December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka mitatu ya Rais Samia ilivyoleta mageuzi kwa wanufaika wa TASAF

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Maswa

KASI ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wanufaika wa Mpango wa Kunuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) inazidi kuleta matokeo chanya ndani ya jamii.

Wanufaika wa mpango huo wanakiri kupata mafanikio makubwa chini ya uongozi wa Rais Samia, ambapo baadhi yao, wameanza kuomba kwa ridhaa yao kuondolewa kwenye mpango huo ili kupisha wengine wenye kipato duni kuweza kunufaika.

Miongoni mwa mashuhuda jinsi walivyonufaika na TASAF, ni wanufaika wa mpango huo wilayani Maswa, ambao wanasema bila TASAF maisha yao yangekuwa magumu na pengine wasingekuwepo.

Mmoja wa wanufaika wa TASAF wilayani Maswa, Jane Charles Chenya (46) anamshukuru Rais Samia na Serikali kwa ujumla kwa kuanzisha mpango huo, kwani umemwezesha kuondokana na hali ngumu ya maisha.

Anasema ameondokana na hali hiyo baada ya kutumia ruzuku aliyopewa kuanzisha biashara ya mama lishe.

Jane Mkazi wa Kijiji cha Shanwa, Kata ya Shanwa, Halmashauri ya Wilaya Maswa mkoani Simiyu, ametoa ushuhuda huo wakati akizungumza na gazeti hili.

Anasema kabla ya TASAF kumshika mkono mwaka 2015, alikuwa akiishi maisha magumu yaliyotokana na kufiwa na mume wake na kumuachia watoto wadogo watatu.

Anasema baada ya kifo cha mumewe, alijikuta hana msaada ya kutunza familia, hivyo alianza kulimia watu vipande vya mashamba, lakini kile alicholipwa kilikuwa hakitoshelezi kupata chakula na mahitaji ya watoto kwenda shule.

“Sikuwa na uhakika wa kupata hata mlo mmoj, sikuwa nasomesha watoto, sikuwa na uwezo wa kuwanunulia mahitaji ya shule, ikiwemo daftari, viatu, sare za shule na mahitaji mengine.

“Nilikuwa naangaika sana. Lakini baada ya kuingizwa kwenye mpango wa TASAF, mwaka 2015 na kupewa ruzuku ya sh. 30,000 ndipo nilianzisha mradi wa mama lishe,” anasema Bi. Jane.

Alitumia fedha hizo kununua unga wa ngano, mafuta ya kupikia na sukari na kuanza mradi wa mama lishe kwa kuanza na kupika chai. Anasema kadri TASAF ilivyokuwa ikiendelea kumpa ruzuku, aliongezea na faida aliyokuwa akipata kwenye mradi wake kuongeza mtaji hadi alianza kupika chakula cha mchana na usiku.

Kwa mujibu wa Jane, wakati anaanza kupika chakula alianza kilo mbili za mchele kwa siku, lakini sasa hivi anapika kilo saba.

“Wakati ule nilikuwa nahudumia wateja kama 10 mchana peke yake, lakini sasa hivi napata wateja zaidi ya 20 wa chakula wa mchana hapo bado wale wa usiku,” anasema Jane na kuongeza;

“Napika wali, nyama, kuku, ugali, mahitaji yote ya wateja wangu yanakuwepo,”anasema Jane.

Jane anasema kadri wateja wake wanavyoongezeka, anaongeza mtaji wake, ambapo kwa sasa kila siku asubuhi anauza chai, supu, chapati, maharage.

“Mambo yangu yamenyooka niko vizuri, nina maisha mazuri,” anasema Bi. Jane na kwa kuthibitisha hilo, anasema wakati mume wake anafariki mtoto wao wa kwanza alikuwa na miaka mitano, mwingine miwili na wa tatu mwaka mmoja.

Anasema kupitia biashara yake hiyo amesomesha mtoto wake wa kwanza aitwaye Paskazia Charles hadi sekondari na baadaye alimsomesha chuo cha uuguzi.

“Kwa sasa Paskazia anafanyakazi ya uuguzi Dodoma na mtoto wangu wa pili, Sarapia Charles alikomea kidato cha nne, kwa sasa anaishi Dar es Salaam ambako anafanya biashara zake na zinaenda vizuri,” anasema Jane.

Kwa upande wa mtoto wa tatu, Sijasimini Charles, ambaye aliachwa na baba yake akiwa na mwaka mmoja, anasoma Sekondari ya kutwa ya Nyalikungu kidato cha nne.

Anaongeza kwamba pamoja biashara yake ya mama lishe, amejiunga kwenye kikundi cha Upendo Biafra A, ambacho kina wanawake 10 wanufaika wa TASAF.

Anasema kila siku jioni wanajiwekea akiba ya sh. 5,000 na fedha hizo ni sehemu ya faida ambayo anapata kila siku kupitia biashara yake hiyo ya mama lishe, lakini pia anakuwa na ziada ya kutunza familia.

“Kwa kweli tunawashukuru TASAF kwa kutuletea maboksi kwa ajili ya kuweka akiba kwenye kikundi, kwani mtu akitaka kukopa, tunajikopesha wenyewe,” anasema Bi. Jane.

Bi. Jane, anasema kikundi hicho kinamsaidia, kwani amekuwa akipata mkopo, hivyo kuongeza mtaji kwenye biashara zake, ambapo mara ya mwisho alikopa sh. 80,000.

“Tunakopeshana hadi sh. 150,000 na baadaye mkopaji anazirudidsha fedha hizo. Mfano, mimi nilipokopa sh. 80,000 niliongeza mtaji kwa kununua unga wa ngano na mafuta,” anasema.

Anasema kwa sasa yupo vizuri na akiendelea hivyo, biashara yake itazidi kupanuka zaidi na ana mpango ya kufungua duka ili aondokane na moto (biashara ya kupika chakula).

Kwa mujibu wa Jane, kwa hatua ambayo TASAF imemfikisha, hata ikitokea siku moja TASAF ikawa haipo, anaweza kuendesha maisha yake bila kuyumba.

“Ninaweza kusimama mwenyewe kwa sababu sasa hivi nina mtaji…hata waseme leo mwisho, mimi niko vizuri,” anasema.

Jane anasema kutokana na biashara yake kupanuka ameweza ‘kuajiri’ binti wa kumsaidia kazi ambaye anamlipa mshahara kila mwezi. Aidha, anasema analipa kodi ya eneo analofanyia biashara bila wasiwasi.

“Eneo ninalofanyia biashara ni nyumba yetu ya urithi mimi na wenzagu, kinachopatikana kutokana na kodi ya pango kutoka kwa wapangaji tunagawana wote, lakini kwa sababu mimi ni mfanyabiashara lazima nilipe kodi siwezi kusema nisilipe kwa sababu ni nyumba yetu.

Ili nione kwamba nafanyakazi ni lazima nilipe kodi kwa mwezi nalipa sh. 30.

Anapoulizwa kuhusiana na mtazamo wa baadhi ya wanufaika wa TASAF, kudai kwamba ruzuku (fedha) zinazotolewa na TASAF ni ndogo haziwezi kuwasaidia, Jane alikuwa na haya ya kusema;

“Fedha za TASAF ukizifanyia biashara zinatosha , lakini ukizipeleka kwenye mambo mengi haitoshi. Nawashauri wanufaika wenzangu wanapopata fedha hizo waanzishe biashara ndogo ndogo na ufugaji wa kuku, bata, mbuzi au biashara ya kutembeza ili kuzalisha hiyo hela.

Hela ya TASAF sio ya kununulia nguo, kunywea pombe au kununua chakula cha nyumbani.”

Mmoja wa wateja wa Jane, Charles Blandes, anaishukuru TASAF, kwa kumuinua Jane, kwani awali alikuwa na hali ngumu ya maisha, na hakuna alijua kama atafika hapo halipo.

