December 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka 60 ya JWTZ ndani ya mikono ya thabiti ya Amiri Jeshi Mkuu Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Dar

JUZI, SEPTEMBA 1, 2024 ilikuwa ni siku muhimu kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambapo lilitimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake ambayo ni sawa na miongo sita. Jeshi hilo, lilianzishwa Septemba mwaka wa 1964.

Kuanzishwa kwa jeshi hili, Ilichukua nafasi ya Jeshi la Tanganyika Rifles lililorithiwa na ukoloni wa Kiingereza. Chanzo cha jeshi nchini Tanzania kilikuwa jeshi la kikoloni la Uingereza katika Afrika ya Mashariki.

Mwaka 1919 Uingereza ilikabidhiwa utawala juu ya Tanganyika na Shirikisho la Mataifa. Baada ya Uhuru mwaka 1961 vikosi vya King’s African Rifles katika Tanganyika vilibadilishwa jina na kuwa Tangayika Rifles (TR).

Pamoja na kubadilika jina Tanganyika Rifles ilikuwa na muundo sawa na Kings African Rifles (KAR). Maafisa wenye mamlaka bado walikuwa Waingereza, pamoja na Waafrika watano waliopandishwa cheo wakati wa uhuru na kupokea mafunzo katika vyuo vya kijeshi vya Kiingereza.

Jeshi jipya lilipangwa katika vikosi viwili vyenye makao makuu huko Dar es Salaam na Tabora. Afisa mkuu alikuwa Brigedia Jenerali Patrick Sholto Douglas. Kwa jumla kulikuwa na hali ya kutoridhika kati ya askari wa TR.

Tangu kuanzishwa kwa JWTZ, mwaka 1964 jeshi hili limetimiza kikamilifu majumu yake kama Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na sio Jeshi la Uvamizi, kama ambavyo amesema Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Samia Suluhu Hassan, kwa katika Maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi hilo.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo Samia amesema kwa miaka 60 Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekuwa jeshi hodari katika utekelezaji wa majuku yake na limekuwa mstari wa mbele katika kutoa msaada wakati wa majanga, ambapo limeendelea kuwa jeshi la ulinzi na sio la uvamizi na halina mpango huo.

Akifunga Maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi hilo sherehe zilizofanyika katika Uwanja vya Uhuru, zilitanguliwa na maonesho ya kijeshi pamoja na zana za kivita.

Kiongozi huyo ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama bchini, alisema katika kipindi chote cha miaka 60 yote Jeshi hilo halijawahi kuvamia nchi yoyote na wala halina mpango huo.

“Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) halikujengwa katika misingi ya kuwa jeshi la uvamizi isipokuwa jeshi la wananchi, hivyo litaendelea kulinda amani na kuhimiza majirani kuhimiza amani katika nchi zao..

“Pamoja na amani iliyopo nchini, jeshi letu linaendelea kujiimarisha katika nyanja zote kuendana na misingi ya kuundwa kwake, dhamira yetu ni kujenga jeshi imara lililo tayari kwa hali zote wakati wowote,” alisema Rais Samia. .

Aidha, alisema JWTZ limeshiriki na kufanikisha harakati za kuleta ukombozi barani Afrika ikiwemo kuyafundisha majeshi ya vyama vya ukombozi lakini pia kuwa mstari wa mbele kwenye uwanja wa vita vya ukombozi katika nchi za Msumbiji, Angola, Zimbabwe, Namibia na Afrika Kusini ambapo leo hii nchi hizo ni uhuru.

“Baada ya ukombozi jeshi letu limeendelea kushiriki kikamilifu na kwa mafanikio makubwa kwenye operesheni mbalimbali za kulinda amani katika nchi mbalimbali ikiwemo Liberia, Sudan Darfur, Lebanon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Visiwa vya Comoro, Msumbiji na DRC,” alisema Rais Samia.

Alilisistiza kwamba kihistoria jeshi hilo halikujengwa katika misingi ya kuwa jeshi la uvamizi, bali jeshi la Wananchi na la ukombozi, hivyo litaendelea kulinda amani ya nchi na kuhimiza nchi majirani kudumisha amani kwenye nchi zao.

Kwa mujibu wa Rais Samia pamoja na amani iliyopo nchini, Jeshi linaendelea kujiimarisha katika nyanja zote kwendana na misingi ya kuundwa kwake, dhamira yao ni kujenga Jeshi imara ambalo lipo tayari kwa hali zote na wakati wowote.

”Mimi binafsi kama Amri Jeshi Mkuu kila ninapotembelea au kushiriki shughuli za Jeshi letu, nashuhudia utayari, uhodari na umahiri, lakini ujasiri wa Jeshi hili, naridhika kuwa Jeshi letu lipo katika kiwango cha juu na kunipata matumaini makubwa kwamba kesho ya nchi yetu na watoto wetu ipo salama,” alisema Rais Samia.

Alisisitiza kwamba Jeshi hilo litaendelea kuwa jeshi la kisasa lenye dhana na nyenzo la kisasa, hivyo waendelee kufanyakazi wakijua Amiri Jeshi Muu yupo nao wakati wote.

“Tunaimarisha Jeshi liende na mabadiliko ya kiteknolojia ya vifaa na dhana, mikakati na mbinu za medani ili kuwezesha kutimiza wajibu wake ipasavyo,” alisema Rais Samia. Alisema Jeshi la Tanzania limekuwa ni la ukombozi na kioo katika harakati za ukombozi wa Afrika na kulinda amani Duniani.

”Katika ibara ya 28 kifungu kidogo cha kwanza cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasema kila raia anawajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha Uhuru, mamlaka ardhi na umoja wa kitaifa, hivyo katika mafanikio ya Jeshi letu, wananchi wa Tanzania wana mchango wao,” alisema Rais Samia na kuongeza;

”Sote tunakumbuka wakati wa Vita ya Kagera namna wananchi walivyojitolea kwa hali na mali kuliunga mkono Jeshi letu, kwani wananchi wamekuwa msingi wa ulinzi wa amani wa nchi yetu na umoja wetu ndani ya taifa.”

Rais Samia alisema kupitia kilele cha maadhimisho hayo anawasihi wananchi wa Tanzania kuendelee kutimiza wajibu wao wa Kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 28 kifungu kidogo cha kwanza kulinda amani ya nchi, huku wakiwakataa na kukemea wanaochochea uhasama na uvunjifu wa amani ndani ya nchi.

”Katika Kipindi cha miaka 60 Jeshi limekuwa ni kimbilio la wananchi na kuwa mstari wa mbele kutoa misaada ya huduma pale wananchi wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo majanga ya asili au ajali.

”Wananchi wanakumbuka mchango wa jeshi katika uokozi nchi ilipopatwa na mafuriko ya Kilosa na Ulanga mwaka 1970, ajali za kuzama Meli Mv Bukoba na Meli ya Mv Spice Bahari ya Zanzibar mwaka 2011 na hivi karibuni mwaka 2024, Janga la maporomoko ya udongo Hanang’a pamoja na kutoa huduma hizi ndani ya nchi pia jeshi limetoa huduma hizi nchini Malawi mwaka 2023 walipopatwa na majanga ya maporomoko kama yalitupata Tanzania,”alisema alisema

Alisema Jeshi limekuwa kinara katika kutafsiri dira,sera na mipango ya Serikali katika awamu zote za uongozi ambapo kwa awamu ya kwanza ya uongozi tTaifa la Tanzania lilitangaza vita kuwa ni maadui watatu, yaani Ujinga,Maladhi na Umaskini, ambapo katika kupambana na adui ujinga Jeshi lilianzisha shule kadhaa katika ngazi tofauti, kuelimisha watu, katika adui maladhi napo wanatoa huduma za afya na ni huduma za kutegemewa, huku kwa upande wa adui umasikini Jeshi kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linawapa vijana hali na stadi za kazi ili waweze kujiajiri na kupambana na umasikini wa kipato.

Rais Samia alisema hivi karibuni Jeshi limetekeleza kwa vitendo miito yote inayotolewa na Serikali ikiwemo katika kushiriki kwenye ujenzi wa IKulu mpya ya Chamwino Dodoma,Ujenzi wa ukuta wa Mererani wenye urefu wa kilomita 24.5 kama moja ya jitihada ya kulinda rasilimali madini inayovunwa katika eneo hilo.

Alisema katika kutekeleza kauli mbiu ya kazi iendelee, Jeshi linajitekeleza katika mageuzi yaendanayo katika mifumo ya ulinzi na uchumi duniani.

”Nchi yetu ina mkakati wa taifa wa kuimarisha uchumi na upatikanaji wa fedha za kigeni, malengo makuu ni kuimarisha uzalishaji wa mauzo ya bidhaa na huduma, kuzalisha bidhaa na huduma mbadala zinazoagizwa kutoka nje na kuimarisha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji binafsi ndani na nje ya nchi,”alisema.

Alisema kazi ya kuuwisha na kuimarisha viwanda vyake ili viweze kuzalisha baadhi ya mahitaji yake nchini na kunusuru matumizi ya fedha za kigeni.

Akizungumzia suala la nidhamu na utiifu, Rais Samia alisema katika Jeshi hilo ameshuhudia askari ambao wanaenda kinyume na misingi mikuu Jeshini wakichukuliwa hatua bila ya kuchelewa.

Rais Samia alisema utiifu wa Jeshi letu nchini,ndio unaojenga imani kwa Watanzania kulithamani na kuliamini na kuwa na matarajio makubwa ya jeshi lao. ”Niwasihi Makamanda na wapiganaji hakikisheni imani hiyo mnailinda kwa nguvu kubwa sana,”alisisitiza Rais Samia.

Rais Samia alifika Uwanja wa Uhuru asubuhi na kuzunguka uwanja wote akiwa kwenye gari maalumu kusalimia waliohudhuria.

Baada ya kuzunguka mkuu huyo wa nchi aliyekuwa amevalia gwanda la JWTZ, mizinga 21 isiyo na madhara ilipigwa ikisindikizwa na wimbo wa Taifa na beti mbili za wimbo wa Afrika Mashariki. Kisha, Rais Samia alikwenda kukagua gwaride katika vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama na wimbo wa Taifa ulipigwa tena.

Wimbo huo ulifuatiwa na gwaride la vikosi mbalimbali vya JWTZ na lililoonekana kuwavutia wengi zaidi ni lile la wanamaji kutokana na mavazi yake meupe. Kama ungekuwa nje ya uwanja huo, ungedhani ni kelele za wanaoshangilia mchezo wa mpira wa miguu, lakini shangwe hizo, ziliakisi furaha ya wahudhuriaji juu ya mwendo na matendo sambamba yaliyofanywa na wanagwaride.

Mistari ya vikosi vya ulinzi na usalama hivyo, ilipangwa mithili ya iliyonyooshwa kwa rula na haikuwa hivyo, kwa JWTZ pekee, hata mgambo walikuwa vema. Nakosa mnyama rahisi wa kumfananisha ukubwa sawia na mbwa walioshuhudiwa na kikosi cha mbwa cha JWTZ, ni wakubwa mithili ya simba jike aliyezaa mara kadhaa.

Gwaride lilipopita mbele ya jukwaa kuu, maaskari waliovalia kijeshi walipiga saluti akiwemo Amri Jeshi Mkuu huyo, Rais Samia.