January 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka 63 ya Uhuru na rekodi treni ya SGR

Na Mwandishi Wetu

LEO Tanzania inaadhimisha miaka 63 ya Uhuru ambao ulipatikana tarehe kama ya leo mwaka 1961.

Siku hii ni muhimu katika historia ya nchi yetu, ambapo ni fursa muhimu ya kila Mtanzania kutafakari tulipotoka, tulipo na twendako.

Mambo hayo ni muhimu kuyatafakari kwa sababu ndiyo nafasi pekee ya kuweza kupima matunda yaliyotokana na nchi yetu kudai Uhuru chini ya uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alifariki Oktoba 14, 1999.

Swali la kujiuliza leo, hivi Mwalimu Nyerere akifufuka anaweza kujutia jitihada zake za kuongoza Watanzania wakati huo kudai Uhuru kutoka mikononi wa Mkoloni.

Bila shaka jibu lake litakuwa hapana. Mwalimu atashuhudia mambo mengi ambayo yamefanyika ndani ya nchi yetu. Miongoni mwa mambo ambayo yatamfanya akune kichwa na kuamini kuwa Tanzania aliiacha kwenye mikono salama kujengwa kwa miundombinu ya Usafiri wa Treni ya Umeme (SGR) ambayo sasa imeanza kutoa huduma.

Wakati Hayati Nyerere anang’atuka madarakani kwenye mipango na mikakati yake ya muda mrefu, kati ya mambo ambayo sikuwa kuona kwenye maono yake ilikuwa ni ujenzi SGR.

Lakini chini ya uongozi shupavu wa Rais Samia Suluhu Hassan, leo hii Tanzania inashudia Watanzania wanaanza kutumia usafiri wa treni ya umeme, ambao wengi walikuwa wanausikia kwa wenzetu wa nchi za Ulaya.

Ukibahatika kusafiri na treni hiyo kauli kama vile; Tulichelewa sana.” Ndizo lugha zinazoongelewa. Kwa nini wanaongea lugha hizo, kikubwa ni kutokana na muda wa safari wanaoutumia kwenye safari zao kutoka Dar es Salaam-Morogoro hadi Dodoma.

Kwa sasa muda wa safari kati ya Dar es Salaam-Morogoro ni kati ya saa 1: 30 hadi saa 1: 40 huku kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma muda wa safari ukiwa ni saa 4.

Lakini kwenye treni maarufu kama mchongoko muda wa safari unaelezwa kuwa ni saa 4 kutokaDar es Salaam-Dodoma. “Hapo swali linapokuwa wale wanaosema tulichelewa wanakosea?”

Jibu la swali hilo lipo wazi, ni kwamba hawajakosea na hayo yamewezekana na historia kuandika chini ya uongoziwa Rais Samia.
Kuanza kwa usafiri wa treni ya SGR mwaka huu ambao Tanzania inaadhimisha miaka 63 ya Uhuru itabaki kumbukumbu isiyofutika kwa Rais Samia kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Rais Samia alizindua usafiri huo Agosti 1, 2024 kutoka Dar es Salaam – Morogoro hadi Dodoma, katika eneo la Stesheni jijini Dar es Salaam.

Viongozi mbalimbali walishiriki na kushuhudia uzinduzi huo ikiwemo kusafiri na Rais Samia kutoka Dar es Salaam- Morogoro hadi Dodoma.

Aidha, Rais Samia alizindua majengo ya Stesheni za Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma achilia miundomboni ya reli kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 722.

Uzinduzi huo ulihitimishwa na hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika Stesheni ya SGR ya Dodoma. Pamoja na mambo mengine, Rais Samia alipongeza mchango wa marais wastaafu katika kufanikisha mradi huo utakaoleta mageuzi ya kiuchumi.

Alisisitiza kwamba kukamilika kwa vipande vya reli kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ni utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa inayolenga kujenga Tanzania yenye uchumi jumuishi.

Kwa hiyo, Rais Dkt. Samia aliiagiza Wizara ya Uchukuzi, Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Shirika la Reli (TRC) kuhakikisha vipande vya reli ya kisasa vinavyoendelea kujengwa kwenda Mwanza na Kigoma vinakamilika kwa wakati na kwa viwango vya ubora uliokubaliwa.

Alisema lengo ni kufanya reli isomane kibiashara na bandari za bahari na Maziwa Makuu na kufungamanisha bandari na usafiri wa anga kwa kuingiza reli katika Terminal 3 ya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.

Kwa msingi huo aliitaka Wizara hiyo kuhakikisha ujenzi na ukarabati wa meli za kubeba mizigo unaoendelea kwenye maziwa mbalimbali unakamilika kabla ujenzi wa mradi huo haujaisha.

***Manufaa ya mradi

Akielezea manufaa ya mradi huu wa kimkakati, Rais Dkt. Samia alisema reli hiyo itaongeza ufanisi wa bandari nchini hususan bandari ya Dar es Salaam kwa kuondosha mizigo kwa haraka zaidi kutokana na uwezo wake wa kuhudumia shehena ya tani milioni 17 kwa mwaka.

Rais Dkt. Samia aliongeza kuwa mradi huu utachochea shughuli za kiuchumi, hususan katika sekta za viwanda, kilimo, ufugaji, utalii na biashara na hivyo kukuza sekta ya viwanda katika maeneo mengine ya nchi kutokana na uhakika wa usafiri na usafirishaji.

“Hivyo, Reli hii itaongeza biashara hapa nchini pamoja na nchi za jirani hususan zile zisizo na bandari pamoja na kikanda. Reli hii pia itaimarisha biashara kati ya nchi yetu na nchi zinazohudumiwa na Ushoroba wa Kati (Central Corridor), zikiwemo Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Uganda na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi,” alisema Rais Samia.

Pia alisema Mradi huu pia utapunguza msongamano wa magari barabarani na ajali, kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa vifurushi na kupunguza uharibifu wa mazingira kwa kutumia reli hiyo inayotumia nishati ya umeme.

***Awapa mbinu wamiliki wa mabasi

Rais Samia, alisema kutokana na kuongezeka kwa mwamko wa abiria kutumia treni ya, aliwataka wamiliki wa mabasi nchini kuja na na mikakati mipya kuhakikisha wanaendelea kuwa sokoni bila biashara zao kuathirika.

***Uhalisia wa alichosema Rais Samia

Kauli hiyo ya Rais Samia ilikuja, kwani tangu kuanza kwa usafiri huo, wamiliki wa mabasi wamekuwa wakilalamikia changamoto katika soko na tayari wengine wameanzisha safari mpya katika njia zisizo na reli ya kisasa.

Kwa kuthibitisha hilo, ushahidi upo wazi kwani kampuni kama Kimbinyiko, BM Coach, Abood na Shabiby tayari zimeanza kupanua huduma katika maeneo mapya, ikiwemo Sumbawanga, Bukoba, Musoma na hata nchi jirani ya Kenya.

Hatua hizi zinalenga kurejesha sehemu ya soko na kudumisha shughuli zao za usafirishaji, licha ya mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri.

SGR imevutia wananchi zaidi, ikiwa na zaidi ya abiria 7,000 wanaosafiri kwa siku kati ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma. Ufanisi na mvuto wa mtandao huo wa reli umesababisha kupungua kwa abiria wanaotumia usafiri wa mabasi kwa njia ya barabara.

Hiyo inadhihirishwa na jinsi wananchi wanavyochangamkia tiketi sa kusafiri na treni ya SGR,kwani kwa sasa ni vigumu abiria anayetaka tiketi kusafiri na treni leo kuweza kuikata na kuipata.