“Watu wengine kijijini wanamtolea mfano, amekuwa mtu wa kuigwa, ni miongoni mwa wanawake wapambanaji na hii hiyo imetokana na Serikali kuanzisha mpango huu wa TASAF,” anasema, Bw. Blandes.

Aidha, wanawake 15 wa Kikundi cha Amani Maganju kinachoundwa na wanufaika TASAF wameanzisha miradi mbalimbali iliyowawezesha kujiingizia kipato cha kujikimu ndani ya familia zao na wameweza kujiwekea akiba ya sh. milioni 9.

Kupitia utaratibu wa kujiwekea akiba ndani ya kikundi, hivi karibuni wanakikundi hao wamegawana sh. milioni 6, kati ya sh. milioni 9, huku kila mmoja akipata mgao wa sh. 400,000.

Kikundi cha Amani Maganju kipo katika Kijiji cha Ipililo, Kata ya Ipililo, Halmashauri ya Wilaya Maswa, mkoani Simiyu.

Mwenyekiti wa Kikundi, Pendo Pipi (33) anasema waliingizwa kwenye TASAF kutokana na hali duni walizokuwa nazo na baada ya kupata ruzuku, kila mmoja alianzisha mradi mdogo mdogo wa kumuingizia kipato.

“Sisi wote unavyotuona hapa tulikuwa na hali ngumu sana, tulikuwa tukiishi kwa kufanya vibarua vya kulimia watu mashamba msimu wa kilimo.

Watoto walikuwa hawawezi kwenda shule na hata walipougua matibabu ilikuwa shida,” anasema Pendo na kwamba kutokana na hali zao, hakuna hata mtu mmoja ambaye wangemkimbilia akawakopesha hela.

Anasema anaishukuru Serikali, kwani baaba ya kuingizwa TASAF na mwaka uliofuata kuanza kupata fedha, kila mmoja alitumia fedha hizo kuanzisha biashara ndogo ndogo na miradi ya ufugaji wa kuku, bata, mbuzi, kondoo na wengine kuanzisha genge.

“Kila mmoja ana biashara anayofanya.” Anasema Agosti 5, 2022 wakiwa wanufaika wa TASAF walianzisha kikundi hicho na kuanza kujiwekea akiba, na kwamba Agosti, 2023 walikuwa wamefikisha akiba ya sh. milioni 9.

Mjumbe wa kikundi hicho, Gudawa Mbesa (54) anaungana na Mwenyekiti wake, Pendo kuipongeza Serikali, kwani ruzuku ya TASAF, imewawezesha wawe na shughuli za kufanya na kujiingizia kipato.

Aidha, anasema hata wanapokuwa na shida wanaenda kwenye kikundi na kukopa fedha na kutatua shida zao.

“Kwanza hakuna sehemu ambayo tunngeenda tukakopeshwa hela, maana jamii ilituona maskini, lakini baada ya kuanzisha kikundi na kujiwekea akiba, kila mmoja akiwa na shida anakimbilia kwenye kikundi anakopeshwa hela anatatua shida yake.

Leo hii watu tuliokuwa tunaonekana maskini wasiokuwa na hata sh. 10, kwa nguvu za Serikali tunamiliki sh. milioni 9,” anasema Gudawa.

Aansema kupitia biashara ndogo ndgo walizokuwa wakifanya, kila wiki mwanachama anatakiwa kujiwekea akiba ya sh. 10,000.

Gudawa, anasema waliendelea na utaratibu huo huo, huku yule aliyekuwa akihitaji kukopa, anakopeshwa na wakati wa kurejesha, analipa riba kidogo.

“Mwanakikundi akikopa sh. 10,000 anarejesha sh. 11,000,”anasema Gudawa na kwamba waliendelea na utaratibu huo hadi wakafikisha sh. milioni 9.

Kwa mujibu Gudawa wametoa sh. milioni 6 kwenye sh. milioni 9 na kugawana ambapo kila mmoja amepata sh. 400,000 na baada ya kila mmoja kupata mgao wake, wapo wana kikundi ambao wamekodi mashamba yenye ukubwa wa ekari mbili na kununua mbolea wakijiandaa kwa kilimo cha pamba, na wengine wameongeza mtaji kwenye biashara zao, wakati huo huo wakiendelea kujiwekea akiba, kwani baada ya kutoa sh. milioni sita walibakiza akiba ya sh. milioni 3.

“Wengine tuna wanafunzi, kwa hiyo fedha zimetusaidia kulipa ada na matumizi mengine ya nyumbani,” alisema Gudawa. Lakini pia anasema miradi ambayo wanaendesha inawasaidia kujikimu ambo mbalimbali, kwani hakuna mwana kikundi anayeweza kusema mtoto ameshindwa kwenda shule kwa kukosa mahitaji ya shule au kwenda kutibiwa.

“Akikwama anakuja kwenye kikundi tunampa hela zipo,” alisema kwa kujiamini.
Aidha, wanufaika hao wameshauriwa walengwa wa mpango huo, kutumia ruzuku kujiletea maendeleo kama ambavyo wengi wamefanya.

Ushauri huo umetolewa na mnufaika wa TASAF Mkazi wa Kijiji Ipililo, Kata ya Ipililo, Halmashauri ya Wilaya Maswa, mkoani Simiyu, Esther Hoja Dome (49) alipokuwa akieleza mafanikio aliyopata tangu alipojiunga na TASAF.

Anasema japo watu wanaopewa ruzuku ya TASAF na kulalamika kuwa ni ndogo, lakini yeye alipoanza kulipwa ruzuku hiyo aliidunduliza baadaye kununua mbuzi wawili, akaanza ufugaji.

Kwa mujibu wa Esther, mbuzi hao wanazaliana anauza, ambapo mbuzi mmoja mkubwa anamuuza sh. 150,000 na alijikuta amepata mtaji na kuanzisha biashara ya kuuza vitenge.

Mbali na kuuza mbuzi na kupata mtaji wa vitenge sh. 200,000, alioanza nao, leo mtaji umeongezeka na kufikia sh. 500,000. Aidha, anasema mbuzi nao wameendelea kuzaliana, ambapo wamefikia 11 kutoka wawili, achilia mbali aliokwisha uza.

Kuhusu biashara yake ya vitenge, anasema kila kimoja anakiuza sh. 15,000, hivyo anapata faifa ya sh. 5,000. Anasema wakati anaingizwa kwenye TASAF mwaka 2015, maisha yake yalikuwa duni, lakini hizo fedha ambazo wenzake wanasema ni ndogo, zimemwezesha kuanzisha miradi.

“Ruzuku ya TASAF imenisaidia sana, nilikuwa naangaika kusomesha watoto, ilikuwa vigumu kupata hela,”anasema Esther na kuongeza;

“Nilikuwa nalima vibarua na watoto wangu, tulikuwa tukiishi maisha magumu, hata uhakika wa mlo moja tulikuwa hatuna.” Hata hivyo, mradi wake wa ufugaji mbuzi na biashara ya kuuza vitenge inamsaidia kupata fedha za kuhudumia watoto na kuhakikisha wanapata elimu.

“Nikikosa matumizi, nauza mbuzi mmoja maisha yanaendelea. Lakini wakati mwingine nikipata ruzuku ya TASAF nanunua mbegu, nakodi mashamba nalima,” anasema na kuongeza;

“Fedha ninazopata kupitia kwenye mradi wangu wa mbuzi zinanisaidi kusomesha watoto, ninasomesha watoto saba ambapo watatu wapo Shule ya Sekondari Ipililo na Shule ya Msingi Ipililo wapo wanne,” anasema Esther na kuongeza;

“Nina uwezo wa kuwanunulia nguo za shule, viatu, daftari na mahitaji mengine bila wasiwasi…wanavaa vizuri na maisha yanaendelea.”

Aidha, anasema kabla ya kunufaika na TASAF, watoto wake walikuwa wanalala chini, lakini kwa sasa amewanunua godoro la sh. 130,000 wanalala pazuri.

Kwa mujibu wa Esther, sasa hivi amenunua bati saba na amefyatua tofali za block 850 ikiwa ni maandalizi ya ujenzi wa nyumba ya kisasa.

“Nilipopata hela nilianza kujiuliza hii hela nikiila sinitapata hasara, nikaona nijitaidi kidogo kidogo ili niwe na nyumba nzuri kama wenzagu, niondoke kwenye umasikini, kwa sababu TASAF imekuja kutunusuru na umaskini na sisi tupate maendeleo,” anasema Esther ambaye malengo yake ni kujenga nyumba ya vyumba vitatu.

“Kwa kweli TASAF imenisaidia maisha yangu yanaenda vizuri, ikilinganishwa na huko nyuma ambako nilikuwa siwezi hata kusomesha watoto,” anasema Esther.

Mbali na shughuli anazozifanya, Esther anasema mwaka jana wameanzisha kikundi kinachoundwa na wanawake wanufaika wa TASAF cha kuweka akiba, ambapo waligawana sh. 1,600,000.

Anasema walipogawana fedha hizo wamekodisha mashamba, wamenunua mbegu na wamekodi trekta kwa ajili ya kuwalimia. “Tumepata mahindi ambayo mengine tumeuza na mengine kuweka ndani kama akiba ya chakula,” anasema na kuongeza kwamba hayo ni matokeo ya TASAF.

Aidha, anasema nyumbani kwake amechimba kisima cha maji kwa gharama ya sh. 360,000 sasa hivi maji anachota nyumbani.

Kwa maendeleo aliyopata, Esther anawashauri wanufaika wa TASAF wanapopewa ruzuku waanzishe miradi midogo midogo itakayowawezesha kuzungusha hizo hela, badala ya kubaki kulalamika.

Anasema kutokana ma alivyonufaika na mpango wa TASAF, anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwani ameweza kupata maendeleo kupitia mpango huo.

“Namuomba mpango huu uendelee kutuvuta, kwani nyuma yangu wapo wengi ambao maisha yao yamebadilika hawaishi wakiangaika kama huko nyuma,” anasema Esther.

Mnufaika mwingine, anasema; “Naishukuru sana TASAF kwa kunitoa kwenye umaskini, watu waliniita Njile (mpitaji) lakini leo wananishangaa, wanasema Njile amekuwa mtu kweli.

Wanasema nimekuwa mtu kweli baada ya kuona mafanikio makubwa niliyoyapata tangu nilipojiunga TASAF.

Kwa kweli nilikuwa na maisha duni sana, kila mmoja alidhani na mimi nitakufa wakati wowote kwa njaa, aliamini nitamfuata mama yangu ambaye alifariki nikiwa na miezi miwili.”

Hiyo ni kauli ya Njile Madahu Makubi (60) mkazi wa Kijiji cha Ipililo, Kata ya Ipililo Halmashauri ya Wilaya Maswa, mkoani Simiyu, aliyoitoa wakati akieleza maisha yake yalivyokuwa huko nyuma na mafanikio aliyopata baada ya kujiunga kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF.

Anasema sababu ya kuitwa jina la Njile na wananchi ni kwa sababu alikuwa maskini sana, hakuwa na uhakika hata wakupata mlo mmoja.

“Kwa kweli nilikuwa masikini sana. Niliambiwa mama alifariki nikiwa na miezi miwili, mimi simjui. wanakijiji waliamini nitakufa kwa njaa, sikuwa na msaada wowote,” anasema Njile.

Anasema mbali ya kutokuwa na uhakika wa chakula, hata sehemu ya kulala alikuwa hana. “Nilikuwa nalala nje mvua ilipokuwa ikinyesha, inaninyeshea mimi, nilikuwa nalala kwenye kachumba kamoja, kalikoezekwa kwa turubai,” anaeleza Njile.

Njile anasema akiwa amekata tamaa ya maisha, huku kila mtu akiamini kwamba Njile hawezi kuwa mtu, ndipo mwaka 2015 alipoamdikishwa TASAF na kuanza kupata ruzuku.

Anasema alipopewa ruzuku ya kwanza kutoka TASAF, hakutaka kuitumia fedha hiyo kwa mambo mengine, bali walianzisha Kikundi cha Wanawake Kujiinua.

Kwa mujibu wa Njile kikundi hicho kinaundwa na wanawake 10 wanufaika wa TASAF. Anasema walianza kujiwekea akiba na alipokuwa akipata ruzuku ya TASAF, alinunua mbegu na mbolea na kuendesha kilimo cha mahindi na mbaazi.

Kwa upande mahindi anasema analima shamba lenye ukubwa wa ekari mbili, ambapo hupata gunia 16 wakati wa mavuno. Anaongeza kwamba anapouza mahindi, fedha hizo amekuwa pia akijiwekea akiba kwenye kikundi chao ambapo wanakutana mara moja kwa mwezi.

“Niliendelea hivyo hivyo kwa kujinyima, huku nikiishi maisha magumu,” anasema. Baada ya hapo anasema kwenye kikundi, walikubaliana kila mmoja awe na mradi wa kufuga ng’ombe, hivyo fedha walizokopeshana kila mwana kikundi alinunuliwa ng’ombe ndama.

“Tulinunua ng’ombe kwa sababu kwenye kikundi chetu hatupeani fedha mkononi, unasema unachotaka kufanya wanaenda kukununulia, na mimi kwa sababu ndiye mwenyekiti wa kikundi nalisimamia hilo, tunakataa mtu akichukua fedha sio anaenda nyumbani kuzila,” anasema Njile na kuongeza;

“Tunafanya hivyo ili kujiinua kama TASAF ilivyokusudia.” Kwa mujibu wa Njile baadaye alikopa fedha kwenye kikundi sh. 200,000.

Anazidi kueleza kuwa baada ya kupata mkopo wa sh. 200,000 kutoka kwenye kikundi na yeye aliuza ng’ombe wake wawili madume kwa sh. 1,500, 000.

Anasema nyumbani kwake alikuwa na akiba ya sh. 300,000, hivyo akawa na jumla ya sh, milioni 1,800,000.

Lakini pia, anasema kwenye kikundi chao wana mradi ambao unawasaidia kuwaingizia kipato.

Anasema wana mradi wa viti 200, sahani 200 na vikombe 200, ambavyo wanavikodisha kwa watu wanaokuwa na sherehe au misiba. Kwa mujibu wa Bi. Njile, kiti kimoja wananakikodisha kwa sh. 300, kikombe sh. 200 na sahani sh. 200.

“Kwa kweli tuna wateja wengi, na hivi sasa ninavyozungumza viti, sahani na vikombe vimekodishwa kwenye harusi,” anasema na kuongeza’

“Mwisho wa mwezi tunagawana fedha hizo na kila mmoja anaenda kufanya kile alichokusudia.”

Kwa hiyo anasema baada ya kuwa na sh. 1,800,000 na alipopata fedha zile wanazogawana kila mwezi kwenye kikundi kutoka kwenye mradi wao, ndipo alipoanza ujenzi.

“Njia hiyo ndiyo imenifanya nijenge nyumba inayowafanya watu washangae, wanaona maajabu ambayo hayakutarajiwa yafanywe na Njile (mpitaji),” anasema.

Anasema amejenga nyumba yake kwa kutumi bati 64 kila bati moja alikuwa akilinunua sh. 16,000 sawa na sh. 1,024,000 na ametumia tofali za kuchoma 2,000.

Anasema kwa miradi yake anayoiendesha na kwa jinsi kwenye kikundi chao walivyoanzisha utaratibu wa kujiwekea akiba na kukopeshana, pamoja na kuwa na mradi ndani ya kikundi ikiwemo wa kufuga ng’ombe, hata leo hii wakisema TASAF haipo, yeye ataendelea kusimama imara.

“Kwa jinsi nilivyojiunga kwenye kikundi naweza kuendelea kusimama imara, lakini naomba TASAF iendelee ili watu wengine wenye maisha duni waendele kunufaika,” anasema Njile.

Njile anasema akibahatika akakutana na Rais Samia, nitamshukuru sana kwa kuwawesha kupitia TASAF. “Tulikuwa maskini sana, tulikuwa tunachekwa, kwa sababu mimi isingekuwa TASAF pengine ningeshakufa,” anasema Njile.

Kwa upande wao wanakikundi cha cha Mwanzo Mgumu, ambacho kinaundwa na wanawake 15 wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), wamesema ruzuku ambayo yamepewa na mfuko huo imewawezesha kuanzisha miradi iliyosaidia kuondoa kwenye orodha ya watu maskini.

Kikundi hicho ambacho kipo katika Kijiji Nyashimba S, Kata Badi Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, kwa sasa kinaendesha miradi, ambayo inakiwezesha kuwa na uhakika wa kipato,ikilingashwa na kipindi cha nyuma.

Hatua hiyo imewezesha wana kikundi wote kujenga nyumba za bati, lakini wakati wanajiunga na TASAF wote walikuwa wakiishi kwenye nyumba za tembe.

Mwenyekiti wa Kikundi, Kwimba Nzaya Jibata (40) ameanika mafanikio ya kikundi hicho wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hali waliyokuwa nayo kabla ya kuingizwa kwenye mpango wa TASAF na hali ya sasa.

Mbali na wote kuwa wamejenga nyumba za bati, Jibata anasema kikundi hicho kinafuga kondoo 93 na ng’ombe dume mmoja.

Aidha, anasema wana mradi ya kilimo, ambapo kwa mwaka huu wamelima heka mbili za alzeti na kupata mavuno gunia tisa. Aidha, anasema wamelima mpunga heka moja na wamevuna gunia nane.

Mbali na kilimo, anasema kupitia kikundi chao wanawekeza hisa, ambapo kila wiki mwanakikundi anatakiwa kununua hisa za kuanzia sh. 2,000 na kuendelea kulingana na uwezo wake.

Aidha, anasema nje ya kikundi, kila mnufaika wa TASAF ana mradi wake binafsi ikiwemo kufanya biashara za kuuza genge, kulima bustani na nyingine ambazo zinawawezesha kupata fedha za kujikimu ndani ya familia zao pamoja na zile za kununua hisa.

Anasema hadi Septemba, 2023 kikundi kina sh. 800,000 mbali na zile ambazo wanakikundi wamekopeshwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha hadi hatua ambayo tumefikia. Zamani tulikuwa hatuna uwezo hata wa kusomesha watoto.

Tulikuwa na hali ngumu. Tulikuwa na hali ya umaskini uliokithiri kwenye kila mji, lakini baada ya TASAF tumepata mafanikio na sasa hatumo tena kwenye orodha ya kaya maskini, tunafuga, tunalima, tunawekeza hisa na kila mmoja anafanya biashara ndogo ndogo na ufugaji nje ya kikundi.

Tuna uwezo wa kusomesha watoto wetu. Hata watoto wakiugua, wanatibiwa. Wengine wanalima mchicha, nyanya, wengine wana biashara za kutembeza, tunapata fedha za kuhudumia familia.”

Kwa mujibu wa Jibata, kama kusingekuwa na TASAF maisha yao yangekuwa magumu kabisa.

Naye Katibu wa Kikundi hicho, Janeth Mashala Ntemi (38) anasema kupitia ruzuku ya TASAF aliyoitumia kuanzisha kilimo cha bustani na ufugaji pamoja kwa kujiunga kikundi, ameweza kusomesha watoto wake sekondari na wengine wanaendelea na shule ya msingi.

Anasema mtoto wake mmoja anasoma kidato cha kwanza mkoani Songea, wawili wapo kidato cha pili. Aidha, anasema mtoto wake mwingine anasoma kidato cha tano mkoani Mara na kwamba wote wanapata mahitaji yao ya shule bila wasiwasi kupitia nguvu za TASAF.

Kwa upande wake, Magreth Sala Chales (51) anasema TASAF imemwezesha kusomesha watoto wake sita, ambapo mmoja yupo chuo cha ualimu na wengine wanaendelea na sekondari na shule ya msingi.

Naye Rahabu Nuru Maligisa (50) anaipongeza TASAF kwa kumwezesha kusomesha watoto, kwani kabla ya hapo walikuwa hawawezi kwenda shule.

Kwa upande mwingine biashara za genge inayoendeshwa na Bw. Martin Runju Kisenje (69) na Agnes Lucas Gihelya (34) imewezesha wakazi hao wa kijiji Mhija, Kata ya Badi, Halmashauri ya Maswa, mkoai Simuyu kuwa na uhakika wa kujiingizia kipato tofauti na kipindi cha nyuma.

Wananchi hao wameweza kuanzisha biashara za genge baada ya kupata ruzuku kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Mmoja wa wakazi hao, Kisenje anasema ruzuku ya TASAF imemwezesha kupata mtaji wa biashara ya genge, ambapo anauza nyanya na vitunguu, hivyo inamsaidia kupata fedha ya kujikimu.

Anasema faida anayoipata kupitia kwenye biashara hiyo na anaitumia kununua mahitaji yake na kiasi kingine cha fedha ananunulia mbegu, mbolea kwa ajili ya kilimo ya cha pamba, vitunguu na nyanya.

Anasema fedha anazopata zinamsaidia kununua nguo, chakula na mahitaji mengine ya nyumbani ikiwemo kusomesha watoto.

“Kabla ya TASAF nilikuwa na maisha magumu magumu, sikuwa na biashara ya genge, wala nilikuwa sijishughulishi na kilimo. TASAF imenipa mtaji.

Mtaji huo umeniwezesha kufanya biashara, nimenunua bati na kujenga nyumba,” anasema na kutoa wito kwa wanufaika wa TASAF kutumia vizuri hela hizo, kwani zitawasaidia.

Kutokana na mafanikio aliyopata anamshauri Rais Samia Suluhu Hassan, akimshauri azidi kusimamia mfuko huo ili uzidi kuwanufaisha.”

Kwa upande wake, Agnes, anasema baada ya kuanzisha biashara ya genge kupitia fedha za TASAF, amekuwa na uhakika wa kusomesha watoto, kuwanunulia sare, daftari na ana uhakika wa chakula nyumbani kwake. Aidha, anasema akipewa ruzuku anaipeleka kwenye kilimo.

Anasema alianza biashara yake ya genge kwa mtaji wa sh. 15,000, lakini sasa hivi umeongezeka hadi sh. 35,000, hivyo kiasi cha faida anachopata kutoka kwenye biashara hiyo angalau inamaidia kupata kipato cha kujikimu, kuliko huko nyuma, ambapo hakuwa na kitu.

Kwa sasa anasema anauza nyanya, vitunguu, dagaa na samaki na ana mpango wa kupanua biashara yake pindi akipata ruzuku ya TASAF na mkopo kutoka kwenye kikundi chake cha Tuleane.

Anasema kwenye kikundi hicho, wapo wanachama 32, ambao wanakutana mara moja kwa wiki na kila mwanachama anatakiwa kununua hisa kuanzia sh. 5,000 na kuendelea.

“Nikikopa ninaongeza mtaji wangu, mara ya mwisho nilikopa sh. 10,000, naomba TASAF iendelee kutuwezesha ili mtaji wangu uzidi kuongezeka,” anasema Agnes.

Anatoa wito kwa wanufaika wa TASAF waendelee kutumia vizuri ruzuku wanayopewa, ili iendelee kuwasaidia watu wengi zaidi.