December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mitambo ya kisasa ya kuzalisha zege kuongeza kasi ya ufanisi SUMAJKT

Na Joyce Kasiki,Timesmajira,Dodoma

MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele amelitaka Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) kuhakikisha linafanya kazi kwa weledi ili kuendelea kuwapa imani wadau wanaowapa kazi kwamba wanaweza kufanya kazi zao kwa viwango vinavyokubalika na kwa ubora zaidi.

Meja Jenerali Mabele ameyasema hayo leo Mei 23,2023 jijini Dodoma wakati akizindua magari na mitambo ya kuzalisha zege ambayo itatumika katika miradi wanayozalisha lakini pia kuwauzia wahitaji wengine katika jiji la Dodoma.

Ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali  ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliamini shirika hilo kwa kulipa kazi huku akiahidi kuendelea kununua vifaa vya kisasa ili kufanya kazi zenye ubora zaidi.

“Tunaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kutuamini na kutupa kazi  na ndiyo maana mnaona na sisi tunapambana  ili kuhakikisha tunakuwa na mitambo ili tuweze kuzitekeleza kazi hizo kwa ufasaha,kwa wakati na vizuri zaidi.”amesema Meja Jenerali Rajab Mabele  na kuogeza kuwa

“Kwa imani hii tunayopewa na Serikali,watendajiwote wa SUMAJKT lazima tuonyeshe kwamba wale wanaotuamini hawajakosea,kwa hiyo tufanye kwa kazi kwa bidii ili kuhakikisha imani ile ile tunayopewa na sisi tuendelee kuonyesha kwamba tupo tayari kwa ajili ya kutekeleza majukumu mbalimbali ya serikali ,tufanye kazi kwa wakati,kazi zenye viwango kama ambavyo tunafanya siku zote tuendelee kuwa na bidii  katika majukumu yetu ya kila siku.”

Aidha ametaka mitambo hiyo itunzwe kwa kufanyiwa ukarabati wa mara kwa mara kila inapohitajika na kwa wakati muafaka ili iendelee kuwa endelevu la kuleta faida ndani ya shirika na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT Kanali Petro Ngata amesema, tukio hilo ni moja ya utekelezaji wa mikakati yao waliyojiwekea ya kuongeza mitambo na vitendea ili kujiongezea uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Awali akitoa taarifa ya mtambo huo Mkurugenzi Mwendeshaji kampuni ya Ujenzi SUMAJKT  Injinia Mogan Nyoni amesema vifaa vilivyozinduliwa vimegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.349 huku akisema  zoezi la usimikaji hadi kufikia Mei 22 mwaka huu  lilikuwa limefikia asilimia  95.

“Kukamilika kwa usimikaji wa mitambo hiyo utaongeza kipato cha kampuni ya ujenzi na shirika kwa ujumla kwani hitajio la zege jijini Doodma ni kubwa lakini pia kutaongeza imani za kiutendaji kutoka kwa washitiri  kutokana na kazi ambazo SUMAJKT na kampuni ya Ujenzi inafanya .”alisema Injia Mogan

Kwa upade wake Mwenyekiti wa Bodi SUMAJKT amesema ,mitambo hiyo itaongeza thamani katika shirika kutokana na ubora wa bidhaa zinazozalishwa,urahisi wa upatikanaji wake ,gharama za uzalishaji kupungua  lakini pia muda wa uzalishaji utapungua.