ajira kwa wananchi.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC),Dkt.Benson Ndiege anasema kuwa Jumuiya ya Wanaushirika na wadau wa Ushirika nchini Tanzania na Duniani Kote wataeendelea kumkumbuka Hayati Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu kwa juhudi zake katika kufufua, kuimarisha na kuendeleza ushirika hapa nchini.

“Kwa hakika wanaushirika na Wadau wote wa ushirika nchini tumepokea taarifa za msiba huu kwa masikitiko makubwa sana. Tutaendelea kumkumbuka Hayati Benjamini Mkapa kama shujaa na mshika maono katika mageuzi ya Ushirika hapa nchini.

Tutaendelea kumkumbuka na kumuenzi kwa mageuzi aliyoyafikiria na kuyaona katika sekta ya ushirika hapa nchini,” anasema Dkt.Ndiege.

Hayati Benjamini Mkapa alipoingia madarakani mwaka 1995 alifanya mikutano mbalimbali na viongozi wa Serikali na Wanaushirika ili kujadili mipango mbalimbali itakayosaidia kuleta mapinduzi ya kilimo, mifugo na uvuvi kupitia Sekta ya Ushirika.

Watafiti na waandishi wengi katika masuala ya ushirika hapa nchini akiwemo Jovi Banturaki waliweza kunukuu sehemu ya hotuba yake aliyoitoa katika mkutano uliofanyika Mwanza mwaka 2000 ambapo Hayati Benjamini Mkapa alionesha waziwazi nia yake ya dhati juu ya umuhimu wa kufufua na kuimarisha ushirika nchini kuwa ni hitaji la haraka (urgent need) kwa ajili ya kuwezesha wananchi kupambana kikamilifu na umaskini.

Akizungumzia jitihada zilizofanywa na Hayati Benjamini Mkapa katika kuimarisha Ushirika, Mratibu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi – Tawi la Dodoma, Bahati Rukiko, anasema kuwa Rais Mkapa aliteua Tume tatu ili ziweze kuhusika na zoezi la kufufua ushirika.

Tume ya kwanza ilikuwa inahusika na kumshauri Rais kuhusu kufufua, kurekebisha na kuimarisha vyama vya Ushirika, Tume ya pili ilikuwa ni ya kufuatilia kesi mbalimbali za vyama vya ushirika na tume ya tatu ilihusika na kuangalia jinsi vyama vikuu vya ushirika Mkoani Kagera visiweze kufilisiwa na mabenki.

“Tume zote tatu zilifanya kazi kubwa amabapo matokeo ya juhudi hizo yanaonekana hadi sasa.

Ninapenda kuelezea hasa matokeo ya Kamati Maalum ya Rais ya Kumshauri Juu ya kufufua, Kuimarisha na Kuendeleza Ushirika Tanzania iliyoongozwa na Marehemu Sir.

Geoge Kahama ambapo ilikuja na mambo 10 iliyoyaita matatizo sugu ya ushirika Tanzania,” anasema Rukiko.

Matatizo yaliyobainishwa ni pamoja na ushirika usiokidhi mahitaji ya wanachama, ukosefu wa mitaji, uongozi mbovu, ubadhilifu na wizi katika ushirika, muundo duni wa ushirika, udhaifu wa Taasisi za Serikali zinazohusika na maendeleo ya ushirika, elimu duni ya ushirika, kasoro katika utekeleaji wa sera ya soko huru na uwezo mdogo wa ushindani wa Vyama vya Ushirika, ushirika kutoenea katika sekta mbalimbali za uchumi, ushirika kutopewa kipaumbele katika mipango ya Serikali na Sera na Sheria ya Ushirika kutokidhi mahitaji ya wakati.

“Tunampongeza Hayati Mkapa kwa kushughulikia matatizo sugu ya ushirika na kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Ushirika hapa nchini, mojawapo ya jitihada zilizofanywa na Serikali yake ni kuanzishwa kwa Wizara ya Ushirika na Masoko, kutungwa kwa Sera mpya ya Maendeleo ya Ushirika ya Mwaka 2002, Sera ambayo inatumika hadi sasa;

Kutungwa kwa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 20 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za Mwaka 2004,” anasema Rukiko.

Hata hivyo, ili kuleta mapinduzi ya katika sekta ya Ushirika baada ya kurekebisha Sera na Sheria za ushirika, ilitayaarishwa Programu ya Mageuzi na Modenizesheni ya Ushirika (2005- 2015), ambapo lengo lake kuu ilikuwa:

Kuwa na Vyama vya Ushirika vinavyoundwa kutokana na mahitaji ya wanachama na kusimamiwa na wanachama wenyewe. Programu hii ilitekelezwa kwa kipindi cha miaka kumi (10) kuanzia mwaka 2005 hadi 2015. Awamu ya kwanza ya utekelezaji wake ulianza mwaka 2005 hadi 2010 ambapo mkazo ulikuwa katika kuimarisha Vyama vya Ushirika vya msingi kwa lengo la kukidhi mahitaji ya wanachama wake kiuchumi na kijamii.

Aidha, Kamati Maalum ya kumshauri Rais ilibaini udhaifu wa Taasisi za Serikali zinazohusika na Maendeleo ya Ushirika, ambapo kwa wakati huo Ushirika ulikuwa chini ya Wizara ya Kilimo na Ushirika na Taasisi zilizokuwa zinahusika na maendeleo ya Ushirika zilikuwa ni iliyokuwa Idara ya Maendeleo ya Ushirika (Msimamizi wa Utekelezaji wa Sera na Sheria ya Ushirika), kilichokuwa Chuo cha Ushirika Moshi (kilikuwa na Jukumu la kutoa Elimu ya Ushirika) na Shirika la Ukaguzi wa Hesabu za Vyama vya Ushirika- COASCO.

Badhi ya dosari zilizobainishwa na tume hiyo ni pamoja na upungufu wa watumishi, upungufu wa nyenzo za kufanyia kazi, mwingiliano wa majukumu na migongano kati ya taasisi hizo za Ushirika.

Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kama Idara ya Serikali inayojitegemea ilianzishwa chini ya Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya Mwaka 2013 kwa lengo la kusimamia na kuhamasisha ushirika hapa nchini.

Hii ni mojawapo ya jitihada za kuimarisha muundo wa Kitaasisi katika Usimamizi wa Vyama vya Ushirika hapa nchini.

Ushirika ulinzishwa hapa nchini mika ya 1920 wakati wa Ukoloni kwa ajili ya kupambana na unyonyaji uliokuwa unafanywa na wakoloni hasa katika mazao ya biashara kama vile kahawa pamba, chai, mkonge n.k.

Vuguvugu hilo lilisababisha kutambuliwa kisheria kwa vyama vya ushirika katika Mkoa wa Kilimanjaro, na kisha lilienea katika Mikoa mingine baada ya kutungwa kwa Sheria ya Ushirika ya Kwanza ya Mwaka 1932.

Sheria hiyo iliendelea kufanya kazi hata baada ya uhuru hadi mwaka 1968 ilipotungwa sheria nyingine ya ushirika. Kwa ujumla historia ya maendeleo ya ushirika katika nchi yetu imeshuhudia hali ya kupanda na kushuka kwa ushirika kutokana na sababu mbalimbali hasa za kisera.

Baada ya uhuru, Azimio la Arusha la Mwaka 1967 lilikuwa na lengo la kuwezesha Watanzania walio wengi kufikia maendeleo ya uchumi wa kijamaa kupitia mkakati wa kuanzishwa kwa vyama vya ushirika.

Hivyo sheria ya ushirika ya mwaka wa 1968 ilibadilishwa mara kadhaa ili kuifanya iwe na sura ya ‘ushirika wa kijamaa’.

Harakati hizo zilifikia kilele mwaka 1975 ilipotungwa sheria ya Vijiji na Vijiji vya Ujamaa, ambayo ilikuwa ilifanya wanavijiji wote katika vijiji kuwa wanachama wa vyama. Mwelekeo huu uliendelea hata baada ya kurejeshwa kwa sheria za vyama vya ushirika za miaka ya 1982 na 1991.

Hata hivyo kutokana na mageuzi ya sera za kiuchumi ulimwenguni na kupanua uchumi wa soko huru kuanzia miaka ya 1980 hadi 1990 iilifanya maandeleo ya Vyama vya Ushirika nchini kurudi nyuma kwa kiasi kikubwa sana hasa vyama vya ushirika wa Masoko ya mazao ya kilimo.

Matokeo ya sera za kiuchumi ambapo pamoja na mambo mengine zililenga kuondoa uthibiti wa bei za mazao, kuondoa ruzuku na kuerekebisha masuala mbalimbali ya utoaji wa mikopo na ubinafisishaji wa mashirika ya umma ili kuwezesha utawala wa soko huru. Kutokana na hali hiyo, Makampuni mengi ya ndani na nje ya nchi yalijitokeza katika ununuzi wa mazao.

Mabadiliko hayo ya kiuchumi yalisababisha vyama vingi kushindwa
kukabiliana na ushindani kwa kuwa havikuwa vimendaliwa vyema kukabiliana na mabadiliko hayo ya kiuchumi.

Matokeo yake vyama vingi hasa vyama vikuu vilianza kufanya kazi ya uwakala wa Makampuni binfasi na kwa sehemu kubwa Vyama vya Ushirika viliendelea kuwa sinzia.