November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mikoa 7 kunufaika na programu ya kuwezesha mnyororo wa thamani wa ufugaji nyuki nchini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

SERIKALI imezindua Programu ya kuwezesha mnyororo wa thamani wa ufugaji nyuki ambayo itawanufaisha wananchi wa mikoa 7 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Programu hiyo ambayo inafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kwa gharama ya Shilingi bilioni 27 itatekelezwa katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Katavi, Singida, Shinyanga, Mkoa wa Kusini Pemba na Kaskazini Pemba.

Akizindua Programu hiyo leo jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema Serikali inafanya uchambuzi wa kitaalamu kubaini wilaya na vijiji vilivyomo ndani ya mikoa hiyo ambapo mradi huu utatekelezwa.

Amesema programu hiyo inakwenda kuimarisha mifumo ya uzalishaji wa mazao ya nyuki, kuwezesha maeneo ya uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya nyuki, kujenga uwezo wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya ufugaji nyuki pamoja na taasisi zinazosimamia sekta hiyo.

Ameongeza kuwa programu hiyo itaiwezesha taasisi ya utafiti wa nyuki ipate vitendea kazi katika maabara ya utafiti iliyopo Njiro mkoani Arusha na kuweka mfumo thabiti utakaowezesha ufanyaji wa biashara ya mazao ya nyuki.

Masanja ametumia fursa hiyo kuwasihi Wakuu wa Mikoa ambayo programu hiyo inatekelezwa kutoa ushirikiano unaostahili na kusaidia kufafanua jambo hilo kwa wananchi.

” Nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi wote walio katika mikoa husika kushiriki katika kutekeleza programu hii ili iweze kuleta matokeo chanya yanayotarajia.

Nitoe maelekezo kwa watendaji watakaoshiriki katika kutekeleza programu hii kuzingatia uadilifu na weledi wakati wote wa utekelezaji wa programu hii.”

“Kwa wasimamizi wa programu niwaelekeze kusimamia programu hii kwa karibu ili kuhakikisha yale yote ambayo Serikali imekubaliana na Umoja wa Ulaya yanatekelezwa na si vinginevyo.” Amesisitiza.

Pia Mary Masanja amewataka viongozi wa Wizara washirikiane na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kutenga maeneo yatakayotangazwa kuwa hifadhi za nyuki ili wananchi na wawekezaji waweze kuyatumia kufuga nyuki kibishara.

Pia ameiomba Ofisi ya Rais-TAMISEMI iwaelekeze wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya hususani kwenye mikoa yenye fursa kubwa ya ufugaji nyuki kuajiri maafisa ufugaji nyuki watakaotumika kutoa huduma kwa wananchi.

Pia ameelekeza maafisa wa nyuki wote wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) watoe mafunzo na huduma za ugani kwa wafugaji nyuki walio katika maeneo mbalimbali hapa nchini pamoja na Wizara kuweka mazingira ya kukusanya takwimu za sekta ya ufugaji nyuki.

Aidha, amewataka wataalam wa Wizara waandae andiko lingine la mradi ili kuwezesha uendelezaji wa ufugaji nyuki katika maeneo mengine ya nchi ambayo yana fursa kubwa ya ufugaji nyuki.

Kwa upande wa Balozi wa Ubeliji nchini Tanzania, Peter Van ACKER amesema Umoja wa Ulaya umetoa ufadhili huo ili kuisaidia Tanzania kutumia fursa ya soko la asali lililoko katika nchi za Umoja huo.

” Nchi za Ulaya zinazalisha asilia inayotosheleza kwa asilimia 60 ya mahitaji, hivyo ni fursa kwa Tanzania kuchangamkia soko la Ulaya kwenye soko la asilimia 40 hasa ikizingatia Tanzania inashika nafasi ya pili Afrika katika uzalishaji mazao ya nyuki nyuma ya Ethiopia.”

Naye Balozi wa Umoja wa Ulaya Tanzania, Manfredo FANTI amesema Tanzania ina fursa ya kutumia soko la Ulaya kufanya biashara kwenye mazao ya kilimo na mifugo ikiwamo mazao ya nyuki bila ushuru au tozo kutokana na mikataba ambayo Tanzania imeingia na Umoja huo.

Awali Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma Mkomi amewahakikishia wananchi ambao watanufaika na miradi hiyo na Umoja wa Ulaya kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii iko tayari kuratibu usimamizi na utekelezaji wa programu zote zilizopangwa kwa maslahi mapaka ya Taifa.

Amesema programu hiyo inayotekelezwa kwa miezi 72 inatarajiwa kuwezesha kufanya mapitio ya Sera, Sheria na kuimarisha mfumo wa udhibiti ubora wa mazao ya nyuki, kuimarisha kiwango cha uzalishaji wa mazao ya nyuki yenye ubora na kuboresha mifumo ya biashara.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo- Zanzibar, Mhe. Lela Mohamed Mussa amesema ili kupata mafanikio yaliyokusudiwa upo umuhimu wa ushirikiano katika ngazi zote zinazotekeleza programu hiyo.