Na Penina Malundo, TimesMajira Online
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Mhandisi Elius Mwakalinga amempa siku saba Mkandarasi anayejenga Barabara ya Rudewa-Kilosa, kuja na mpango mkakati wa kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati.
Ametoa agizo hilo juzi baada ya agizo la Rais John Magufuli kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 24.
Juzi Rais Magufuli akiwa katika hafla ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara hiyo, licha ya kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo, ametoa muda wa mwezi mmoja kwa mkandarasi huyo kufanya mabadiliko chanya endapo anataka kuendelea na ujenzi wa mradi huo.
Akizungumza katika kikao cha dharura kati ya Katibu Mkuu Mwakalinga, Wakala wa Barabara nchini (TANROADs) na Mkandarasi Umoja-Kilosa JV, Mhandisi Mwakalinga alimtaka mkandarasi huyo kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa haraka na kwa ubora uliokusudiwa ili kuiwezesha Serikali kuwa na imani na wakandarasi wazawa.
“Hakikisheni mnajenga imani kwa Serikali yenu ili iwaamini na hivyo muweze kupata miradi mingi ya ujenzi hapa nchini na hivyo kukuza uchumi wa nchi na ajira kwa wazalendo,” amesema mhandisi Mwakalinga
Amesema nia ya Serikali ni kuwawezesha wakandarasi wazawa kuwa na uwezo na mtaji na hivyo kujenga miradi mingi ya ujenzi ili fedha nyingi inayolipwa kwa wakandarasi kubaki nchini na kuhuisha uchumi na kukuza ajira za Watanzania.
“Kuungana, uaminifu, uzalendo na kuchapakazi kwa bidii, kutaiwezesha Serikali kutoa miradi mingi ya ujenzi kwa wakandarasi wazawa na hivyo kuwajengea uwezo wa kimtaji, utaalamu na uzoefu na kuongeza ajira kwa Watanzania,” amesema Mwakalinga
Barabara ya Rudewa-Kilosa ni sehemu ya barabara ya Dumila-Kilosa-Mikumi yenye urefu wa Km 142, inayotarajiwa kukamilika Januari mwakani itakapokamilika, barabara hiyo itaunganisha mikoa ya Tanga, Morogoro na Iringa bila kupita mbuga ya wanyama ya Mikumi na hivyo kupunguza ajali katika mbuga hiyo .
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa