Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, TABORA
HALMASHAURI ya Manispaa Tabora imekipongeza kikundi cha Vijana Waendesha Bodaboda cha KAZI IENDELEE kwa kupata mafanikio makubwa kupitia mkopo waliowezeshwa na halmashauri hiyo katika mwaka wa fedha 2022/23.
Pongezi hizo zimetolewa juzi na madiwani wa manispaa hiyo baada ya kuridhishwa na matumizi mazuri ya mkopo waliopewa ambao umekuwa kichocheo kikubwa cha mafanikio yao.
Diwani wa Kata ya Itonjanda Alfonsi Shushi ameeleza kuwa mkopo waliopewa umewainua kimaisha na kila mmoja ameweza kumaliza marejesho yake ndani ya mwaka mmoja na kumiliki pikipiki yake, sasa Kazi Inaendelea.
Amebainisha kuwa kikundi hicho kilichopo katika Kijiji cha Itonjanda, kata ya Itonjanda katika halmashauri hiyo, chenye jumla ya vijana 10 kilipewa mkopo wa sh mil 25 Oktoba 6, 2022 ili kuwarahisishia shughuli yao za usafirishaji abiria.
‘Hii mikopo ni mkombozi kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, nawapongeza sana vijana wetu kwa kutumia vizuri mkopo huo na kuurejesha kwa wakati ili na wenzao wapate, sasa wameinuka kimaisha’, amesema.
Akikabidhi kadi halisi za umiliki wa vyombo hivyo Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ramadhan Kapela amesema kuwa dhamira ya serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hasan ni kuona mikopo hiyo inaleta tija.
Amesisitiza kuwa ikitumiwa vizuri maisha ya wananchi walio wengi yatabadilika, kwani vikundi vingi vimeshapewa fedha hizo na kuzirejesha kwa wakati ila baadhi yao bado wanasuasua kwenye marejesho.
Ameaagiza Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo kuendelea kufuatilia maendeleo ya vikundi vyote vilivyokwisha kukopeshwa ili kujionea mafanikio waliyopata na kuwahamasisha kurejesha kwa wakati.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa hiyo Tumaini Mgaya ameeleza kuwa kikundi hicho kilipewa mkopo wa mwaka mmoja kuanzia Novemba 8, 2022 na walitakiwa kurejesha sh 447,000 kila wiki kwa wiki 56 ili ifikapo Nov. 7, 2023 wawe wamemaliza.
‘Hawa vijana ni mfano wa kuigwa, tumewapa mkopo na wamemaliza marejesho kwa wakati, leo hii tunawakabidhi kadi zao halisi za umiliki wa vyombo hivi, na wakati mwingine wakiomba tena tutawapa’, amesema.
Amebainisha kuwa vikundi vingi vilivyowezeshwa mikopo hiyo vimepata mafanikio makubwa na kurejesha kwa wakati, ila ni vikundi vichache tu vinavyosua sua na kushindwa kurejesha kwa wakati.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapatoÂ