Na Stephano Mango,TimesMajira online
HIVI karibuni Rais Samia alikutana na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa niaba ya wazee wote nchini ambapo mambo mbalimbali yalijitokeza katika kikao hicho cha wazee baada ya Mwenyekiti wa Baraza la wazee wa mkoa huo Salum Matimbwa kuelezea changamoto ambazo zinawakabili.
Rais Samia alisema matatizo waliyowasilisha na wazee hao ameyachukua na atayafanyia kadri itakavyowezekana ili wazee hao waishi kwa amani kwasababu walishalitumikia taifa katika shughuli mbalimbali walipokuwa katika majukumu yao kabla hawajawa wazee.
Pia anasema kuwa yeye ameshaingia uzee hivyo nilazima awekeze katika utatuzi wa changamoto ambazo zinawakabili wazee ili naye aje aishi katika mazingira mazuri ya uzee hayo ni hakika kuwa ni maneno ya faraja na yameongeza matumaini ya utatuzi wa kero zinazowasumbua wazee katika maisha yao ya uzeeni.
Alipokuwa kwenye kambi ya wazee Nunge alisikika akisema “Ni imani yangu kuwa endapo watu wote tutajitoa kwa dhati tutaweza kuwahudumia wazee na watu wasiojiweza na hivyo kuwapunguzia makali ya maisha . Tukumbuke ‘kutoa ni moyo na si utajiri’ na kwamba “sisi sote ni wazee na walemavu watarajiwa”.
Serikali ina wajibu mkubwa katika kuhudumia wazee na watu wasiojiweza hivyo Serikali pekee haiwezi kumaliza matatizo yote yanayowakabili wazee na watu wasiojiweza, hivyo basi,sote kwa pamoja tunao wajibu wa kusaidia nguvu za Serikali katika kuwahudumia watu hao.
Hivyo kipimo kimojawapo cha kupima jamii iliyostaarabika na inayoheshimu misingi ya utu ni kuangalia namna inavyo wathamini wazee na watu wasiojiweza,kwa sababu wazee na watu wasiojiweza wanahitaji upendo, kuthaminiwa nakusaidiwa katika jamii zetu.
Hakika ni maneno mazito na ya faraja sana kwa wazee na watu wasiojiweza nchini hivyo kila mwananchi anawajibu wa kutambua kwamba bila wazee hakuna tutakachoweza kufanya hivyo ni muhimu kuwa enzi na kuwasaidia wazee walioko majumbani na mitaani.
Akizungumzia kitendo hicho Katibu Mkuu wa Mtandao wa Kinga Jamii Nchini (TSPN) Iskaka Msigwa alipongeza kitendo hicho kilichofanya na Rais Samia na kumuomba sasa aone umuhimu wa kuendeleza harakati za kuwathamini wazee na watu wasiojiweza kwa utengamano wa jamii na maendeleo ya uchumi wa taifa.
Msigwa anasema kuwa Tanzania Social Protection Network(TSPN) ni muungano wa mashirika 34 yasiyo ya kiserikali yaliyosajiliwa kisheria kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara na Visiwani yanayojishughulisha na kuwahudumia wazee,watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali na watoto waishio katika mazingira hatarishi na kwamba mtandao huo uliundwa rasmi mwaka 2010
“Wizara ya Kazi,Ajira na Maendeleo ya Vijana kwa kushirikiana na Shirika la Help Age International Ofisi ya Tanzania mwaka 2009/2010 waliendesha utafiti wa kina juu ya uwezekano wa Tanzania kuanza kutoa pensheni kwa wazee wote nchini”alisema Msigwa
Ripoti ya utafiti huo ilizinduliwa na Waziri wa Wizara hiyo Juni 30, mwaka 2010 ambapo wataalam wa utafiti huo walionyesha wazi uwezekano wa wazee wote milioni 2.1 kulipwa pensheni kwani watatumia 1.28% ya GDP ya pato la taifa
Kitendo cha Serikali kutambua umuhimu wa kuwalipa pensheni wazee ni cha thamani sana kwani kimeonyesha kujari juhudi za wazee hao kulijenga taifa lao walipokuwa na nguvu kabla hawajazeeka
