January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Milioni 379.5 kujenga madarasa ya awali kwa shule tano za msingi

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online Tanga

Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 379.5 kwa ajili ujenzi wa vyumba vya madarasa ya awali kwenye shule za msingi tano jijini Tanga kupitia mradi wa BOOST.

Ofisa Elimu Msingi Shomari Bane na timu yake ya utekelezaji wa mradi huo amefanya mkutano kwenye shule ya msingi Mwakidila vinapojengwa vyumba viwili na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo.

Bane amesema ujenzi wa vyumba hivyo utaenda sambamba na matundu sita ya vyoo kati ya matundu hayo matatu kwa ajili ya wavulana na matatu ya wasichana, uzio,uwanja wa michezo ya watoto na samani, vyote vikiwa na gharama ya milioni 69.1.

Shule nyingine zitakazonufaika na mpango huo ni Kasera pamoja na shule shikizi ambayo imepata kiasi cha milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili na milioni 12.6 kwa ajili ya kujenga matundu sita ya vyoo,

“Nimewaomba wananchi kutumia nguvu zao kujitolea na michango yao kwa ajili ya kujenga ofisi ya walimu kwa sababu kuna watoto hawa wadogo wa elimu ya awali, hivyo wanapokuwa na ofisi jirani na walimu wao itapendeza zaidi kiusalama,” amesema.

Amefafanua kwamba shule za msingi Majengo na Shaban Robbert kila moja ilipatiwa milioni 75 kwa ujenzi wa madarasa matatu pamoja na milion 12.6 kwa ajili ya matundu 6 ya vyoo.

Hata hivyo mpango wa kujenga madarasa kwenye shule hizo, ulibadilishwa na fedha zimepelekwa kwenye shule zingine za msingi Ziwani na Kange, kwa kuwa, Shaban Robart na Majengo upo mpango wa kujengwa gorofa.

“Mradi huu unatekelezwa ndani ya miaka sita, kuanzia mwaka 2021 hadi 2027 tunaukabidhi kwa uongozi wa kata katika shule husika kwa kuwa wao ndiyo watakaosimamia mradi huu” amefafanua Bane.

Baadhi ya wananchi wameelezea furaha yao kufuatia mradi huo na kusema itawasaidia wanafunzi kukaa darasani kwa nafasi kwani vyumba vya madarasa vilivyopo sasa ni vichache ikilinganishwa na wanafunzi waliopo.

Mwenyrkiti wa mtaa wa Mwakidila B, Athumaji Mbulinyingi amesema kilio chao na kero yao ni msongamano wa watoto darasani.

“Tuna imani na mradi huu na mimi kama Mwenyekiti wa Mtaa nitausimamia nikishirikiana na wananchi wangu,utafanyika na hakutakuwa na dosari yoyote, malumbano wala mgogoro wa aina yoyote,” amesema.