November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti,

Milioni 307/- zawatokea puani watumishi Kagera

Polisi, TAKUKURU waelekezwa kuwatia mbaroni baada ya kushindwa kuzirejesha kwa muda waliopewa, wengine wasimamishwa kazi, kuhojiwa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Biharamulo

MKUU wa Mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti, amewaagiza  Kamanda wa Polisi mkoani Kagera na Kamanda wa TAKUKURU kuwakamata watumishi 34 wa Halmashauri ya Wilaya Biharamulo wakiwemo watendaji wa vijiji, Kata kwa kushindwa kurejesha fedha sh. milioni 307 zilizokusanywa kutoka vyanzo vya mapato vya ndani bila kupelekwa Benki.

Pia ameagiza kusimamishwa kazi Kaimu Mweka Hazina, Sospiter Makene na mwenzake, Jastine Banula pamoja na maofisa tehama wawili, Rogers Semukoko na Beatrice Gurusya.

Agizo hilo lilitolewa jana na RC Gaguti alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo iliyolenga kutoa maelekezo ya kiutendeji kutokana na halmashauri hiyo kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato na kuoneka kuna ubadhirifu wa fedha za Serikali.

Gaguti amechukua uamuzi huo baada ya kutoa siku saba kwa watumishi hao kurejesha fedha hizo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichofanyika Juni 5, mwaka huu.

Kikao hicho kilikuwa cha kujibu hoja zilizoibuliwa kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Nilikuja hapa nikatoa maelekezo kwa wale wote waliokuwa wanakusanya fedha kwa kutumia mashine za Poss bila kuzipeleka benki warejeshe ndani ya siku 7, lakini fedha iliyorejeshwa ni asilimia 2.

Kwa mwendo huu hatuwezi kwenda lazima tuweke misingi imara ya kuboresha utumishi na uadilifu, hapa nina orodha ya watendaji 30, ambayo nampatia Kamanda wa Polisi ili wakamatwe  popote walipo na wengine wanne hawa naagiza wasimamishwe kazi, lakini wawe chini ya uangalizi wa Kamati ya Ulizi na Usalama ili kutoa ushirikiano,” amefafanie Mkuu wa Mkoa Gaguti.

Ameongeza kuwa watumishi wa umma wanatakiwa kuwa waadilifu na kuiogopa fedha ya Serikali na kuahidi kuwachukulia hatua wote watakaobainika kufanya vitendo vya ubadhirifu.

Ametoa onyo kali kwa watendaji wa vijiji na kata mkoani humo, akitaka wahakikishe wanasimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali bila kuleta ujanjau janja.

“Fedha ya Serikali ni ya moto hivyo haipaswi kulala, niwasihi tu ndugu zangu tusijaribiane, hatutasita kumchukulia hatua yeyote atakayehusika na upotevu wa pesa.

Tambueni watendaji ndiyo mna dhamana ya kukusanya mapato ya ndani kutoka katika vyanzo vya mapato katika maeneo yenu,” amesema Gaguti.

Aidha Gaguti amesema baadhi ya watumishi walikataa kusajili vyanzo vya mapato kwa makusudi na baadaye kuwarudia wafanyabiashara na kuchukua fedha kinyemela na kusababisha serikali kukosa mapato yake.