December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka 57 ya Muungano,tumeshuhudia mafanikio makubwa ya kujivunia

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online

TAREHE 26 Aprili, 1964 Mataifa mawili haya ya Jamuhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar yalioungana na kuunda Taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo badae ikabadilishwa na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni dhahiri kuwa miaka 56 ya Muungano wetu imekuwa yenye kuleta maendeleo kwa Taifa katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa yanayonufaisha wanachi wa pande zote mbili za Muungano.

Kudumu kwa Muungano huu kumeleta mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na amani na utulivu uliopo nchini mwetu. Wananchi wanafanya shughuli zao za maendeleo kwa uhuru na utulivu sehemu yoyote ya Muungano. Vilevile, wananchi wa pande zote mbili za Muungano wameendelea kuwa na uhusiano na mshikamano wa karibu kadri siku zinavyoendelea.

Kadhalika, mwananchi yuko huru kuishi katika sehemu yoyote ya Muungano bila ya bughudha na wananchi wanashirikiana katika kazi za kuendesha maisha yao na kujenga Taifa.

Muungano huu umedumu kutokana na dhamira za dhati za umoja waliokuwanao waasisi wake, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Shekh Abeid Aman Karume sera sahihi za TANU na ASP na sasa CCM; jitihada zinazoendelezwa na viongozi waliofuatia baada ya waasisi pamoja na kuungwa mkono na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuthamini manufaa yake.

Zaidi ya yote utamaduni wa kukaa na kuzungumzia changamoto zinazojitokeza na kuzifanyia kazi imeongeza ufanisi katika kuufanikisha Muungano wetu.

Katika kipindi cha Miaka 57 ya Muungano, tumeshuhudia mafanikio makubwa ya kujivunia, Watanzania wamejenga umoja na misingi endelevu ya udugu baina yao, ikiwa ni uthibitisho kuwa Muungano unaendelea kuimarika.

Kwa kutumia misingi iliyowekwa,wananchi na viongozi wanahakikisha kwamba historia uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar vinaenziwa. Vilevile, pande mbili za Muungano zimejenga mifumo ya kuendesha Serikali zake kwa uwazi chini ya misingi ya demokrasia na utawala bora.

Misingi hiyo imeimarika kutokana na uelewa mzuri wa dhana ya uwajibikaji kwa viongozi wa ngazi zote.

Kipindi chote cha Muungano wetu,tumeshuhudia kuimarika kwa miundombinu ya barabara, usafiri wa anga, usafiri wa majini na kuimarika kwa huduma za jamii.

Aidha,tumeendelea kutumia maliasili zetu vizuri zaidi kwa manufaa ya wananchi wa pande mbili za Muungano. Mafanikio hayo yametokana na usikivu, utulivu, uzalendo, moyo wa kujituma na kujitolea na ushirikiano wa dhati wa viongozi na wananchi wote wa pande mbili za Muungano.

Tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuasisiwa mwaka 1964, Serikali zetu mbili zimeendelea na jitihada za makusudi za kuhakikisha kuwa masuala yanayoleta vikwazo katika Muungano yanashughulikiwa.

Aidha,Serikali zimeweka utaratibu wa wataalam na viongozi wa kisiasa kukutana na kujadili masuala yanayoonekana kuwa ni changamoto na kutoa ushauri.

Pia, utaratibu mwingine ni ule wa kuunda Tume na Kamati ili kuisaidia Serikali katika kushughulikia changamoto hizo.

Mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 57 ni pamoja na: -Sheria nyingi kutungwa au kurekebishwa kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa mambo ya Muungano, kwa mfano:- Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria Na.13 ya 1995; Sheria ya Uhamiaji, Na. 6 ya mwaka 1995 imetungwa na sasa Watanzania wanaweza kwenda sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila vikwazo.

Sheria ya Mamlaka ya Kodi, Na. 11 ya 1995; Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Na. 1 ya 1995; Sheria ya Tume ya Pamoja na Fedha Na. 14 1996; Sheria ya Biashara ya Bima ya Tanzania Na.18 ya 1996; Sheria ya Usalama wa Taifa Na. 15 ya 1996; Sheria ya Uraia Na. 6 ya mwaka 1995; na Sheria ya Usalama wa Taifa Na. 15 ya mwaka 1995.

Sheria namba 34 ya mwaka 1994 iliyoanzisha Ofisi ya Makamu wa Rais na kumpatia jukumu lingine la kuratibu ushirikiano katika masuala yasiyo ya Muungano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, lengo ikiwa ni kuimarisha masuala yasiyo ya Muungano ya pande mbili za Muungano;

Jeshi la Polisi limefanya kazi kubwa ya kudumisha amani na kushirikiana na wananchi katika shughuli za maendeleo.
Jeshi hili limeundwa na askari toka pande mbili za Muungano ambao wanafanya kazi kwa ushirikiano.

Kuongezeka kwa uelewa kuhusu umuhimu na faida za Muungano kwa umma wa Watanzania kuhusu Muungano wetu.Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea na jitihada za kuelimisha umma kuhusu umuhimu na faida za Muungano kupitia Redio, Televisheni, Magazeti, Semina, Warsha, Makongamano, Maonesho ya Kitaifa, Ziara na machapisho;

Uratibu wa vikao vya kutafutia ufumbuzi changamoto za Muungano. Changamoto zilizopatiwa ufumbuzi ni: – Utekelezaji wa Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; Utekelezaji wa Merchant Shipping Act katika Jamhuri ya Muungano na Uwezo wa Zanzibar Kujiunga na International Maritime Organisation (IMO); Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; Uwezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kukopa Ndani na Nje ya Nchi.

Pia Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT); Ajira kwa Watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano; Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asili; Ongezeko la Gharama za Umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO; Ushiriki wa SMZ katika masuala mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda; Kuondoa kodi katika unga wa maziwa toka Zanzibar kuja Tanzania Bara; Gharama za Kushusha Mizigo (Landing Fees); na Upatikanaji wa fursa za ushiriki wa Zanzibar katika miradi ya maendeleo ya viwango na ubora wa bidhaa na maendeleo ya wajasiriamali.

Miradi ya maendeleo imebuniwa na kutekelezwa na Serikali zetu mbili ili kunufaisha wananchi wake. Utekelezaji wake umekuwa na matokeo endelevu katika nyanja zifuatazo:Elimu; Afya; Masoko; Maji; Mazingira pamoja na Usafiri na Usafirishaji.

Uratibu wa masuala ya ushirikiano baina ya Serikali zetu mbili umeendelea kuimarisha Muungano kwani umewekwa mwongozo wa vikao vya kisekta ambavyo vinasimamiwa na kuratibiwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar; na

SMT imejenga majengo kadhaa Zanzibar kwa lengo la kusogeza karibu huduma kwa watanzania wote. Ofisi hizo ni pamoja na: – Ujenzi wa Ofisi na Makazi ya Makamu wa Rais Tunguu, Zanzibar; Ujenzi wa Tawi la Benki Kuu – Gulioni, Zanzibar; Ofisi ya Uhamiaji, Zanzibar; Ofisi ya Bunge Tunguu, Zanzibar; Makao Makuu ya Mamlaka ya Uvuvi katika Ukanda wa Bahari Kuu – Fumba, Zanzibar; na Taasisi ya Sayansi za Bahari –Buyu, Zanzibar. Ofisi zingine zilizoanzishwa ni: – Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Kikwajuni – Zanzibar; Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imefungua Ofisi ndogo – Zanzibar; TANTRADE; NIDA; Sekretarieti ya Ajira, Shangani – Zanzibar; TAEC na COSTECH, Maruhubu – Zanzibar.

Kimsingi, tunayo kila sababu ya kujivunia kufikisha miaka 56 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Zipo sababu nyingi za kujivunia zikiwemo Muungano wetu kudumu kwa muda mrefu.

Bila shaka ni wajibu na jukumu la kila Mtanzania kuulinda, kuimarisha na kuudumisha Muungano wetu kwa kwa maendeleo endelevu ya taifa letu.