November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mifugo yote kuuzwa kwa kupimwa uzito

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dodoma

SERIKALI inaweka utaratibu wa kuhakikisha mifugo yote inauzwa kwa kupimwa uzito, badala ya kukisia kama inavyofanyika sasa kwenye minada na maeneo mengine nchini.

Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mafunzo ya wafanyabiashara na wajasiriamali wa mkoa huo yaliyoandaliwa na Wakala wa Vipimo (WMA) ili kuwawezesha kujua matumizi sahihi ya vipimo na ufungashaji.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge, Mumba amesema wafanyabiashara na wajasiriamali wanatakiwa kuhakiki mizani wanayotumia kwenye manunuzi.

“Kwa hiyo nazishauri mamlaka zetu za Serikali za Mitaa kwenye maeneo yao kuna masoko mbalimbali yakiwemo magulio na baadhi ya minada, haina vipimo sahihi au haitumii mizani, kwa hiyo tunapoendelea Serikali inaweka utaratibu kuhakikisha mifugo yote inauzwa kwa kupimwa uzito badala ya kukisia,” amefafanua Mumba.

Amesema kwamba kwa kadri wananchi watakavyozingatia suala la vipimo, manufaa yake yataonekana kwa wadau wote, anayezalisha na yule anayekwenda kutumia hiyo bidhaa, kwani atakuwa na uhakika kwamba thamani ya fedha yake inalingana na kitu kile ambacho amepewa.

Baadhi ya wafanyabiashara na wajasiriamali yakipunga mikono kuashiria kumkaribisha mgeni rasmi Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba kufungua semina yao iliyoandaliwa Wakala wa Vipimo (WMA) ili kuwawezesha kujua matumizi sahihi ya vipimo na ufungashaji. Alifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge, jana.

“Hicho ndicho kikubwa zaidi, kwani pande zote zinafaidika na matumizi sahihi ya vipimo,” amesema Mumba.

Amesema semina hiyo itawezesha wafanyabiashara na wenye viwanda kuweza kuelewa kwa kina suala la uzingatiaji wa vipimo sahihi.

Kwa mujibu wa Mumba kupitia kampeni mbalimbali, Serikali imekuwa ikiendesha kaguzi ili kuhakikisha wananchi na wadau wote wanazingatia suala zima la vipimo kutokana na unyeti wake katika maendeleo ya nchi yetu.

Ameongeza kwamba wamekuwa wakipokea malalamiko kadhaa kuhusiana na matumizi batili ya vipimo kwenye mkoa huo na kupitia WMA, wameendelea kushirikiana kuhakikisha wadau wote wanaendelea kutumia vipimo sahihi.

Amezidi kufafanua kwamba Dodoma peke yake kuna viwanda zaidi ya 3,000, vikiwemo vya kusindika alizeti, unga, viwanda vya mvinyo, hivyo suala la kuzingatia vipimo ni muhimu sana kuanzia shambani wakulima wanapokuwa wanauza mazao.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Stella Kahwa, amesema WMA jukumu lake kuu ni kumlinda mlaji kupitia matumizi sahihi ya vipimo.

“Kwa hiyo tuna kazi ya kuhakiki vipimo na kuhakikisha vinatumika kwa usahihi,” amesema Kahwa na kuongeza; “Tuna jukumu la kuhakikisha kwamba bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu zinafungashwa kwa usahihi, kwa sababu ili uweze kupenya kwenye soko la kimataifa ni lazima ufungashaji wa bidhaa zako uzingatie miongozo yote ya Shirika la Vipimo Duniani.”

Amesema WMA ni mwanachama hai wa Shirika la Vipimo Duniani, hivyo wao wanatakiwa kutoa miongozo hiyo kwa wazalishaji wa ndani ili waweze kushindana kimataifa na kitaifa.

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba kufungua semina iliyoandaliwa Wakala wa Vipimo (WMA).

Ameongeza kwamba ili kuelekea Tanzania ya Viwanda , lazima vipimo sahihi vizingatiwe na kwamba wanafanya semina za aina hiyo nchini kote ili kuwafikia wafungashaji na wazalishaji wadogo wadogo waweze kukua, wawe wazalishaji na wafungashaji wa kati na mwisho wa siku wawe wa kimataifa.

“Kwa hiyo tunatumia semina hizi kwa ajili ya kuwaelimisha wafungashaji na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali nchini na sasa tupo mkoa wa Dodoma na mikoa mingine zimekwisha fanyika semina na mafunzo kama haya kwa ajili ya kujenga uchumi wa viwanda Tanzania,”amesema Kahwa.

Naye Kaimu Meneja wa WMA mkoa wa Dodoma, Karim Zuberi, alisema semina hiyo ni kwa ajili ya kuelimisha matumizi sahihi ya vipimo na ufungaji kwa wafanyabiashara na wajasiriamali mbalimbali wenye viwanda na wengineo.

Amesema semina hiyo ni mwendelezo wa semina za mara kwa mara ambazo wamekuwa wakizifanya ambapo wanapokuwa maeneo ya uzalishaji wanatoa elimu kwa mfanyabiashara mwenye kiwanda mmoja mmoja na kwa watumishi wa Serikali na wamekuwa wakishirikiana na watendaji wa Kata.

Zuberi amesema wao kama mkoa ni kuhakikisha Dodoma inaondokana na matumizi yasiyokuwa sahihi ya vipimo.

Amesema watakuwa wanafanya kaguzi mbalimbali zikiwemo za kawaida na za kushtukiza. Zuberi alisema kwa sasa vipimo vimeongezeka na wanakagua vipimo vingi, hivyo hali ni nzuri.

Washiriki wa mafunzo hayo waliahidi kuzingatia mafunzo hayo na kuyatumia katika shughuli zao. Wamesema hata walaji watakuwa na uhakika na kile walichopimiwa na wameahidi kuwa walimu kwa wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi aliyefungua mafunzo hayo, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba.

Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake Wapambana Mkoa wa Dodoma, Asuna Baya, alishukuru kupatiwa mafunzo hayo na kwamba yatawasaidia kwenye shughuli zao.

Ameipongeza WMA kwa kuwapatia mafunzo hayo na kwamba yatawasaidia kubadilika na kuwa na nidhamu ya vipimo kwa kuondokana na vipimo vya mazoea. Alisema Dodoma sasa hivi ni makao makuu, hivyo kuna haja ya kuzingatia vipimo wanavyoelimishwa na ili kufanikiwa hilo ni lazima wawe na hofu ya Mungu.