Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Singida.
WAANDISHI wa Habari wametakiwa kutumia kalamu zao kuandika habari zenye kuinua Uhuru wa Kujieleza miongoni mwa wanajamii ili kupata majawabu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Hayo yamebainika katika mafunzo ya siku tatu (3) yaliyoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika,Tawi la Tanzania (MISA-TAN) kuwajengea uwezo wa kutafuta na kuchakata habari zitakazo chochea Uhuru wa kujieleza kwa Wanahabari zaidi ya 40 kutoka Mikoa ya Tabora, Dodoma, Shinyanga, Simiyu na wenyeji mkoa wa Singida.
Akizungumza na washiriki ,Mwezeshaji wa Mafunzo hayo mwandishi mkongwe Marko Gideon, amesema Wanahabari wanapaswa kutumia kalamu zao vyema kuandika habari za uhuru wa kujieleza katika Nyanja mbalimbali ili kupaza sauti za wananchi ambao kwa kiasi kikubwa wanategemea vyombo vya habari kufikisha vilio vyao.
“Uhuru wa Kujieleza ni moja ya nguzo katika kujenga msingi imara Utawala wa bora kwa vile wananchi wote watashiriki katika kutoa maoni kwa ujenzi wa mambo mbalimbali katika taifa,
“Nchi isiyo na Uhuru wa kujieleza hautakuwepo uwajibikaji kwa viongozi, hakutakuwa na usawa wa kisheria, hakuna uwazi, uchaguzi hauwezi kuwa huru na haki, wala kudhibiti matumizi mabaya madaraka kwa viongozi,”amesema.
Hata hivyo,washiriki wa mafunzo hayo wamesema kwamba sera za baadhi ya vyombo vya habari zimekuwa kikwazo kwa baadhi ya Waandishi kutojihusisha na uandishi wa habari za uchunguzi zitakazoweza kuibua mambo mbalimbali yanayoikabili jamii ikiwemo Uhuru wa kujieleza.
“Kuna baadhi ya vyombo vya habari vina mlengo ambao moja kwa moja lengo ni kuminya uhuru wa kujieleza,vyombo au wamiliki wake wameegamia upande ambao hautakiwi kuguswa kwa lolote” amesema Nicholous Machunda mwandishi na mshiriki kutoka mkoa wa Simiyu.
Pamoja na hilo,baadhi ya washiriki hao wamesema hofu ya usalama imekuwa kikwazo kikubwa kwa waandishi kutafuta na kuchakata habari za kiuchunguzi na zile zenye kuibua uhuru wa kujieleza.
“Waandishi wanakosa kujiamini,wanaishi kwa mashaka wakidhani kwamba wakiandika habari ya aina hii usalama wao utakuwa hatarini” amebainisha Jeniva John mshiriki kutoka mkoa wa Shinyanga.
Naye Andrew Marawiti kutoka Misa-Tan, amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kuzalisha maudhui yenye ubora yanayohusiana na Uhuru wa Kujieleza
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi