November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkandarasi atakiwa kuongeza kasi mradi wa barabara Buswelu uliofikia asilimia 28.72

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Mradi wa ujenzi wa barabara za Buswelu-Nyamadoke-Nyamhongolo na Buswelu-Busenga-Cocacola zenye urefu wa kilomita 12.8,umefikia asilimia 28.72,huku Mkandarasi kampuni ya Nyanza Road Works akitakiwa kuongeza kasi ili ukamilike kwa wakati na ubora.

Mradi huo ulianza kutekelezwa Novemba 19, 2023 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mpango wake wa uboreshaji miundombinu ya miji Tanzania (TACTIC).

Mbunge wa Jimbo la Ilemela,Dkt. Angeline Mabula ametoa rai hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo jimboni humo pamoja na kusikiliza kero za wananchi wa Kata ya Nyamh’ongolo.

“Nimeridhishwa na hatua za ujenzi wa mradi,nimuombe Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi pamoja na kuzingatia ushauri tunaoutoa ikiwa ni pamoja na kutatua kero zinazolalamikiwa na wananchi katika mradi huu kama uwekaji wa njia za mchepuko,”ameeleza Dkt.Angeline.

Kwa upande wake Mratibu wa miradi ya kimkakati na uendelezaji wa majiji TACTIC Wilaya ya Ilemela Mhandisi Juma King’ola ameeleza kuwa mradi wote utagharimu kiasi cha bilioni 23.49 na unatarajiwa kukamilika Februari 2025 na mpaka sasa Mkandarasi ameshalipwa kiasi cha bilioni 3.5.

Naye Mhandisi Mkadiriaji majenzi ambae pia ni mwakilishi wa Mkandarasi anaetekeleza mradi huo,Juma Maro amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo ulikabiliwa na changamoto za mvua, uchelewaji wa uhamishaji wa miundombinu ya maji na umeme pamoja na mabadiliko ya mara kwa mara ya baadhi ya michoro kulingana na uhitaji wa wakati huku akiahidi kukamilisha kwa wakati mradi huo.

Hata hivyo Diwani wa Kata ya Nyamh’ongolo Andrea Nginila amelalamikia vumbi wakati wa ujenzi wa mradi linalosumbua wananchi wake pamoja na kutokuwepo kwa njia za mchepuko za kutosha hivyo kuomba kuongezwa.