Na George Mwigulu, Timesmajira Nsimbo.
Mkandarasi wa Kampuni ya Planco (T) Ltd ameanza kuchukua hatua za kuhakikisha analipa madai ya fedha ya zaidi ya milioni 3, kwa vibarua ambao walichimba mitaro kwenye ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Katambike Kata ya Ugalla Halmashauri ya Nsimbo Wilaya Mpanda mkoani Katavi.
Hatua hizo ni matokeo chanya ya ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Mwanamvua Mrindoko alioifanya Februari 16,2024 katika halmashauri hiyo ya kukagua ujenzi miradi ya maendeleo ambapo wakati akisikiliza kero za wananchi liliibuka suala la ucheleweshaji wa malipo ya fedha kwa vibarua.
Mrindoko alichukua hatua ya kutoa maagizo kwa kampuni Planco (T) Ltd kuhakikisha ndani ya siku saba inawalipa fedha hizo na ifikapo Aprili mwaka huu ujenzi wa mradi wa maji Katambike unakamilika kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wanaopata tabu ya maji kwa muda mrefu.
Othman Dunga, Mkurugenzi wa kampuni hiyo akizungumza ofisini kwake Februari 18,mwaka huu amekili kupokea agizo hilo na amechukua hatua tayari za haraka za kuhakikisha malipo hayo yanafanyika.
Mkurugenzi huyo ametoa tangazo tayari kwa vibarua wote wa ndani na nje ya Mkoa waliofanya kazi ya kuchimba mitaro kuhakikisha ifikapo siku ya Alhamisi Februari 22, 2024 wanafika kwenye eneo la mradi Katambike kwa ajili ya kuanza kufanya malipo.
“Ni kweli kampuni yangu inadaiwa na vibarua kwa bahati mbaya walio wengi baadhi yao wako nje ya Mkoa wa Katavi walikuja kufanya kazi na wakaondoka kwaio ili waweze kulipwa tumetoa agizo na tumeshawapa taarifa wafike siku ya Alhamisi kwenye site Katambike ili kila moja aweze kupata haki yake,”amesema.
Amesitiza kuwa watapima kila sehemu ambayo kibarua amefanya kazi kwa ajili ya kila mmoja alipwe fedha kutokana na kazi alizozifanya na kwamba agizo la Mkuu wa Mkoa halina tatizo na litatekelezwa kama jinsi alivyoagiza.
Dunga amebainisha licha ya mkataba wake wa ujenzi wa mradi wa maji Katambike unamwelekeza kuhakikisha ifikapo Aprili mwaka huu kuwa amemaliza ujenzi huo lakini kwa juhudi anazofanya mradi huo utakamilika Machi.
“Namwakikishia Mkuu wa Mkoa wa Katavi na wananchi wa kijiji cha Katambike na Kata ya Ugalla kwamba mradi huo utakamilika ndani ya mwenzi ujao wa Machi na wananchi wote watapata huduma ya maji,sasa tunachofanya kampuni ipo kazini na mimi sitaondoka na sijaondoka mkoani Katavi hadi mradi huu ukamilike,”amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Mwanamvua Mrindoko anaendelea na ziara yake katika ambapo amekuwa akikagua utekelezaji wa ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo na kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.
More Stories
Tanzania,Uturuki kushirikiana kuinua sekta ya utalii nchini
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu