Na Teresia Mhagama,TimesMajira online,Dodoma
WAZIRI wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani amesema kuwa, takriban miradi minne ya umeme inatekelezwa katika Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuhakikisha kuwa maeneo yote ya Mkoa yanapata nishati ya umeme itakayowasaidia wananchi katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Waziri wa Nishati amesema hayo wakati alipofika katika Kijiji cha Makutupa wilayani Kongwa,mkoani Dodoma ili kuwasha umeme kwenye Kijiji hicho ambapo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Suleiman Serera, Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga na watendaji mbalimbali wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Ametaja miradi hiyo kuwa ni, mradi wa kusambaza umeme vijijini unaoendelea sasa wa Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu ijayo, mradi wa kupeleka umeme vitongojini, mradi wa kupeleka umeme kwenye maeneo yaliyo karibu na mitaa mijini (Peri-urban) na miradi inayotekelezwa na TANESCO.
“Kwa Mradi wa kusambaza umeme vijijini Dodoma, Serikali imetoa takriban shilingi bilioni 60, mradi wa kupeleka umeme vitongojini Serikali imetoa shilingi bilioni 48.3, kwa mradi wa Peri-Urban Serikali imetoa shilingi bilioni 23 na mradi mwingine unatekelezwa na fedha kutoka TANESCO kama ilivyo hapa Makutupa,” amesema Dkt.Kalemani
Kuhusu kazi ya usambazaji umeme vijijini mkoani Dodoma, Dkt.Kalemani amesema kuwa, vijiji 467 vimeshasambaziwa umeme, kati ya vijiji 581 ambayo ni zaidi ya asilimia 81.
Vilevile, kwa Vijiji 114 ambavyo bado havijasambaziwa umeme mkoani Dodoma, alieleza kuwa wakandarasi pamoja na fedha za kusambaza umeme zimepatikana hivyo vijiji husika vitapata umeme ndani ya miezi 18.
Aidha, katika Wilaya Kongwa,amesema kuwa, kuna vijiji 87 na Vijiji ambavyo havina umeme ni vinne tu ambavyo vitasambaziwa umeme ndani ya miezi mitatu ijayo.
Dkt.Kalemani ameongeza kuwa, kwa vijiji 1974 ambavyo bado havijasambaziwa umeme nchi nzima kati ya vijiji 12,268, wakandarasi wa kusambaza umeme kwenye vijiji hivyo wameshapatikana na wataingia katika maeneo ya kazi wiki ijayo.
Akiwa wilayani Kongwa,Waziri wa Nishati pia ametembelea eneo la Mbande ambalo wananchi wake wamekuwa wakilalamika kuwa kuna nguzo za umeme zilizosimikwa muda mrefu bila wananchi hao kuunganishiwa umeme.
Akiwa katika eneo hilo, Dkt.Kalemani ameahidi kuwa, Mkandarasi, kampuni ya Derm Electric ataanza kuwaunganishia umeme wananchi kuanzia Ijumaa ya Mei 7,mwaka huu.
Akizungumza na wananchi wa Makutupa na Mbande, Dkt.Kalemani amewasisitiza kutumia umeme kwa matumizi mbalimbali kwani Serikali inatumia fedha nyingi kufikisha umeme katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na kupunguza gharama za uunganishaji ili kila mtanzania atumie nishati hiyo muhimu.
More Stories
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi
SACP Katabazi: Elimu ya usafirishaji wa kemikali bado ni muhimu kwa watanzania
REA yajitosa kwenye nishati safi ya kupikia