January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Milioni 850, zimetolewa kulipa fidia wananchi Ileje

Na Moses Ngw’at, Timesmajira Online,ILEJE

SERIKALI imetoa kiasi cha milioni 850 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha ujenzi wa barabara ya Isongole wilayani Ileje hadi Kasumuku wilayani Kyela mkoani Mbeya yenye urefu wa kilometa 124 itakayojengwa kwa kiwango cha lami ambayo kwa sehemu kubwa inatenganisha mpaka wa Tanzania na Malawi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bupigu,baada ya kufanya ukaguzi wa barabara hiyo , akiwa anahitimisha ziara yake ya kikazi ya siku nne kwa kutembelea miradi ya barabara inayotekelezwa na serikali katika Mkoa wa Songwe.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo unatarajia kuanza hivi karibuni baada ya kupatikana kwa mkandarasi, ambapo ujenzi utaanza kwa kujenga kilometa 52 kutoka Isongole hadi Ndembo – Isoka wilayani Ileje na kwamba tayari wananchi wote wamelipwa fidia kiasi hicho cha milioni 850.

Amebainisha kuwa lengo la serikali ni kuboresha miundombinu ya mawasiliano ya barabara katika kuhakikisha inakuza uchumi wa nchi na kwa watanzania kwa ujumla ambapo ujenzi wa barabara ni muhimu kwa nchini kwa kuunganisha na nchi za Sadac kwa kusafirisha mizigo kupitia barabara hiyo.

Naibu Waziri huyo wa Ujenzi ameelezea umuhimu mwingine wa barabara hiyo kuwa ni barabara ya ulinzi kwa kuwa sehemu kubwa imepita nchini hapa na nchi ya Malawi.

“Barabara hii mbali na umuhimu wake katika ulinzi wa mpaka lakini ni barabara ya kimkakati kwani itasaidia kusafirisha shehena ya makaa ya mawe kutoka katika mgodi wetu wa Kiwira,kipande hiki cha barabara kikikamilika kitasadia kuifungua nchi kutoka mikoa ya Kusini hadi Magharibi kisha kwenda nchi za Burundi na Kongo,”amesema Kasekenya.

Sanjari na hayo amewataka wananchi wanaotakiwa kupisha ujenzi wa kipande cha pili cha barabara hiyo kuanzia Ndembo wilayani Ileje hadi Ngana kwenda Kasumulu wilayani Kyela kutoa ushirikiano kwa wataalam wataofika katika maeneo yao kwa ajili ya kufanya uthamini.

Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga, ameeleza kuwa taratibu za kupata mkandarasi atakaeanza ujenzi wa barabara hiyo kutoka Isongole hadi Ndembo kwenda Isoko tayari mchakato umeanza.