September 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mikataba ya lishe inavyoenda kuboresha afya kwa watoto wadogo

Joyce Kasiki

“Tunajua lishe ina madhara makubwa sana isiposimamiwa vizuri kwa makuzi ya watoto wenyewe ,uelewa wao kiakili darasani,lakini pia kama lishe haikuwa  vizuri tunakuwa na watoto ambao hawana uelewa mzuri katika masomo na mambo mengine.”

Ni maneno ya Naibu Waziri,Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (TAMISEMI) Dkt.Festo Dugange wakati akizungumza na mwandishi wa makala hii.

Kufuatia hali hiyo ,Naibu Waziri huyo anasema Serikali imeamua kuwekeza kwenye lishe ya watoto ili waweze kukua vyema .

Serikali imewekeza sana katika eneo la lishe 2016 ambapo tangu akiwa Makamu wa Rais ,Rais Dkt.Samia  Suluhu Hassan amekuwa kinara namba moja wa kusimamia suala la lishe na akasaini mikataba na wakuu wa mikoa yote 26 Tanzania Bara na tukaanda afua mahsusi.

“Kwa hiyo kwa ujumla afya ya mtoto ni muhimu kwa kwa sababu mtoto ndiyo Taifa la kesho maana mtoto mwenye afya njema ,afya bora anakuwa na uwezo mzuri darasani ,atakuwa na uwezo mzuri wa kujenga maisha yake,jamii yake na maendeleo ya nchi kwa ujumla,

“hivyo ,tunaamini uwekezaji kwenye afya ya mtoto ni msingi wa maendeleo ya Taifa na ndiyo maana baada ya uwekezaji kwenye eneo hilo ,tumeona ‘score card’(maendeleo) yetu inaenda vizuri ,maana yake tunakwenda na kijani yaan ‘trend’ ya lishe inaenda vizuri.”anasema Dkt.Dugange

Aidha anatumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi,wazazi na walezi ,waendelee kuwasikiliza wataalam, watumie huduma za afya zinazotolewa katika maeneo yao,wajifunze kuhakikisha kwamba kile ambacho kinaelekezwa kwa manufaa ya watoto  kinazingatiwa ili kuwe na Taifa lenye watu bora.

Anasema uwekezaji katika eneo la lishe unazingatiwa katika afua tano mahsusi ambazo ni pamoja na kutenga shilingi 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano kwa kila halmashauri ambapo utengaji  wa fedha hizo umeongezeka.

“Wakati tunaanza tulikuwa na asilimia 65,tukaenda silimia 70 na sasa tupo zaidi ya asilimia 99 halmashauri zote zinatenga shilingi 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano aliyepo ndani halmashauri husika.”

Anasema jambo la pili ni matumizi ya fedha hizo ambapo anasema sasa zaidi ya asilimia 95 ya fedha ambazo zinatengwa kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe zinatekeleza afua hizo.

“Na hii imekuwa ni mafanikio makubwa ,lakini alipoingia kuwa Rais alianzisha utaratibu huo tena wa kusaini mikataba mingine tena ambayo  ilienda kwa wakuu wa mikoa,wakuu wa wilaya,wakurugenzi,watendaji wa kata na viongozi wengine,

“Na tumeendelea kuona maendeleo makubwa ya utekelezaji wa afua za lishe ,udumavu umeendelea kupungua ambapo 2005 kurudi nyuma kasi ya udumavu nchini ilikuwa zaidi ya asilimia 48 ,kwa hiyo ‘almost’ asilimia 50 ya watoto walikuwa na udumavu,2015 tukashuka kutoka asilimia 48 mpaka asilimia 34 na mwaka huu sasa tupo asilimia 30,” anasisitiza Dkt.Dugange

Hata hivyo anasema dhamira ya serikali ni kuendelea kushusha kasi ya udumavu kutoka hiyo asilimia 30 hadi chini zaidi mpaka utakapomalizika huku akisema malengo yaliyowekwa ni kupunguza angalau siyo chini ya asilimia 5  kila baada ya miaka mitano .

Kwa mujibu wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto 9PJT-MMMAM) ,takribani robo tatu sawa na asilimia 66 ya watoto wote wenye umri  chini ya miaka mitano walio kusini mwa jangwa la Sahara wapo kwenye hatari ya kutokufikia hatua timilifu za ukuaji kutokana
na kukosa malezi bora, umasikini, utapiamlo pamoja na matatizo mengine ya kijamii na kiuchumi,

Aidha ,kwa mujibu wa Takwimu za Taifa za Idadi ya Watu za mwaka 2022 Tanzania ina takribani watoto 16,694,763 (wavulana 8,329,725 na wasichana 8,365,038) wenye umri wa miaka 0 – 8 (sawa na 27.0% ya watu wote) ambalo ni kundi kubwa linalohitaji kufikia ukuaji timilifu.

Anasema kwa kasi hiyo ,Serikali inatarajia  utekelezaji wa afua za lishe utaendelea kupunguza  udumavu kwa lengo kubwa la kuendelea kuboresha afya za watoto pamoja na kuboresha makuzi yao.

Anasema kila  mwaka Serikali inafanya mkutano mkuu wa lishe ambapo huwakutanisha Mawaziri wa Afya,Mawaziri wa TAMISEMI na wataalam wa wizara zote mwaganga wakuu wa mikoa ,Makatibu Tawala wa Mikoa,,Makatibu Tawala wa Wilaya , Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi wa Halmashauri na maafisa lishe wote nchi nzima wa halmashauri na mikoa hukutana kwa ajili ya kufanya tathimini  ya kuangalia maeneo waliyofanikiwa,yenye changamoto na kuweka mikakati ya kuondokana na changamoto hizo.

Aidha anasema ,changamoto tatu zilizobainika  kwenye tathimini ya lishe ni Fedha inayotengwa kwa ajili ya mtoto bado haitoshi kutekeleza afua za lishe ipasavyo na hivyo kuwapa jukumu wataalam wafanyie tathimini lakini pia na halmashauri waone uwezekano wa kuongeza fedha ili ile sh.1,000 iwe ni kiwango cha chini,lengo ni kuwa na uwezo mzuri zaidi kuwafikia watoto wote katika eneo la lishe.

Anasema changamoto nyingine  ni kulegalega kwa baadhi ya mikoa watoto kupata chakula shuleni huku akisema,kwenye eneo hilo wamekubaliana viongozi wa mikoa wakaone ni wapi kunakosababisha watoto hawapati chakula vizuri shuleni.

“Changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa watalaam ambao anasema Serikali inaendelea kuajiri maafisa Lishe ili kupunguza uhaba wa watumishi wa lishe ili waweze kufika vizuri kwenye ngazi ya vijiji na mitaa kutoa elimu na kusimamia masuala ya lishe na hatimaye kuboresha zaidi suala la lishe.

Aidha anasema,upo mpango unaoanza kutekelezwa na serikali wa kuongeza virutubishi kwenye chakula iwe ni unga wa mahindi,ngano,mafuta ya kula.

Afisa Lishe mkoa wa Dodoma Herieth Carin katika taarifa  ya Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kipindi cha Julai 2023-Juni 2024 mkoani humo anasema ,kati ya Shilingi milioni 698.3 zilizotengwa kutekeleza shughuli za Lishe kwa kipindi cha Julai,2023 – Juni,2024, Shilingi 686.9  zilitolewa na kutumika sawa na asilimia 98.4.

Aidha anasema,Halmashauri zimefanikiwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afua za Lishe kutoka asilimia 82 (2022/23) hadi asilimia 98 (2023/24) huku asilimia ya Shule zinazotoa chakula zikiongezeka kutoka asilimia 85 (2022/23) hadi kufikia asilimia 99.7 (2023/24).

 Kwa mujibu wa taarifa hiyo kiasi  cha fedha za ndani zilizotumika kwa      kila mtoto chini ya miaka mitano Bahi sh.1,514,Chamwino sh.1,174,Chemba sh.1,584,Dodoma Jiji sh.1,780,Kondoa sh.1,476,Kondoa Mji sh.2,425,Kongwa sh.1,326 na Mpwapwa sh.1,099.

 Vile vile anasema,kwa kipindi cha kampeni ya vitamini A, Mkoa umefanikiwa kutoa matone ya Vitamin A kwa watoto walio na umri wa miezi 6 -59 kwa asilimia 110 .

Hata hivyo pamoja na mafanikio hayo anasema bado kuna changamoto katika utekelezaji wa mkataba huo ikiwemo idadi ndogo ya wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari wanaokula chakula shuleni,upungufu wa mashine za urutubishaji wa unga wa mahindi katika Halmashauri,na chakula kutorutubishwa.

Anasema mikakati iliyopo kuzikabili changamoto hizo ni Halmashauri kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi wote,Mkoa kwa kushirikiana na Mdau wa SANKU kuwezesha Halmashauri kufunga mashine za kufanya urutubishaji na kusimamia vyema Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji na kuendelea kutoa elimu ya afya na Lishe kwa Jamii.

 Mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule anazungumza katika kikao hicho  anasema utengaji wa fedha kwa kila mtoto wa umri chini ya miaka mitano ni asilimia 98 huku akisema uwezo wa  kufikia asilimia 100  wanao kwa mwaka huu wa fedha.

Hata hivyo ametaka kujua fedha zilizotolewa kama zimetumika kwa malengo mahususi ya kufanya mabadiliko kwenye lishe huku akiwaagiza wataalam kufuatilia hilo.

Naye  Afisa Elimu Vicent Kayombo anawaagiza  walimu wakuu shule za msingi na sekondari kutenga angalau heka mbili kwa ajili  ya kilimo cha bustani za mbogamboga na miti ya matunda.