November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mifugo 2,225 yakamatwa, ikisafirishwa bila kibali

Na Mwandishi wetu Jeshi la Polisi, Timesmajira Online

Jeshi la Polisi Nchini kupitia kikosi cha Kuzua na kupambana na Wizi wa Mifugo (STPU) katika operesheni mbalimbali wamefanikiwa kukamata jumla ya mifugo 2,225 ambayo ilikua inasafirishwa bila kufuata utaratibu ambapo mifugo hiyo iliingizwa katika mapori tengefu pamoja na vyanzo vya maji.

Akitoa taarifa hiyo leo Januari 30, 2023 Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Simon Pasua amesema katika operesheni hiyo iliyofanyika mwezi huu watuhumiwa 48 walikamatwa wakiwa na mifugo hiyo kwa makosa mbalimbali.

Kamanda Pasua amesema makosa hayo ni pamoja na kuingiza mifugo katika vyanzo vya maji, kusafirisha kutoka mkoa mmoja kwenda Mkoa mwingine bila kuwa na kibali na kuingiza mifugo kiholela katika mapori tengefu ama vyanzo vya maji.

ACP Pasua alibainisha kati ya mifugo iliyokamatwa 1,263 ilikamatwa katika pori tengefu la Pololeti wilayani Ngorongoro na 962 ilikamatwa ikisafirishwa kutoka Mkoa wa Morogoro kwenda mkoa wa Ruvuma bila ya kufuata taratibu za kisheria.

Kamanda Pasua amewataka wafugaji wote nchini kuacha mara moja tabia ya kuhamisha mifugo kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine bila ya kufuata utaratibu wa kupata vibali toka serikalini kwani jeshi hilo halitaruhusu jambo hilo kutokea na litachukua hatua kwa kukamata mifugo hiyo.

Halikadhalika kwa upande wa wafugaji wenye tabia ya kuingiza mifugo ndani ya mapori tengefu ama vyanzo vya maji amewataka kuacha mara moja kwani mifugo yao itakamatwa na kutaifishwa.

Sambamba na hilo pia amesema Jeshi hilo kwa kipindi cha mwezi januari mwaka huu limefanikiwa kutoa elimu kwa wafugaji kote nchini katika minada ya mifugo kupitia vipindi 110 vilivyoandaliwa.