Na Mwandishi wetu, timesmajira
KUTOKANA na kuimarika kwa Ulinzi katika hifadhi ya Taifa ya Burigi -Chato, Ng’ombe 261 wamekamatwa wakiwa wanachungwa ndani ya hifadhi hiyo.
Akizungumzia tukio hilo,Afisa Uhifadhi Mkuu wa ldara ya Ulinzi,Deogratius Mwageni amesema ng’ombe hao wamekamatwa eneo la Kimbogo na Miringa katikati ya hifadhi hiyo.
Mwageni amesema kukamatwa kwa mifugo hiyo ni kutokana na kuimarika Ulinzi na akaonya baadhi ya viongozi wa vijiji kushirikiana na wahalifu kuingiza Mifugo hifadhini.
Mwanasheria na Kitengo cha Uchunguzi na Kuendeshaji Kesi katika hifadhi ya Burigi -Chato, Emmanuel Zumba amesema Mifugo hiyo iliyokamatwa itafikishwa Mahakamani.
“Tumekuwa na operesheni ya kukamata Mifugo hifadhini kuanzia Julai 2024 hadi sasa tumekamata Ng’ombe zaidi ya 1000 na tunakesi 165 na 74 zimetolewa uamuzi na tumeshinda “amesema.
Mkuu wa hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Ismail Omar amesema Ulinzi wa hifadhi hiyo sasa umeimarika hali ambayo inasabisha utulivu wa Wanyamapori na Wanyamapori kuanza kuongezeka.
Omar amesema ,changamoto ambayo wanaendelea Kuidhibiti ni kuingizwa Mifugo kutoka nchi jirani na baadhi ya viongozi wa vijiji wasio waadilifu .
“Tuna vijiji 38 vinavyozunguka hifadhi sasa baadhi ya maeneo kuna viongozi wanapokea wafugaji kutoka nchi jirani na kuingiza Mifugo hifadhini hasa katika maeneo ya milima na mabonde”amesema
Hata hivyo, amesema kutokana na matumizi ya Teknolojia za kisasa katika Ulinzi Mifugo imekuwa ikikamatwa na kufikishwa Mahakamani.
“Tunaomba viongozi wachache wa vijiji waache kuhujumu hifadhi na wajuwe lazima tutawakamata wao na Mifugo iliyoingizwa hifadhini”amesema.
Hifadhi ya Burigi -Chato ilianzishwa mwaka 2019 baada ya kupandishwa hadhi na sasa ni miongoni mwa hifadhi bora nchini ambazo Utalii umeanza kuimarika.
More Stories
Waziri Lukuvi aeleza maono ya Isimani ijayo
Madiwani Korogwe TC wahakikishiwa maji ya uhakika
CHADEMA wampongeza Mkurugenzi Mpanda