Na Jackline Martin, TimesMajira Online
SERIKALI kupitia Tume ya Umwagiliaji imetenga zaidi ya sh. Bilioni 374 kwa mwaka 2023 kwa ajili ya kujenga mabwawa, kuchimba visima na kuweka miradi ya umwagiliaji vizuri ili wakulima waweze kuzalisha mazao mwaka mzima badala ya kutegemea mvua.
Hayo yameyasema Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Mkutano Jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF) 2023 unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC) leo Jijini Dar es Salaam.
Msigwa amesema kulingana na takwimu, zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wanajihusisha na kilimo, hivyo kwa kutambua hilo Serikali imeamua kuchukua hatua madhubuti kuimarisha Sekta ya kilimo na kuongeza bajeti ya kilimo hadi zaidi ya sh. Bilioni 970.
“Fedha hizi zinapelekwa kwenye kilimo kwa sababu Serikali yetu imeanua kufanya mageuzi kwenye kilimo, tuondoke kwenye kilimo cha zamani, twende kwenye kilimo cha kisasa, tuondoke kwenye kilimo Cha kutegemea mvua, tulime kilimo cha umwagiliaji,” alisema.
Amesema lengo la Serikali ni kuongeza hifadhi ya chakula, kwani wamekuwa na hifadhi ya chakula tani 2000 ambapo kwa sasa wanakwenda kwenye hifadhi ya tani 500,000.
“Zipo programu nyingine nyingi ikiwemo utunzaji wa mazao yenyewe, programu kabambe katika Wizara ya Kilimo kupitia shirika la Hifadhi ya Chakula na Nafaka (NFRA).
Programu ya kujenga vihenge 56 lakini pia tumefanya uamuzi serikalini kwamba hata yale maghala ambayo yalikuwepo vijijini kwenye maeneo mbalimbali na yenyewe wayatumie kuhifadhi chakula cha Watanzania.”
Pia Msigwa amesema kwa maghala waliyoyajenga sasa hivi watakwenda kuhifadhi tani 510,000, lakini pia wanataka kupanua zaidi wajenge vihenge vingi ili wafikie tani laki saba na nusu ifikapo mwaka 2025.
“Huu ni mpango unaowezekana lengo tupunguze madhara ya kuharibika kwa mazao baada ya mavuno, tupate mavuno na yote tuyapeleke sokoni tuyauze yasiharibike yakiwa mikononi mwa wakulima,”amesema.
Kadhalika Msigwa amesema wana programu ya kutoa ruzuku ya pembejeo, mbolea, dawa za kilimo, vitendea kazi vya wakulima, kujenga miundombinu kupitia TARURA, na kujenga barabara nyingi kuelekea vijijini
” kilimo hadi kifanyike vizuri kinahitaji mitaji, miundombinu, teknolojia ambayo tunaendelea kuifanya,” amesema.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi