November 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Milioni 500 zatumika kuboresha elimu Kwimba

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Kwimba

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA),imetumia .kiasi cha milioni 501 kukamilisha bweni la wasichana, maabara na vyumba vya madarasa ya shule ya sekondari Nyamilama wilayani Kwimba.

Ofisa Elimu Wilaya Kwimba,Emmanuel Katemi, amesema wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mwanza, leo.

Amesema serikali imejenga na kukamilisha bweni la wasichana 180 wa shule ya sekondari Nyamilama ili kuwaepusha na mimba za utotoni kwa sh. milioni 140, maabara mbili za Kemia na Baiolojia kwa sh.milioni 118.

Katunzi amesema katika kuchochea wanafunzi kujifunza imekamilisha miundombinu ya vyumba 112 vya madarasa kwa sh.milioni 240 zilizotolewa na serikali kupitia Mradi wa TEA.

“Kujengwa kwa miundombinu hii kumeleta manufaa kwa shule, mazingira yameboreka,ufaulu umeongezeka,mimba za utotoni zimepungua ari ya watoto wa kike kupenda masomo ya Sayansi imeongezeka,” amesema Katunzi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja ‘Smart’ amesema Kamati ya Siasa imefarijika kwa utekelezaji bora wa Ilani ya Uchaguzi Nyamilama sekondari.”Kamati imekuja kuagalia kilichofanyika kwa fedha alizoleta Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, tullichokiona kinalingana na thamani ya fedha, shule hii ni nzuri kwa mazingira ya kujifunzia na kufundishia ni shule bora kuliko za binafsi,”amesema.

Smart amesema penye ushirikiano mambo yana kwenda vizuri na mafanikio yanaonekana , hivyo kamati imeridhika kwa kazi zilizofanyika Kwimba na kuwahimiza kuendelea kuchapa kazi ili kuleta matokeo chanya katika kuleta maendeleo ya jamii.