Msingi wa kuwepo pensheni jamii kwa wazee wote unatokana na haki,sera na hali halisi na changamoto zinazowakabili wazee katika maisha yao ya uzeeni na ndio maana utafiti ulifanyika na kuthibitisha faida zake katika kupambana na umaskini na maradhi na hapa ndipo serikali inatakiwa itoe kinga jamii na pensheni jamii kwa wazee hao
Kinga jamii ni hatua au tendo la Serikali au jamii kutoa usaidizi wa moja kwa moja kwa watu ili kuwawezesha kukabiliana na majanga, hali ya kutojiweza na umaskini,kukosa ajira,ugonjwa,uzee au kufiwa na wategemezi hapo ndio Serikali inawajibika kutoa fedha ili kunusuru uwepo wa majanga
Kwa muktadha huo Pensheni jamii ambayo wazee wamekuwa wakiitaka serikali iwape ni utaratibu wa kumpatia mzee fedha taslim kila baada ya muda uliokubaliwa inawezekana ikawa kila mwezi, kila miezi miwili au robo mwaka
Ni dhahiri kuwa kinga jamii ni haki ya mtu na ndio maana tangazo la haki za binadamu la mwaka 1948(Universal Declaration of Human Rights) kwenye ibara ya 22 inatamka kuwa kila mtu ana haki ya hifadhi ya jamii
Na ibara ya 25 inatamka haki ya hifadhi ya jamii wakati wa uzee na hata maelekezo ya kisera nchini pia inatambua haki ya kinga jamii na hifadhi jamii kwa mfano Katiba ya Nchi ibara ya 11(1) na MKUKUTA II ukurasa wa 81 lengo la 6 na sera ya taifa ya hifadhi ya jamii, hizi zote ni juhudi njema za Serikali za kuboresha maisha ya wazee
Kwa mujibu wa Sera ya Wazee nchini, mzee ni mtu mwenye umri wa miaka 60 au zaidi na ripoti ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inaonyesha kuwa kundi hili linahusisha asilimia 5.6 ya watu wote takriban milioni 45 waliopo nchini.
Na katika muda huo watumishi wa umma na taasisi zake hufikia umri wa kustaafu ajira zao na wale wasio katika mfumo wa ajira rasmi pia hufikia hatua ya kupunguza majukumu ya kazi zao kwasababu ya umri, hivyo suala la uzee na kuzeeka ni dhana inayoelezea hatua ya mwisho ya makuzi ya binadamu yeyote baada ya kupita katika hatua muhimu za utoto na ujana.
Serikali iliandaa Sera yenye lengo la kutambua changamoto zinazowakabili wazee, kwa kuwa ilitambua kuwa wazee ni rasilimali muhimu katika maendeleo ya taifa na ikasisitiza umuhimu wa kutengwa kwa rasilimali za kutosha kwa lengo la kuboresha huduma kwa wazee; kuwashirikisha wazee katika maamuzi muhimu yanayowahusu wao na taifa kwa ujumla na kutoa ulinzi wa kisheria kwa wazee kama kundi maalum, hayo yote yanaelezwa kwenye aya ya 1.3 ya sera hiyo.
Umuhimu wa pensheni jamii kwa wazee ni kumwezesha mzee kuwa na uhakika na pato ambalo umwezesha kujipatia huduma za lazima na kuzifikia huduma nyingine za msingi zinazopatikana kwenye mazingira yake
Huandaa nguvu kazi bora ya taifa na huinua soko la ndani ya jamii kwa kuchochea kuwekeza katika uzalishaji na kuleta mshikamano wa kijamii na kuboresha mahusiano kati ya serikali na wananchi
Huwawezesha wazee kujiamini na kuwarudishia heshima au madaraka yao ya asili kwani familia zitaanza kuwapenda wazee na kuwatunza kutokana na fedha watakazokuwa wanapata kama pensheni ya uzeeni
Wazee wakipewa pensheni itawapa unafuu wa maisha wa kumudu mambo ya msingi, kwa kuwa wazee nao walishiriki ujenzi wa taifa kwa namna moja ama nyingine bila kujali alikuwa ni mfanyakazi katika sekta rasmi au la
Katika maisha ya jamii ya kila siku wazee wanakubalika kuwa ni kisima cha ujuzi katika masuala mbalimbali ya kijamii na pia walitumika katika kutoa mwongozo au ufumbuzi kwa jamii katika masuala muhimu katika nyanja za uchumi, siasa, utamaduni na hata imani.
Na kwamba zipo nchi ambazo wazee huheshimiwa sana kutokana na mchango wao katika jamii husika na hupatiwa mahitaji yote muhimu kama malazi, mavazi, chakula, uangalizi wa fya zao na ulinzi
Pensheni jamii huondoa udhalilishaji kwa wazee ambao wanaonekana kuwa omba omba, huongeza tija kwa wafanya kazi na kuwezesha mifumo mingine kufanya kazi za kuliongezea kipato taifa
Wazee wote nchini wale waliofanya kazi kwenye sekta rasmi na sekta zisizo rasmi wanatakiwa wapewe pensheni bila ubaguzi kwani jambo hilo litaongeza mshikamano na upendo katika jamii
Lakini pia itarahisisha Serikali kusimamia utoaji wa pensheni hiyo, ingawa pia itaondoa vitendo vya urasimu miongoni mwa watendaji wa Serikali ambao wamekuwa wakitoa huduma kwa njia ya rushwa
Kuondoa waongo kupewa haki na wakweli kukosa haki kwani watu watakuwa wanaelewa nani wanaostahili kunufaika bila mashaka kwani hapatatokea udanganyifu wa kiumri
Pia kutumia kigezo cha unafuu wa maisha(uwezo) wa wazee kupata pensheni kitaleta athari ya kimaadili,kiuchumi,kisiasa,kijamii na kiuendeshaji hivyo ni lazima wazee wote walitimiza miaka 60 na kuendelea wakapata pensheni kama sera na matamko mbalimbali nchini yanavyotamka
Matamko mbalimbali yamekuwa yakiendelea kutolewa kwa nia ya kuikumbusha serikali na jamii juu ya wajibu wao katika kuhakikisha kwamba wazee wanapata haki zao na kuitaka Serikali itimize wajibu wake muhimu wa kuwalinda na kuwathamini wazee nchini
Masuala mengi mazuri kuhusiana na wazee yamebaki kuwa midomoni mwa jamii au kwenye nyaraka mbalimbali za serikali na kwamba utekelezaji kuhusiana na namna ya kumaliza kero za wazee umeendelea kuwa wa chini sana na matokeo yake, wazee wetu wameendelea kukabiliwa na changamoto nyingi za kimaisha.
Sera ya Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2003 na Sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii ambapo sera ya Taifa ya afya ya mwaka 2007 iliyofanyiwa marekebisho inataja wazee kuwa ni kundi maalum litakalofaidika na huduma za afya bure.
Sera ya Taifa ya idadi ya watu na tamko lake elekezi linahimiza kuanzisha hifadhi za kijamii zinazoshughulikia matatizo ya wazee, kuhimiza sekta binafsi, asasi zisizokuwa za Serikali na mashiriki ya kidini kuwekeza katika utoaji wa huduma za kijamii, hususan huduma za afya kwa jamii lakini mpaka sasa utekelezaji wake ni hafifu
Zipo pia sera nyingine nyingi ikiwemo sera ya taifa ya maafa ya mwaka 2004, sera ya taifa ya ardhi, sera ya taifa ya hifadhi za jamii ya mwaka 2003, sera ya lishe na sera zingine zinatamka mahitaji ya wazee lakini utekelezaji wake umeshindwa kutekelezwa
Pamoja na wingi wa nyaraka zinazozungumzia wazee, viongozi mbalimbali pia wamekuwa hodari katika kuelezea umuhimu wa ustawi wa wazee kwa taifa lakini wameshindwa kutekeleza ahadi zao
Mwandishi mmoja anaitwa Vince Lombardi aliwahi kusema”kila mtu anapenda kufanikiwa ila niwachache wanapenda kujiandaa kufanikiwa” ni ukweli ulio wazi kuwa wengi wanatamani mafanikio ila hawajui na hawakubali masharti ya kufanikiwa
Hakuna anayepanga kushindwa ila wengi wanashindwa kupanga na ndio maana maandalizi ni kitu cha msingi kwa mafanikio ya kitu chochote hivyo kuwepo kwa utafiti niliousema hapo mwanzo,kuwepo kwa sera na matamko ni mwanzo mzuri wa kukamilisha adhima ya ustawi wa wazee nchini
Ndio maana nathubutu kusema kuwa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete imejenga misingi mizuri ya kuhakikisha wazee wanatambulika na wanathaminiwa katika kupata huduma muhimu za kimaisha, hivyo Serikali ya awamu ya sita inatakiwa itekeleze kikamilifu madai ya wazee nchini.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika