NA DAUD MAGESA, MWANZA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza,inachunguza miradi 15 ya elimu,afya na maji yenye thamani ya bilioni 50.6 iliyobainika kuwa na kasoro kubwa.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza,James Ruge amesema leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba,mwaka jana.
Amesema katika kipindi cha miezi mitatu Oktoba hadi Desemba mwaka jana,walifuatilia miradi 38 ya maendeleo yenye thamani ya bilioni 85.94 na kubaini kati ya hiyo, miradi 15 yenye thamani ya bilioni 50.6 katika wilaya za Magu,Misungwi,Ilemela na Ukerewe ilikuwa na dosari kubwa.
Ruge amesema ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi hiyo ya maendeleo ulilenga kufahamu ubora na thamani ya fedha iliyotumika, kati ya miradi hiyo 38 iliyokaguliwa,15 ilikutwa na mapungufu kutokamilika kwa wakati,matumizi ya vifaa visivyo na ubora yaliyosababisha majengo kujengwa chini ya kiwango na hivyo kusababisha nyufa.
Amesema kutokana na kasoro hizo wanachunguza mradi wa maji Ukiriguru unaogharimu zaidi ya bilioni 38.37 ukidaiwa mchakato wa kumpata mkandarasi ulikiuka taratibu za manunuzi na uchunguzi mwingine unafanyika katika mradi wa maji Kigongo wenye thamani ya bilioni 6.5 ambao umechelewa kukamilika kwa wakati.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya TAKUKURU Wilaya ya Misungwi inaongozwa kwa miradi yenye kasoro kubwa yenye thamani zaidi ya bilioni 47.7 ambayo ni ya maji na elimu huku Wilaya ya Magu yenye miradi elimu na afya inayogharimu bilioni 1.5,Ukerewe na Ilemela zenye miradi ya milioni 584.28 kila moja katika sekta ya elimu.
“Tumeanzisha uchunguzi kwa miradi iliyobainika kuwa na kasoro kubwa na miradi iliyokuwa na mapungufu madogo ushauri wa kurekebisha mapungufu hayo umetolewa na kuwezesha kukamilika thamani ya fedha ionekane,”ameeleza Ruge.
Pia, taasisi hiyo katika kuzuia rushwa nchini,inafanya uimarishaji wa mifumo ya utendaji kazi wa taasisi za serikali,umma na binafsi kwa kufanya uchambuzi wa mifumo,vikao vya warsha na kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yanayotokana na vikao hivyo.
Ruge amesema kufanya kazi hiyo kunalenga kubaini mianya ya rushwa na kushauri namna ya kuiziba mianya hiyo ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuzuia vitendo vya rushwa.
“Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka jana, TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, ilifanya uchambuzi wa mfumo wa kutoa huduma katika sekta ya ardhi nchini ikilenga kutathmini uzingatiaji wa sheria, kanuni na miongozo ya utoaji huduma za sekta hiyo ili kubaini mianya ya rushwa,”amesema.
Ameeleza kuwa walifanya kazi hiyo wakijikita kuangalia eneo la kupima ardhi,kumilikisha na kusajili ardhi,kuthaminisha ardhi,utoaji wa vibali vya ujenzi na utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Ruge ameeleza zaidi kuwa walibaini wataalamu kutozingatia huduma kwa mteja wa Wizara ya Ardhi inayotamka siku anazotakiwa kutumia mwananchi (mteja) kwa huduma anayoihitaji,milolongo mirefu ya utoaji huduma za ardhi,uchache wa watumishi wa idara hiyo kwa halmashauri baadhi na wananchi kushindwa kulipa malimbikizo ya kodi za ardhi.
Pia,uelewa duni wa wananchi wa matumizi ya ardhi wanapohitaji kubadilisha matumizi,waliopimiwa kushindwa kuchukua hati kwa wakati,upungufu wa mfumo wa serikali unaotumika kutoa huduma za ardhi.
Mengine waliyoyabaini ni ukosefu wa vitendea kazi kwa watumishi wa idara hiyo,halmashauri kukosa fedha za kulipa fidia ya maeneo ya kupisha upimaji wa viwanja na kutokuwa na viwanja vilivyopimwa vya kutosha kuwapatia wananchi.
Ruge amesema mapungufu hayo na mengi yaliyobainishwa yanasababisha kuendelea kuwepo kwa vitendo vya rushwa na malalamiko yasiyoisha katika utoaji huduma wa sekta ya ardhi,hivyo watafanya vikao na watendaji wa halmashauri za Mkoa ili kutoa matokeo ya kazi iliyofanyika,kupanga mkakati na kuweka maazimio ya kutatua kero zilizobainishwa katika uchambuzi wa mfumo.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito