November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mikakati ya Tanzania kuwekwa kwenye ramani ya dunia katika masuala ya ubunifu yaandaliwa

Na Joyce Kasiki,timesmajira,online,Dodoma

SERIKALI imesema itandelea kutoa kipaumbele kwenye masuala ya  ubunifu ili kuleta tija kwenye maendeleo ya Sayansi na Teknolojia nchini.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga wakati wa ufunguzi wa warsha inayohusiana na masuala ya Teknolojia na ubunifu iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

Warsha hiyo imelenga kujadiliana na kuweka mikakati ya pamoja katika kuimarisha nafasi ya Tanzania katika ramani ya Dunia katika masuala ya ubunifu.

“Ripoti zinaonyesha kuwa  nchi yetu imekuwa ikipiga hatua katika masuala ya ubunifu na kupanda juu ambapo mwaka 2020 ilikuwa nchi ya nne Kusini mwa Jangwa la Sahara ikitanguliwa na Afrika Kusini ,Kenya na Mourisiuos .”amesema Kipanga na kuongeza kuwa

Hata hivyo amesema bado nchi inayo nafasi ya kufanya vizuri huku akiwataka wajumbe wa warsha hiyo kuweka mikakati thabiti ya kuwezesha eneo la ubunifu liweze kuleta tija zaidi.

Amesema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 imeelekeza hatua mbalimbali za kuchukua ili mchango wa sayansi Teknolojia na ubunifu ulete tija katika  maendeleo kijamii na kiuchumi.

“Hali kadhalika mpango wa tatu wa miaka mitano wa maendeleo unasisitiza matumizi ya sayansi teknolojia na ubunifu katika nyanja zote  ili kuleta tija na ufanisi “amesema Kipanga na kuongeza kuwa

“Naamini mjadala huu uliosheheni wataalam mbalimbali utatoa na kuweka mikakati itakayohakikisha nafasi ya nchi yetu inapaa katika ramani ya Dunia kuhusiana na masuala ya ubunifu,”amesema

Aidha amesema Tanzania  imeendelea kutambua masuala ya ubunifu ambapo mwaka 2019 ilianzisha mashindano ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU)  ambapo zaidi ya bunifu 1,700 zilitambulika na zaidi ya bunifu 130 zipo katika mchakato ili ziweze kuleta tija .

“Kwa hiyo jukumu letu ni kuweka kipaumbele katika kuweka bajeti toshelezi  kuhakikisha tunakwenda kusimamia neno hili kikamilifu.”amesisitiza