December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MISA Tanzania yakutana na Wabunge vinara, wajadili vifungu vya sheria za habari

Na Zena Mohamed, TimesMajira Online, Dodoma.

TAASISI ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA TANZANIA) imeendesha warsha kwa  wabunge vinara na marafiki wa vyombo vya habari Pamoja na asasi mbalimbali za kiraia kujadili baadhi ya vifungu vilivyop kwenye sheria za habari.

 Akifungua warsha hiyo ya kuwajengea uwezo makundi hayo iliyofanyika jijini Dodoma,  Mwenyekiti wa MISA TANZANIA Bi.Salome Kitomari amesema dhumuni kubwa la warsha hiyo ni kuwashirikisha wabunge na wadau wa Habari mambo mbalimbali ambayo yapo katika sheria za Habari na yanachangia kudidimiza uhuru wa kujieleza.

“Tumewaita baadhi ya Wabunge wetu vinara kuwashirikisha kile ambacho waandishi wamekuwa wanakilalamikia mara kwa mara hivyo panapotokea mapitio ya sheria wawe na uzoefu na waweze kuona madhara ya baadhi ya vifungu vya sheria katika tasnia ya Habari.” amesema Kitomari

Kwa upande wake Halima Mdee (Viti Maalum- CHADEMA) kuna baadhi ya sheria zinaminya uhuru wa vyombo vya Habari kutekeleza majukumu yao kwa kile kinachoitwa ‘maslahi ya umma’

Mdee amesema tafsiri ya maslahi ya umma katika mambo mbalimbali yanayotokea nchini haipo wazi kwani upande wa utawala unaweza ukawa na tafsiri tofauti na kile ambacho wananchi wanachokitarajia.

“Habari yenye maslahi na umma ni lazima iandikwe bila kuwekea vigezo vyovyote vile,jambo lenye maslahi ya umma lazima ujue jambo hilo sio kulificha ficha.” Amebainisha Mdee huku akiomba vyombo vya Habari vinavyotambulika kama vya umma kutoa taarifa kwa maslahi ya umma na sio kutoa muda mwingi kwa watawala tu.

Naye mbunge wa Momba(CCM),Condester Sichwale aliwataka waandishi wa Habari kuandika Habari kwa weledi ili kuaminika katika jamii,na pia ameshauri vyombo vya Habari kujikita katika kutafuta suluhisho kwa matatizo ya yanayokabili jamii.” ameeeleza Sichwale.

“Tunaomba mjitahidi kusimamia maadili na miongozo inayosimamia tasnia yenu,kuna baadhi ya mambo yanakuzwa na vyombo vya habari bila sababu ya msingi na wakati mwingine Habari hizo zinaenda kupotosha jamii” amesema Sichwale

Akizungumza kwa niaba ya wabunge hao, Mbunge wa Mlalo (CCM) Rashidi Shangazi amesema kuna umuhimu wa kuanzishwa baraza la walaji wa Habari ili wao kama watumiaji wa Habari wawe na jukwaa la kufikisha maoni yao kuhusu muenendo wa tasnia hiyo.

“Kama walaji wengine wana mabaraza yao na sisi walaji wa Habari ni bora tukafikiria kuanzisha jukwaa letu ili inapobidi tuwaambie kwamba mnachotulisha siyo tunachohitaji.”alisisitiza Shangazi.

Shangazi pia aliishukuru MISA TAN kwa kuwajengea uwezo kundi hilo la wabunge na kuwashauri kuendelea na semina hizo kwa kamati mbalimbali za bunge ili kuwaonesha namna baadhi ya vifungu vya sheria zinazopitishwa bungeni zinavyaathiri uhuru wa tasnia ya Habari nchini.

Semina hiyo iliongozwa na Wahariri Waandamizi Jesse Kwayu na Neville Meena ambao waliwapitisha washiriki katika vifungu mbalimbali vya sheria ikiwemo Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari, 2016.