Baadhi ya wamiliki wa mabasi wanasema, licha ya treni kuchukua soko katika njia zilizozozoeleka, haitakuwa shida kwao kwa kuwa Tanzania ni kubwa.

Tanzania ina eneo la kilomita za mraba 945,087 ikiwa ni kubwa zaidi kuliko Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda kwa pamoja. Eneo la nchi hizo nne lina ukubwa wa kilomita za mraba 877,852, huku Kenya na Uganda zikichukua sehemu kubwa zaidi ya kilomita za mraba 582,646 na 241,038, mtawalia.

Kuwepo kwa mipaka na nchi saba, ambapo nchi mbili kati ya hizo hazina bahari na zinategemea Bandari za Tanzania kwa biashara za kimataifa, kunatoa fursa kwa wamiliki wa mabasi kutumia fursa hiyo

*** Rais Samia aliliona hili

Akizindua treni ya SGR, Rais Samia alisema licha ya athari zilizoanza kujitokeza kwa wamiliki wa mabasi na malori, bado Tanzania ina fursa nyingi za wasafirishaji hao kunufaika.

Rais Samia alisema bado wasafirishaji hao wana fursa ya kunufaika, hasa katika njia nyingine ambazo mradi huo haujafika. Hata hivyo, alisema kupungua kwa mabasi barabarani inaweza kuwa athari mbaya kwa wafanyabiashara, lakini nzuri kwa Serikali kwa kuwa itapunguza ajali.

“Hasara moja ambayo imeanza kuonekana ni kupungua kwa mabasi barabarani, kwa wafanyabiashara ni mbaya ,lakini kwa nchi ni nzuri kwa sababu inapunguza ajali pia na sasa usafiri barabarani unadhibitiwa vizuri,” alisema.

Alieleza kwamba bado wasafirishaji hao hawataathirika kwa kuwa kuna njia nyingine ambazo, treni hiyo haijafika na hivyo wana nafasi ya kupeleka mabasi huko.

***Mkakati wa wenye mabasi

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Kimbinyiko, Ferdinand Mabumo, alinukuliwa hivi karibuni akisema tayari kampuni yake ilishaanzisha njia nne mpya, ili kuendana na soko linalobadilika.

“Tumepunguza safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma kutoka safari 10 hadi nne kwa siku,” alisema. Njia mpya sasa ni Dodoma-Arusha, Arusha-Mbeya, Dodoma-Njombe na Moshi- Mbeya. Mipango ya baadaye ya kampuni ni kupanua huduma hadi Nairobi, nchini Kenya.” alisema.

Naye Meneja wa Kampuni ya Mabasi ya Shabiby, Edward Magawa, alinukuliwa akisema ni umuhimu kupanua maeneo ya huduma ili kukabiliana na mabadiliko yaliyosababishwa na SGR.

“Tanzania ni kubwa ingawa bado kuna mahitaji ya safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma, tumejikita katika njia mpya kama vile Dodoma- Sumbawanga, Dodoma-Bukoba na Dodoma-Musoma,” alisema.

“Kwa sasa tupo kwenye majaribio na tuna mipango ya kupanua hadi Kampala (Uganga) na Rwanda,” alinukuliwa Meneja wa Operesheni wa BM Coach, Gabriel Makundi, wakati akizungumza na chombo kimoja cha habari (sio Majira).

Alisema kampuni hiyo itaendesha safari nne kwa siku kwenye njia hiyo na inafikiria kuongeza njia ya Dar es Salaam-Tunduma hivi karibuni.

Kabla ya kuanza kwa SGR, BM Coach ilikuwa ikiendesha hadi mabasi 22 kwa siku kwenye njia ya Dar es Salaam-Morogoro na mabasi 10 kati ya Dar es Salaam na Dodoma.

Hata hivyo, kutokana na kuongezeka kwa usafiri wa reli, sasa ni mabasi sita tu yanayofanya safari kati ya Dar es Salaam na Morogoro na manne kati ya Dar es Salaam na Dodoma.

Licha ya changamoto zinazotokana na SGR, wamiliki wa mabasi nchini wanatumia uwezo wao wa kubadilika na kupanua njia zao, ili kuhakikisha wanaendelea kuwa sehemu muhimu ya mtandao wa usafiri nchini.

***Kilio kuhamia kwa wenye malori

Kilio kinachowakumba abiria kutokana na abiria wengi kuhamia kwenye usafiri wa treni ya SGR kinatarajia kuhamia kwa wenye malori hivi karibuni.

Hiyo ni kwa sababu TRC inatarajia kupokea mabehewa 264 kwa ajili ya mizigo katika ya (SGR katikati ya mwezi huu.

Taarifa iliyotolewa Novemba 15, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa shirika hilo, Fredy Mwanjala, ilieleza kwamba; “Shirika la Reli Tanzania TRC linautaarifu umma kuwa utengenezaji wa mabehewa 264 ya mizigo yatakayotumika katika reli ya kiwango cha kimataifa SGR umekamilika nchini China.

Meli iliyobeba mabehewa hayo imeng’oa nanga China Novemba 12, 2024 na inatarajiwa kufika Tanzania katikati ya Desemba 2024,” imesema taarifa hiyo.

Mwanjala aliongeza kuwa; “Katika mzigo huo kuna mabehewa 200 ya kubeba makasha (makontena) na 64 ya kubeba mizigo isiyofungwa (loose cargo).

“Shehena hiyo ya mabehewa 264 ni sehemu ya jumla ya mabehewa 1,430 ambayo kwa mujibu wa mkataba yanatakiwa kutengenezwa na kampuni ya CRRC.

Katika kipindi hiki ambacho mabehewa hayo hayajafika, mizigo yenye uzito uliopitiliza hairuhusiwi katika treni hizo, abiria wa daraja la biashara anapaswa kuwa na mzigo usiozidi kilo 30, huku daraja la uchumi usizidi kilo 20.
*** Mafanikio ya SGR

Kilio cha wenye mabasi kutokana na ujio wa treni ya SGR unadhihirishwa na

Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhusu mapato na takwimu za abiria waliosafiri na treni hiyo tangu kuanzishwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC)

Akizungumza Novemba 14,2024 baada ya kutembelea shirika hilo, Mwenyekiti wa PIC, Augustino Vuma, alisema wameridhika na hali ya uendeshaji wa treni hiyo.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, akizungumza na waandishi wa habari wakati Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ilipotembelea TRC alisema;

“Mapato yatokanayo na abiria huwa ni asilimia ndogo lakini asilimia 80 na zaidi mara nyingi inatokana na usafirishaji wa mizigo, kama haya yaliyopatikana ni asilimia 20 tunaamini mizigo ikianza wafanyabiashara wengi watatumia fursa hiyo na mapato ya shirika yataongezeka,” amesema Vuma.

Kamati hiyo pia iliishauri shirika hilo liendelee kuweka teknolojia zaidi za ulinzi na kuwachukulia hatua kali watu wanaohujumu miundombinu ya reli hiyo..

Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, alisema watahakikisha wanamalizia vipande vilivyobaki ili shirika liendelee kunufaika kwa kubeba abiria na mizigo wapate faida kubwa kama nchi.

“Kamati imeridhika kwamba uwekezaji uliofanywa katika sekta hii una tija kubwa kwa taifa letu kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo, tutafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa ili shirika liendelee kunufaika,” alisema Kihenzile.

Alisema Serikali inajenga reli hiyo kutoka Dar es Salaam – Mwanza – Kigoma kilomita 2,300 na kwamba hadi sasa sh. trilioni 27 zimewekezwa kwenye mradi huo.

Kuanzia mwakani shirika hilo linatarajia kuanza kusafirisha mizigo kwenye reli hiyo hatua itakayowezesha mapato kuongezeka zaidi.