Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza imetumia zaidi ya shilingi bilioni tano kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya ikiwemo ujenzi na ukarabati wa zahanati na vituo vya afya kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Emmanuel Shelembi amesema vituo vipya vya afya vilivyokamilika ni Igalla, Murutilima na Ilugwa pamoja na ujenzi wa zahanati za Buguza na Ghana ambapo miradi hiyo itaondoa adha ya wananchi kufuata huduma umbali mrefu.
Shelembi amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha huduma za afya ambapo katika Hospitali ya Bwisa imejenga jengo la ICU lililogharimu shilingi milioni 250.
Pia Shelembi amebainisha kuwa katika kuboresha mazingira ya watumishi, Serikali imejenga nyumba yenye muundo wa kutumika na watumishi watatu (3 in 1) katika kituo cha afya Kagunguli yenye thamani ya shilingi milioni 90 na kukarabati vituo vya afya 24 pamoja na kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
“Visiwa 15 kati ya 38 vya Wilaya ya Ukerewe vinakaliwa na watu hivyo lengo la Serikali ni kufikisha huduma kwa wananchi katika visiwa hivyo na kuwaondolea adha ya kutumia vivuko kufuata huduma hizo” amesema Shelembi.
Mganga Mkuu Wilaya ya Ukerewe, Dkt. Charlse Mkombe amesema pia zahanani mpya nane zimejengwa na hivyo kusogeza karibu zaidi huduma za fya kwa wananchi katika wilaya hiyo ambayo asilimia 90 imezungukwa na maji.
“Lengo la Serikali ni huduma kumfuata mwananchi aliko na siyo wananchi kufuata huduma mbali kwani dharura inaweza kutokea hasa majira ya usiku na wakashindwa kupata huduma kwa wakati. Pia tuna ‘ambulance’ za boti mbili na tuko kwenye mpango wa kuongeza nyingine ili kutoa huduma za dharura visiwani” amesema Dkt. Mkombe.
Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Igalla, Dkt. Jeremia Katwale amesema katika Kituo hicho, Halmashauri kupitia mradi wa WASH imetatua changamoto ya uhaba wa maji baada ya kujenga tenki la chini lenye ujazo wa lita elfu 50 kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua, kujenga eneo la kunawia mikopo pamoja na ujenzi wa kichomea taka.
“Wananchi hususa akina mama watakaofika hapa kujifungua sasa wataondokana na adha ya uhaba wa maji baada ya mradi huu wa WASH kukamilika” amesema Dkt. Katwale.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Igalla, Obedi Mkingila amesema kukamilika na kuanza kutumika kwa kituo cha afya Igalla kutaondoa adha kwa wananchi wa Kata ya Igalla ambao hutumia usafiri wa pikipiki kufuata huduma za afya katika kituo cha afya Muriti.
“Akina mama wajawazito tunapata changamoto kutembea umbali mrefu hadi kituo cha afya Muriti. Tumefurahi ujenzi wa kituo chetu cha hapa Igalla umekamilika na tunasubiri kwa hamu kuona kinaanza kufanya kazi” amesema mkazi wa Igalla, Nyakwesi Katula.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mganga Mkuu Wilaya ya Ukerewe, Dkt. Charlse Mkombe akieleza kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya.
Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Igalla, Dkt. Jeremia Katwale akieleza namna mradi wa WASH umefanikisha kuondoa adha ya uhaba wa maji katika kituoni hapo baada ya ujenzi wa tenki la chini kwa ajili ya uvunaji maji ya mvua ambalo lina ujazo lita elfu hamsini.
Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Muriti, Dkt. Daniel Matekele akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mradi wa WASH ambao umefanikisha ujenzi wa miundombinu ya maji kituoni hapo.
Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Igalla, Dkt. Jeremia Katwale akionesha tenki la chini kwa ajili ya uvunaji wa maji ya mvua.
Mwonekano wa kichomea taka katika Kituo cha Afya Igalla kilichojengwa kupitia mradi wa WASH.
Mwonekano wa eneo la kunawia mikono (kulia) katika Kituo cha Afya Igalla lililojengwa kupitia mradi wa WASH ili kuimarisha hali ya usafi kwa wananchi na watumishi wanaofika kituoni hapo hatua itakayosaidia kujikinga na maradhi mbalimbali.
Mwonekano wa eneo la kunawia mikonokatika Kituo cha Afya Igalla.
Mwonekano wa eneo la kunawia mikono katika Kituo cha Afya Muriti.
Mganga Mkuu Wilaya ya Ukerewe, Dkt. Charlse Mkombe akinawa mikono alipowasili katika Kituo cha Afya Muriti.
Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe wakinawa mikono baada ya kuwasili katika Kituo cha Afya Muriti kukagua miundombinu ya maji iliyokamilika kupitia mradi wa WASH.
Mwonekano wa juu wa majengo mbalimbali katika Kituo cha Afya Igalla kilichopo Ukerewe mkoani Mwanza.
More Stories
Maandalizi ya mkutano mkuu CCM yapamba moto
Jela miezi sita kwa kuvaa sare za JWTZ
Watolewa hofu uvumi juu ya uwepo wa Teleza