January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mifarakano ya wazazi inavyoathiri malezi na makuzi ya watoto

Na Joyce Kasiki

Kukosa malezi ya wazazi,walezi ama hata jamii ,ni moja ya changamoto inayowakabili baadhi ya watoto nchini na kulazimika kuishi bila makazi na kwenye mazingira magumu ,yanayohatarisha ukuaji na maendeleo yao ya awali kama inavyoainishwa katika Programu Jumuishai ya Taifa wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.

Umri wa miaka 0-8 kwa mujibu wa tafiti za kisayansi ndiyo umri unaoamua hatma ya mtu kwenye umri wa utu uzima wake,lakini lipo kundi linakosa misingi mizuri ya malezi na kujikuta wakiishi bila malezi ya wazazi kwa maana ya baba na mama na hivyo kuishi katika mazingira magumu na mwisho wa siku kujiingiza kwenye uvutaji wa gundi mitaani.

Amina Juma mkazi wa Kigamboni jijini Dodoma mama aliyeachwa na watoto wawili anasema watoto wake ni miongoni mwa watoto waliotelekezewa na baba yao .

 Katika simulizi yake anasema,yeye na mumewe walizaa watoto wawili  ,ambapo baada ya miaka michache ,mumewe aliondoka nyumbani bila taarifa yoyote na kumuacha na watoto wakiwa wadogo.

“Mume wangu  alipoondoka nilikuwa nafanya kazi saluni , kipato kilikuwa ni kati ya sh.2000 hadi 3000,kilikuwa ni kidogo hivyo hakikuweza kunitosheleza na watoto…,kutokana na hali hiyo na mimi  niliamua kuondoka nikawatelekeza watoto wangu kwa jirani nikaenda Tanga kutafuta pesa .”

Amina  anasema ,alifanya hivyo kwani hakuwa na pesa hivyo alishindwa kumudu kuwatunza watoto kwani walikuwa hata wakiumwa hakuwa na namna ya kuwasaidia.

Hata hivyo anasema baada ya kutafutwa sana na ndugu,jamaa na marafiki aliamua kurudi nyumbani ambapo aliwakuta watoto wake kituo cha polisi, baada ya kuwachukua watoto akaanza maisha upya na hali ya maisha ikiwa bado ngumu.

“Nilianza kufanya biashara ndogo ndogo mwisho wa siku nikaanza kujiuza ili nipate pesa za kuwasomesha watoto wangu,ilitokea kama bahati nikapata mwanaume aliyenipatia  shilingi milioni  3 ,nikaenda kulipa ada ya mtoto ya mwaka mzima , wakati huo mkubwa alikuwa darasa la kwanza,

“Kwa  pesa hiyo  ,nikanunua vifaa vya saluni  nikaanza biashara yangu ,na chumba nilichokuwa nalala na waoto  ndiyo hicho hicho nilikitumia kama ofisi .”anasema Amina

Hata hivyo anasema baaadaye akaingia kwenye mikopo akakuza biashara yake,akajifunza kutengeneza bidhaa mbalimbali na biashara ilipochanganya akatafuta chumba cha biashara na sasa anaendelea na maisha ambapo mtoto mkubwa kwa sasa yupo darasa la tano na mdogo yupo darasa la tatu.

Amina ameishauri serikali ,kuwachukulia hatua wanaume wanaotelekeza watoto ili iwe fundisho kwa wengine na kuwafanya wawatunze watoto wao lakini pia wajiepushe na mifarakano katika ndoa .

Mtaalam  wa Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoka Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya Watoto (CiC) Davis Gisuka anasema sayansi ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto inaonesha ,mifarakano ya wazazi inamkosesha mtoto mambo mengi ikiwemo mapenzi ya baba ya mama  na wengine kuangukia kwenye malezi ya mtaani  kitu ambacho ni hatari  katika makuzi yake.

“Mtoto akishakosa mapenzi ya baba na mama tayari inaathiri ukuaji wake  ,mtoto atakosa muda wa kukaa na wazazi wote wawili ,maana yake ni kwamba hata yale mahusiano ya mtoto na wazazi pia yanapungua kwa kiasi kikubwa,

“Kwa hiyo mtoto kama hayupo karibu na hawa watu maana yake wanadidimiza makuzi yake ya ubongo,na makuzi ya ubongo yakidumaa ,hata uwezo wake wa kujifunza atakapokuwa anaingia darasani  katika ujifunzaji nako ufaulu wake hautakuwa mzuri.”anasema Gisuka

Aidha anasema ,mifarakano ya wazazi inachangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa watoto wasio na makazi  na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa sababu mtoto anakosa msaada ambapo anaona kama hapati zile huduma za msingi anaona bora aende mtaani kujitafutia.

“Sasa kama ni mtoto ambaye yupo chini ya umri wa miaka minane moja kwa moja inaathiri makuzi yake ya ubongo,na ukishaathiri makuzi ya ubongo hata makuzi yake kwa ujumla yanaathirika ,hii ni pamoja na makuzi ya mwili kwa sababu atakuwa hapati chakula  cha kutosha kwa sababu mwili unakua vizuri kwa kupata chakula kizuri,

“Maana yake sasa, anakosa zile afua tano za kile kihunzi cha malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ,atakosa lishe bora ,hatakuwa na ulinzi ,hatapata fursa ya ujifunzaji ,hata habari afya kwake itakuwa changamoto maana nani atakuwa anampeleka kwenye kliniki kupata huduma za afya ,anakosa malezi yenye mwitikio,kwa hiyo akivikosa hivyo ni lazima adumae kimwili ,atadumaa makuzi ya ubongo na atadumaa kiakili.”

Kufuatia changamoto zilizopo katika jamii za malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ,Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ambayo imelenga watoto wenye umri wa miaka sifuri hadi minane.

Programu hiyo imelenga kuwekeza moja kwa moja kwenye maendeleo ya mwanadamu kwa kukuza malezi jumuishi yenye tija katika uchumi kwa kuhimiza ushiriki wa sekta mbalimbali kutoa malezi jumuishi kwa kuzingatia vipengele vitano ambavyo ni Lishe ya kutosha tangu ujauzito,malezi yenye mwitikio ,fursa za ujifunzaji wa awali pamoja na ulinzi na usalma wa mtoto na afya bora.

Aidha kwa mujibu wa PJT-MMMAM ulimwengu mzima una watoto milioni 250 wenye umri chini ya miaka mitano ambao wanapatikana kwenye nchi za uchumi wa chini na zile za uchumi wa kati ambao wapo kwenye hatari ya kutofikia kwenye hatua zao za ukuaji .

Pia  takribani theluthi mbili sawa na asilimia 66 ya watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano walio Kusini mwa Jangwa la Sahara wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua timilifu za ukuaji kutokana na kukosa malezi bora,umasikini ,utapiamlo pamoja na matatizo mengine ya kijamii na kiuchumi.

Mrakibu Msaidizi wa Polisi Christer  Kayombo anasema ,migogoro ya wazazi na kesi zinazofika kwenye dawati i zinazohusiana na migogoro ya familia ni nyingi .

Anasema wamekuwa wakishughulikia kesi hizo kwa namna tofauti ikiwa ni pamoja na kuzipeleka Ustawi wa Jamii,kwa viongozi wa dini na zile za jinai huzipeleka mahakamani.

“Kwa mfano kama tukiona ni kesi za kutelekeza au kushindwa kutunza familia tunazifungulia kesi za jinai na mashauri hayo tunapeleka mahakamani ,lakini kuna wakati inakuja migogoro haina jinai,hivyo kama haina jinai tunaielekeza Ustawi wa Jamii ambayo kwa mujibu wa sheria ya mtoto ,Maafisa Ustawi wa Jamii ndiyo wenye mamlaka ya kushughulikia masuala yote yanayohusiana na watoto,

“Kama ni migogoro ya wazazi ,malezi ya watoto ,na sasa hivi kuna wimbi la wazazi kugombaniana watoto kwa kuwachukua kwa mbinu mbalimbali,kwa migogoro kama hii pia tunaielekeza makanisani au misikitini ambako kuna uwezekano wa wanafamilia hao kurudishwa na kuwa wamoja tena na hivyo kuendelea na malezi ya watoto .” anasema Kayombo

Hivi karibuni,Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima anasema kuwa hapa nchini kumekuwa na ongezeko la mashauri ya migogoro ya ndoa kwa asilimia 8.3 ndani ya miezi 11, hadi kufikia Aprili mwaka huu mashauri yaliyoshughulikiwa yalikuwa 31,380 ikilinganishwa na 28,773 yaliyoshughulikiwa 2022/2023 ambayo ni ongezeko la mashauri 2,607 sawa na asilimia 8.3.

Aidha anasema katika kipindi  cha Julai 2023 hadi Aprili mwaka huu ,Wizara yake wa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI imewatambua watoto wanaoishi na kufanya kazi katika maeneo mengine yenye mikusanyiko ya shughuli za kiuchumi wapatao 8,372 kutoka Halmashauri zote nchini ikilinganishwa na watoto 5,728 waliotambuliwa kipindi cha Julai 2022 hadi Aprili 2023.

“Kuna ongezeko la watoto 2,644, ongezeko hili linaonesha ukubwa wa tatizo la watoto wa mitaani kuendelea kuongezeka kwa sababu mbalimbali ikiwemo mifarakano ya wazazi.”

Dkt.Gwajima anatoa wito wa viongozi wa dini kuendelea kutoa mafunzo wa wanaofunga ndoa na kwa vijana kupitia mikusanyiko  katika madhehebu yao ,ili kuwaandaa kubeba majukumu ya ndoa kabla ya kuingia humo ili kuleta utulivu wa ndoa na familia ambao ni msingi mkubwa wa ustawi wa watoto na jamii kwa ujumla.

Naye Askofu wa Kanisa la Kalmeli Asemblies of God Dkt.Evance Chande anasema mara nyingi kanisa limekuwa likitoa nasaha za kuwafanya wazazi waishi katika maisha ambayo hayawaathiri watoto katika malezi na makuzi yao wa ujumla .