December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miradi 67 Tanga kufikiwa na Mwenge wa Uhuru

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Tanga

IMEELEZWA kuwa, miradi 67 yenye thamani ya shilingi bilioni 14.3 inatarajiwa kukaguliwa na mingine kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru 2021 katika Wilaya nane za Mkoa wa Tanga zenye jumla ya kilomita 1187 ambao ni mkoa wa kwanza kati ya mikoa 26 ya upande wa Tanzania Bara.

Awali akizungumza baada ya kupokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib, RC Malima amesema Mwenge wa Uhuru utakagua miradi hiyo ambayo fedha zake zimetokana na nguvu kazi za wananchi.

Malima amesema, Mkoa wa Tanga umekuwa wa kwanza kukimbiza Mwenge wa Uhuru ambapo unatarajiwa kuzindua, na kukagua Miradi mbalimbali yenye thamani ya zaidi sh.bilioni 14.

Aidha, RC Malima amesema kuwa mwenge utakimbizwa kwa siku nane ukianzia katika wilaya ya Tanga mjini kisha,Pangani,Muheza,Mkinga,Lushoto,Handeni,Kilindi,na kumalizikia Korogwe ambapo utakabidhiwa kwa Mkoa wa Kilimanjaro.

RC Malima ametoa wito kwa wakazi wa jiji la Tanga kujitokeza kwa wingi katika shamrashamra za kukimbiza mwenge huo na katika mkesha, mwenge ambao umewasili Mkoani Tanga Lengo kuu likiwa ni kukuza miradi kwa maslahi ya watanzania wote

Akizungumza wakati akikabidhi Mwenge wa Uhuru, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk amesema mwenge wa uhuru ukiwa mkoani hapo ulikagua na kuzindua miradi mbalimbali katika Wilaya za Wete na Micheweni katika majimbo 9.

Mkuu huyo wa Mkoa Kaskazini Pemba amesema kuwa, ameukabidhi Mwenge wa uhuru mkoani Tanga ukiwa kwenye usalama wa hali ya juu pamoja na jumla ya wakimbiza mwenge kitaifa 5.

Katika makabidhiano hayo kiongozi Luteni Josephine Mwambashi amewataka wakuu wa Mkoa na Wilaya zinazotarajia kupokea Mwenge kuhakikisha wanakabidhiwa nyaraka za miradi wanayokwenda kukagua mapema kabla hawajafika kwenye miradi husika huku akisema hawatakuwa na huruma kwenye miradi ya itakayodhaniwa kuwa na kasoro.

“Niwasisitize tu kwamba kwenye miradi hasa inayohusu miundombinu na maeneo mengine kutuwahishia mapema nyaraka husika na sio kusubiri mpaka tufike kwenye miradi ndio mtukabidhi, “alisistiza Mwambashi.