January 27, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Misungwi yajivunia miaka 47 ya CCM

Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Misungwi

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Misungwi,mkoani Mwanza,kimeadhimisha miaka 47 ya kuzaliwa kwa chama hicho huku kikijivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta mbalimbali, maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanaonekana kwa macho.

Pia,kimeridhishwa na namna ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2025 ilivyotekelezwa na serikali kuwa imeutendea haki Mkoa wa Mwanza kwa miradi ya maendeleo ya wananchi ikiwemo ya kimkakati.

Kauli hiyo ilitolewa wilayani Misungwi na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza,Michael Masanja (Smart),wakati akihutubia wananchi na wanachama wa chama hicho katika maadhimisho ya miaka 47 ya CCM ngazi ya Wilaya yaliyofanyika Kijiji cha Mabuki wilayani humo.

“Mwanza miaka 47 ya CCM tumeona mafanikio mengi ya maendeleo ya wananchi katika sekta mbalimbali na kiuchumi,tuna miradi ya kimkakati ya meli kubwa ya abiria na mizigo,daraja la JPM limefikia asilimia 82 ambalo Rais Samia wakati anaingia madarakani lilikuwa asilimia 28 na stendi za mabasi Nyegezi na Nyamh’ongolo zimekamilika,”amesema Smart na kuongeza;

“Reli ya SGR ujenzi unaendelea,ujenzi wa jengo la abiria la uwanja wa ndege na uboreshaji wa uwanja huo Mkandarasi ameishapatikana na mkataba utasainiwa karibuni ambapo ukikamilika ni fursa kwa wananchi.”

Amesema dhamira ya Rais Samia ni kuzalisha wafanyabiashara mamilionea wapya kupitia sekta za uvuvi na mifugo ambapo kazi kubwa imefanyika kwa serikali kuleta ng’ombe wa kisasa 500 wazalishwe na kupewa wafugaji na hivi karibuni wavuvi Mwanza walipewa boti 55 huku wengine 989 wakinufaika kwa vizimba vya kufugia samaki.

“Yote hayo ni mafanikio yaliyoletwa na Dkt.Samia, tunastahili kumpongeza,ameruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa,amefanya mabadiliko ya sheria ya uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa,amewarejesha nchini wakimbizi wa kisiasa na ameanzisha maridhiano ya kisiasa kupitia falsafa yake ya 4R, hivyo asiyeyaona hayo tutambue ni kipofu,”amesema Smart.

Amesema changamoto ya dhuluma ya ardhi, ukosefu wa malisho ya mifugo na mitaji ya biashara ya ujasirimali,serikali inaendelea kuzitatua na kwamba CCM inajivunia uimara wake unaotokana na mizizi na misingi iliyoasisiwa na vyama vya TANU na ASP.

Akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa amesema kazi kubwa kwa wana Misungwi ni kuongeza idadi ya wanachama wakizingatia mtaji wa biashara ni faida ili kuongeza kipato na mtaji wa siasa ni wanachama,hivyo wajisajili katika daftari la kudumu la wapiga kura,kujenga uwezo wa watendaji na wanawake wajitokeze kugombea nafasi za uongozi.

Naye Katibu wa chama hicho Mkoa wa Mwanza,Omar Mtuwa amesema miaka 47 bado CCM kiko imara,kina mvuto na kitaendelea kuwa na mvuto kwa wananchi kutokana na kujipambanua kwa kazi nzuri ilizofanya za kuleta maendeleo.

Diwani wa Kata ya Usagara (CCM) Erasto Machibya kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi,John Chacha,amesema wananchi wa Wilaya hiyo wanaona fahari ya kuadhimisha miaka 47 wameziona fedha za miradi ya maendeleo hawakuwahi kuziona katika sekta za elimu na afya.

“Misungwi tunamshukuru Rais Dk.Samia,mwaka 2022/23 hadi Juni tulipokea kiasi cha bilioni 53.7 sawa na asilimia 98.3 kati ya bilioni 54.Sekta ya afya Aprili 2021 wakati akipokea nchi alitoa kiasi cha bilioni 3.08 za kujega hospitali ya Wilaya,mwaka 2022 Usagara ilipokea kiasi cha milioni 500 za kituo afya,bilioni 2.9 za madarasa pia 2023 alitoa fedha zingine za madarasa 44, kiasi cha bilioni 1.08 za kujenga shule mpya mbili,”amesema.

Awali Katibu wa CCM wa Wilaya ya Misungwi,Nyalukuru Mwita Nyahingi,amesema wana jumla ya wanachama 80,801 kati yao 39,280 ni wanaume na wanawake 45,521 huku wanachama 20,020 kati ya 35,000 wakiwa wamesajiliwa katika mfumo wa kielektroniki,tumesajili wengine wapya 21,200 na hali ya kisiasa ndani ya chama iko shwari.

“Wilaya ya Misungwi si wapweke kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa tuna wanachama zaidi ya nusu ya wapiga kura, hivyo tuna uhakika vijiji 115 na vitongoji 700 vitabaki CCM na tayari tumepokea kadi 5,483 za wanachama kutokana na maelekezo ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC),”amesema.

Katibu huyo wa CCM Misungwi amesema; “Uchaguzi ukifika wenye sifa jitokezeni kuchukua fomu na kamati itatenda haki,viongozi watoe fomu zisitolewe kwa matakwa ya watendaji kwa watu wao wanaowataka lakini wenye makundi ya maslahi tunayakemea ili kuepuka kukigawa chama.