January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mikopo ya ZEEA yaanza kutolewa kidijitali, maofisa washauriwa kuwa makini

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

MIKOPO kwa njia ya kidijitali inayoanza kutolewa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) imeelezwa kuwa itawasaidia wananchi kupata fedha kwa wakati na kuendeleza biashara zao ili kujikwamua Kiuchumi.

Wakati hatua hiyo ikianza maafisa wanaohusika na maombi ya mikopo hiyo kupitia mfuko wa makundi maalumu (4-4-2) Kisiwani Pemba, wametakiwa kuwa makini wakati wa uwasilishaji wa mfumo wa maombi ya mkopo huo kwa njia ya mtandao.

Hayo yameelezwa na Afisa Mikopo kutoka ZEEA Suleiman Ali Hamad wakati wa ufunguzi wa mafunzo, kwa maafisa kutoka mabaraza ya miji, halmashauri, viongozi wa vikundi, maafisa vijana, watu wenye ulemavu, maafisa kutoka wanawake na watoto yaliyofanyika Gombani Pemba.

Hamad amesema kwa sasa mfumo mzima wa maombi ya mikopo yataombwa kupitia mtandaoni na sio kwa kutumia makaratasi kama zamani na hivyo itarahisha wananchi kupata fedha kwa wakati.

“Mikopo tayari itaanza kutolewa kidijitali, leo hapa watu wanaendelea kupatiwa mafunzo ambayo ni muhimu katika kuhakikisha wanafanikiwa kuomba mikopo hii kwa njia ya mtandao, tunaamini hawa wanaopata mafunzo watakwenda kuwafundisha na wengine,” amesema

Mratibu wa ZEEA Ofisi ya Pemba, Haji Mohamed Haji amesema moja ya masharti katika uombaji wa mikopo hiyo kwa njia ya mtandao ni lazima kikundi kiwe kimesajiliwa, waombaji wawe na kitambulisho cha mzanzibari.

Naye Afisa Akiba na Mikopo kutoka Idara ya Maendeleo ya Ushirika Pemba, Zuwena Abdalla Suleiman, amesema wanaposajili ushirika viongozi wanapaswa kuwa na sifa

“Ikitokea mmoja wa kiongozi amekosa sifa kikundi kinatakiwa kubadilisha Katiba kwa kumbadilisha kiongozi huyo aliyekosa sifa, na ndio maana tumekuwa tukitoa elimu ya kuhakikisha kila mtu anakuwa na vingezo vyote ikiwemo kitambulisho cha mzanzibari mkaazi,” amesema

Kwa upande wake Ofisa Kitengo cha Fedha Jumuishi kutoka Kampuni ya Airpay Tanzania, Majid Makilla amesema kutokana na mfumo ambao wamewatengenezea ZEEA wa kutoa mikopo kwa wazanzibari, wamejipanga kuhakikisha mfumo upo sawa muda wote ili kuruhusu wale wote wanaoomba na kutuma maombi wanaweze kufanikisha hayo kwa wakati.

Amesema wamejidhatiti kwa kuhakikisha wanajitoa kadiri wawezavyo ili kuwafundisha wazanzibari namna ya kuomba hiyo mikopo kwa kutumia mfumo huo mpya wa kidijitali.

“Tutatengeneza video ambayo itakuwa inaonesha kuanzia hatua ya kwanza hadi mwisho ya mtu anavyoweza kuomba mkopo kwa kupitia mfumo huu ambao tumeutengeneza.” amesema