Na Joyce Kasiki,TimesMajira Online
CHUO cha Ufundi Stadi (VETA) mwaka huu kimeadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake kwa mafanikio makubwa katika kukuza ujuzi, kuongeza vyuo, na kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi ili kuhakikisha wahitimu wake wanaingia moja kwa moja kwenye soko la ajira au kujiajiri.
Kwa mujibu wa Joseph Mchanake, Mtaalamu wa Ubunifu na Ujenzi wa Majengo kutoka VETA Makao Makuu, taasisi hiyo imejipanga kubadilika kulingana na mahitaji ya wakati huku akisema ,katika kipindi cha miaka 30, VETA imeongeza idadi ya vyuo kutoka 47 mwaka 2021 hadi 80 mwaka huu, huku serikali ikiendelea na ujenzi wa vyuo vingine 65 kote nchini (64 vya wilaya na kimoja cha mkoa).
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la VETA kwenye maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba,Mtaalam huyo amesema,mabadiliko haya yamechochewa na tafiti za soko la ajira zinazoonesha maeneo yenye mahitaji makubwa ya mafunzo ya ufundi karibu na wananchi, badala ya kuwalazimisha kusafiri mbali kutafuta elimu hiyo.
Amesema,katika kuboresha utoaji wa elimu, VETA hutoa mafunzo kwa njia ya vitendo ambapo wanafunzi huzalisha bidhaa halisi zinazokidhi mahitaji ya soko na kwamba , baadhi ya bidhaa hizo huingia moja kwa moja kwenye biashara, jambo linalowajengea wanafunzi uelewa wa kibiashara na kujiamini wanapoingia mtaani. Uzalishaji huu huendeshwa sambamba na tafiti za kila mwaka kuhusu aina ya mafundi na ubunifu unaohitajika sokoni.
Vile vile amesema,idadi ya fani zinazotolewa imeongezeka kutoka 28 hadi 89, na udahili wa wanafunzi umeongezeka kutoka 1,940 hadi zaidi ya 83,000 kwa mwaka. Kuongezeka kwa vyuo pia kumeongeza uwezo wa kudahili wanafunzi wa muda mrefu na muda mfupi, huku serikali ikitenga zaidi ya Shilingi bilioni 10 kila mwaka kwa ajili ya kuboresha vyuo vya zamani na kuongeza vifaa vya kisasa vinavyoendana na maendeleo ya teknolojia.
pia amesema VETA pia inashirikiana na sekta binafsi, hasa viwanda, kwa kutoa mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi waliopo, kutoa wanafunzi kwa mafunzo ya vitendo, na kuwasaidia baadhi ya wahitimu kupata ajira. Katika sekta ya madini, VETA inashirikiana na taasisi husika kuwapa vijana mafunzo ya kisayansi ya uchimbaji wa madini, wakitoka chuoni wakiwa na uwezo wa kufanya kazi kitaalamu au kujiajiri kama wachimbaji wadogo wenye uelewa wa kitaalamu.
Aidha amesema ,kupitia mpango wa urasimishaji wa ujuzi , VETA inawatambua mafundi waliopata ujuzi kupitia njia zisizo rasmi kwa kuwafundisha kwa muda mfupi, kuwafanyia tathmini na kuwapa vyeti vinavyotambulika kitaifa. Hatua hii imeongeza fursa za ajira kwa mafundi wa mtaani ambao awali walikosa uthibitisho wa ujuzi wao.
Amesema,mafunzo kwa wajasiriamali pia ni sehemu ya mafanikio ya VETA, ambapo taasisi hiyo hushirikiana na serikali na mashirika mbalimbali kuwapa mafunzo wanawake, vijana, na makundi ya biashara ndogondogo kama mama lishe. Hivi karibuni, VETA imetoa mafunzo kwa wanawake kupitia mpango wa “Wanawake na Samia”, ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo wananchi kujitegemea.
VETA pia imepiga hatua kubwa katika kuwahudumia watu wenye ulemavu kwa kuwapa mafunzo ya ufundi bila ubaguzi. Idadi ya wanafunzi kutoka makundi maalum imeongezeka kutoka wanane hadi 362 kwa mwaka, hatua inayosaidia kuwaondoa katika hali ya utegemezi na kuwawezesha kupata kipato halali kwa kutumia ujuzi wao.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi