Na Joyce Kasiki,timesmajira onlone,Dodoma
MKURUGENZI Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Watoto Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto Sebastian Kitiku amesema,miongoni mwa changamoto zinazoikabili idara hiyo katika kupambana na ukatili wa kijinsia ukiwemo ukeketaji ni namna ya kubadilisha fikra za wananchi katika kile wanachokiamini kuhusiana na mila desturi.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt.John Jingu kuhusiana na maadhimisho ya Kitaifa ya kupinga ukeketaji dhidi ya mwanamke na mtoto wa kike ambayo huadhimishwa Februari 6 ya kila mwaka.
Amesema,licha ya elimu mbalimbali kutolewa kuhusiana na kupinga ukatili huo lakini bado jamii imekuwa ikiamini mila na desturi ambazo zipo tangu enzi ambazo nyingi husababisha ukatili kwa wanawake na watoto wa kike .
“Adhabu zipo nyingi na ni adhabu kali,lakini utaona licha ya kuwepo kwa adhabu hizo lakini matukio ya ukatili kwa wanawake na watoto wa kike hasa katika ukeketaji,kwa hiyo hapa changamoto kubwa namna ya kushughulikia mila na desturi ambazo zipo tangu enzi.”amesema Kitiku
Kitiku ameitaja mikoa inayoongoza kwa ukeketaji kuwa ni pamoja na Manyara asilimia 58,Dodoma asilimia 47,Arusha asilimia 41,Mara asilimia 32 na Singida asilimia 31 huku kwa upande wa kitaifa ukeketaji umefikia asilimia 10.
Amesema changamoto nyingine ni ya ukeketaji wa kuvuka mipaka kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na pembeni ya Afrika ambapo jamii ya nchi moja huvuka mipaka kwa ajili ya ukeketaji katika nchi nyingine na kurudi nchini kwake ili kukwepa mkono wa sheria.
Kitiku amesema kwa kutambua hilo Serikali za nchi hizo ikiwemo Uganda,Kenya ,Somalia na Ethiopia ziliingia makubaliano ya kukabiliana na ukeketaji wa kuvuka mipaka kwa kutekeleza mpango kazi wa pamoja .
Aidha amezungumzia madhara ya ukeketaji kwa makundi hayo huku akisema athari hizo zipo kiafya na kijamii ambapo kijamii athari inahusisha kuendeleza ukatili kwa watoto kwa kuchochea ndoa za utotoni na kutengwa kwa wanawake ambao hawajakeketwa na hivyo kuwasababisha unyanyapaa na kuongezeka kwa idadi ya wanawake na watoto wenye msongo wa mawazo.
Hata hivyo amesema,katika kushughulikia tatizo la ukeketaji nchini Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa kutokomeza Ukeketaji wa mwaka 2019-2022 ambapo kupitia mpango huo Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutoa elimu kuhusu athari za ukeketaji na kuimarisha mifumo ya kushughulikia vitendo vya ukeketaji.
Pia amesema kwamba 2017 Serikali kwa kushirikiana na wadau iliandaa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018-2021/2022 ambao umelenga kupunguza vitendo vya ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam