December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miili ya watu wawili yaopolewa Z.Victoria,watatu wakiendelea kutafutwa

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mwanza 

Miili ya watu wawili kati ya watano ambao walikuwa hawajapatikana baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama ndani ya Ziwa Victoria imeopolewa  na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa ushirikiano wa wananchi wa Wilaya ya Sengerema mkoani hapa.

Mtumbwi huo uliokuwa umebeba watu zaidi ya 20, ulizama  Agosti 05,2024 majira ya 2:00 usiku katikati ya Kisiwa cha Yozu na Ziragula wakati wakitokea  kwenye sherehe ya mashabiki wa Yanga (Yanga day) iliyofanyika kisiwani Yozu wakielekea kitongoji cha Itabagumba ambapo watu 17 waliokolewa.

Agosti 07.2024 majira ya saa 5 asubuhi (11:00hrs)  eneo la Butala  Mawe mawili, kisiwa cha Yozu, Jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi  wamefanikiwa kuopoa miili ya watu wawili ambao ni Mashauri Ishabakaki(42), mkazi wa Mbugani na Jonathan

Mutasyoba(50) .

Akizungumza mkoani hapa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilbroad Mutafungwa ameeleza kuwa jitihada za kutafuta watu wengine watatu zinaendelea ambao ni Masaka  Angote(60) mkazi wa Burihaeke, Edward Kachelemi(46), mkazi wa Burihaeke na Shija Paschal(30) mkazi wa Yozu ambao bado hawajapatikana.

 “Miili ya marehemu waliopatikana imekabidhiwa kwa ndugu kuendelea na taratibu za mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu,”ameeleza DCP Mutafungwa.