May 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mixx by Yas, DSE wazindua Min App kuhusu soko la hisa

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

MIXX by Yas kwa kushirikiana na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), wamezindua rasmi DSE Hisa Kiganjani Mini App, inayopatikana ndani ya Mixx Super App.

Hiyo ni kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na kuwawezesha Watanzania katika safari yao ya kifedha,

Huo ni ushirikiano wa kwanza wa aina yake nchini Tanzania na unaleta zama mpya za uwekezaji jumuishi, ambapo watumiaji kutoka kila kona ya nchi, bila kujali hali au mahali walipo, wanaweza kununua na kuuza hisa kwa urahisi kupitia Mixx Super App.

Akizungumza wakati wa uzinduzi uliofanyika jijini Dar es Salaam leo, CPA Thomas Matogolo Mongella kutoka Benki Kuu ya Tanzania amesisitiza umuhimu wa ubunifu huu kwa maendeleo ya taifa.

“Majukwaa ya kidijitali kama haya ni nyenzo muhimu za kuongeza kina cha masoko ya kifedha nchini na kuwawezesha Watanzania kudhibiti uwekezaji wao.

“Hii inaendana na malengo yetu ya kitaifa ya kuhakikisha upatikanaji mpana wa huduma za kifedha.”DSE Hisa Kiganjani – Mini App, inayopatikana kupitia Mixx Super App, imeondoa urasimu unaotajwa mara kwa mara katika uwekezaji wa soko la hisa.

“Kwa taarifa za wakati halisi za mitindo ya hisa za ndani na nje ya nchi, mchakato rahisi wa usajili, na usalama wa miamala, programu hii inaleta masoko ya mitaji karibu zaidi na wananchi kwa mbofyo mmoja tu,” amesema CPA Matogolo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mixx by Yas, Angelica Pesha ameeleza kwa msisitizo kuhusu athari kubwa za jukwaa hilo jipya.

“Hii si tu kipengele cha kidijitali, ni mapinduzi ya kweli katika uwekezaji nchini. Tunawawezesha Watanzania kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi wao kwa kuwapa uwezo wa kufikia soko la hisa moja kwa moja kutoka kwenye simu zao.

“Tunaamini kuwa ujumuishaji wa kifedha wa kweli ni kuondoa vizingiti na kujenga fursa kwa kila mtu.

DSE Hisa Kiganjani – Mini App, inayopatikana kwa mara ya kwanza ndani ya Mixx Super App kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, ni ushahidi wa dhamira yetu ya kutoa suluhisho la kwanza sokoni ambalo ni rahisi, salama, na jumuishi,” amesema Angelica Pesha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela aliunga mkono kauli hiyo kwa kueleza kuwa ushirikiano huu ni hatua kubwa katika dira ya DSE ya kujenga mfumo jumuishi wa kifedha:“Dira yetu DSE ni kupanua ushiriki na upatikanaji wa masoko ya mitaji.

“Kupitia DSE Hisa Kiganjani – Mini App ndani ya Mixx Super App, tunawawezesha Watanzania wote bila kujali hadhi au eneo walipo, kushiriki moja kwa moja katika safari ya ukuaji wa uchumi wa taifa. Ni salama, rahisi kutumia, na imeundwa kwa kuangalia mahitaji ya sasa na yajayo.

”Uzinduzi huu pia, uliambatana na mjadala wa kitaalamu uliobeba mada, “Mustakabali wa Uwekezaji wa Kifedha Tanzania”, uliogusa masuala ya teknolojia katika kuongeza fursa za uwekezaji hasa kwa vijana, wafanyabiashara wadogo, na makundi yasiyo na uwakilishi mkubwa kwenye masoko ya fedha,” amesema.

Kadri Tanzania inavyozidi kusonga mbele kwenye uchumi wa kidijitali, ushirikiano kati ya Mixx by Yas na DSE ni mfano wa kuigwa wa namna teknolojia inavyoweza kufungua milango ya fursa kwa kila Mtanzania.