December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miundombinu ya TASAF yainua
taaluma Sekondari ya Mlowa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajiraonline, Makambako

MIUNDOMBINU ya nyunba za mbili za walimu (two in one), hosteli ya wanafunzi, jengo la utawala, jiko na bwalo iliyojengwa katika Shule ya Sekondari Mlowa katika Halmashauri ya Mji Makambako mkoani Njombe imepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zilizokuwa zikikabili shule hiyo na kukwamisha utolewaji wa elimu bora.

Miundombinu katika shule hiyo imejengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa sh. 355,433,812.5 na wananchi kuchangia nguvu kazi kwa asilimia zisizopungua 10.

Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea shule hiyo kujionea miumdombinu hiyo ilivyotatua changamoto zilizokuwa zikikabili hiyo Mwalimu Mkuu, Raymond Kyando ameishukuru TASAF, akisema sasa kiwango cha taaluma katika shule hiyo kimepanda ikilinganishwa na kipindi ambacho haikuwa na miundombinu hiyo.

Kyando amesema miradi ya TASAF shuleni hapo ilianza mwaka 2018 kwa ujenzi wa hosteli ya wanafunzi 72, ujenzi wa nyumba za walimu, jengo la utawala.

“Kabla TASAF kutujengea hosteli wanafunzi walikuwa wanatembea mbali kilometa kilometa 24 kwenda na kurudi. Tulibaini watoto wanapata shida ilitulazimu kuweka kambi ambapo tulitenga madarasa mawili ambayo walikuwa wanalala wanafunzi,” amesema Kyando.

Amesema kutokana na changamoto ya uhaba wa hosteli kuwa kubwa wananchi kupitia mkutano wa kijiji waliomba TASAF iwajengee hosteli ambayo imekuwa mkombozi mkubwa tangu ilipojengwa.

Kyando ametoa mfano kwamba kabla ya ujenzi wa hosteli hiyo kila mwaka wanafunzi kati ya wanne hadi watano walikuwa wakipata ujauzito. “Lakini tangu TASAF itujengee hosteli hiyo hatujawahi kuwa na changamoto hiyo kwa sababu hosteli hiyo imelenga wanafunzi wa kike.”

Aidha, amesema tangu kujengwa kwa hoteli hiyo kiwango cha taaluma kimepanda ambapo kwenye mitihani ya ndani na ya nje kwenye kata wanaoongoza ni watoto wa kike wa shule hiyo.

Mwalimu Mkuu, Raymond Kyando

“Hivyo tunaamini kabisa uwepo wa hii hospteli umesaidia watoto wa kike na imewabadilisha kitaaluma na kuwawezesha kuelekea kutimiza ndoto zao, lakini pia vikwazo vingine vimeondoka.

“Ndiyo maana Serikali kuanzia ngazi ya mitaa na kata wakaamua sekondari hii iwe shule ya wasichana na lengo letu ni kuifanya iwe shule teule ya wanafunzi wa kike,” amesema.

Ametaja sababu nyingine iliyochangia utoro ilikuwa ni kukosekana kwa chakula cha mchana. Alisema tangu shule hiyo ilipoanza kutoa chakula cha mchana kwenye bwalo ambalo limejengwa na TASAF nayo imekuwa chachu ya kupunguza utoro.

“Watoto wanaondoka shuleni saa 11 jioni sasa kama hawapati chakula cha mchana kunachangia utoro, hivyo tulianzisha kampeni ya kuwa na chakula cha mchana ambayo pia imepunguza utoro,”alisema.

Kwa upande wa nyumba za walimu zilizojengwa na TASAF, Kyando alisema zimejengwa mbili (Two in one sawa na nyumba nne) ambazo ambapo zimewezesha walilimu kuishi karibu na shule na wamekuwa wakisaidia wanafunzi wakatia wakujisomea usiku.

“Muda wote walimu wanakuwa shuleni wanasaidia wanafunzi wakati wa kujisomea usiku na muda wote wanaweza kuwafundisha,” alisema Kyando. Kuhusu jengo la utawala amesema limesaidia shughuli za kiutawala na walimu wana ofisi nzuri ikilinganishwa na hapo nyuma,”alisema.

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Mlowa wakiendelea na masomo darasani

Naye mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo, Irene Mgunda ameishukuru TASAF kwa kuwajengea hosteli hiyo, kwani imewasaidia kumaliza changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo kabla ya ujenzi huo.

Alitoa mfano kwamba wazazi wake wanaishi Makambako hivyo bila kuwepo kwa hosteli hiyo asingemudu kutembea kwa miguu kwenda shuleni hapo. Alisema ujenzi wa hosteli hiyo umekuwa mkombozi kwani watoto wa kike wanaoishi nyumbani wanakumbana na changamoto nyingi wakati wa kwenda na kurudi shuleni.

Naye Esther John alisema ujenzi wa hosteli hiyo unawasaidia wakati wa usiku kupata muda wa kujisomea tofauti na yule mwanafunzi anayetokea nyumbani kwani anakuwa na majukumu mengi, hivyo anakosa muda wa kujisomea.

“Tunapotaka msaada kutoka kwa mwalimu tunaupata kutoka kwa walimu maana wapo hapa shuleni ni tofauti na mwanafunzi anayetoka nyumbani kuja shule na mara nyingi wanakumbana na vishawishi vingi,” anasema.

Kuhusu nyumba za walimu zilizojengwa na TASAF mwanafunzi huyo amesema nazo zimekuwa mkombozi, kwani wanapokuwa wanajisomea wanapata msaada kwa urahisi kutoka kwa walimu kwa sababu wanakuwepo shuleni.

Naye mlezi wa wanafunzi katika hosteli hiyo, Upendo John (24) alisema ujenzi wa hosteli hiyo umekuwa msaada mkubwa kwa jamii ya Mlowa, hasa ikizingatiwa watoto wanatoka sehemu mbalimbali na wengine wanakopita sio salama na kuna vishawishi vya aina nyingi.

Ametoa mfano wakati mwingine shuleni kuna vipindi vya ziada ambavyo vinawafanya watoke shuleni wamechelewa hivyo vinaweza kuwafanya wafike nyumbani usiku.

“Lakini wanapokuwa hosteli wanakuwa sehemu salama hivyo ni vigumu kupata vishawishi. Hosteli hii imefanya wanafunzi kuwa salama,” amesema Pendo.