November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhina: Nishati safi itachochea uchumi, kuimarisha afya za wananchi

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi (LPG) itasaidia wananchi hususani wanawake kuondokana na changamoto za kiafya,athari za mazingira pamoja na kuchochea uchumi wa taifa.

Kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wa miaka 10(2024 – 2034),imebainisha utafutaji wa kuni hususani vijijini kwa ajili ya kupikia nyumbani hutumia wastani wa saa sita kila siku.

Hivyo, huathiri shughuli za kiuchumi kutokana na kutumia muda mrefu kutafuta nishati hiyo,ambapo muda huo ungeweza kutumika kwa shughuli za maendeleo kama kujiendeleza kielimu, kujitafutia na kujiongezea kipato.

Akizungumza na Timesmajira Online,Agosti 8,2024, katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi yaliofanyika uwanja wa Nyamh’ongolo wilayani Ilemela mkoani Mwanza,Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA),Kanda ya Ziwa George Mhina ameeleza kuwa wanawahimiza wananchi kuepuka matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa na badala yake watumie nishati safi ikiwemo gesi ya kupikia kwa ustawi wa maisha yao na uchumi wa taifa.

Ambapo ameeleza kuwa matumizi ya gesi ya kupikia inaweza kugharimu wastani wa sh.30,000 hadi 35,000 kwa mwezi tofauti na anayetumia nishati ya mkaa anaweza kutumia sh.60,000 kwa mwezi.

“Inaokoa fedha ambayo angetumia kwenye mkaa na kuni kwa mwezi anaweza kutumia kutunza kwa ajili ya matumizi mengine ya kimaendeleo,pia inaepusha maradhi na magonjwa kwani ile fedha ambayo angetumia kujitibu ataitumia kwenye shughuli za maendeleo,”ameeleza Mhina na kuongeza kuwa

“inaokoa mazingira pia na muda kwani kitu ambacho ungepika kwa nusu saa kwenye nishati ya mkaa au kuni kwenye gesi unaweza kutumia dakika kumi hivyo muda uliobaki unaweza kutumia kwa ajili ya kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo,kijamii na mengineyo,”.

Ambapo kwa mujibu wa Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Misitu ya Mwaka 2021 – 2031, inakadiriwa kuwa kiasi cha hekta 469,420 za misitu hukatwa kwa mwaka kwa ajili ya shughuli za kibinadamu ikiwemo kukata miti kwa ajili ya kuni na kuchoma mkaa, hivyo,
kuchangia kuongezeka kwa ukame nchini pamoja na athari za kiikolojia.

Pia Mhina ameeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alizindua mpango mkakati wa miaka kumi(2024-2034) wa kuhimiza nishati safi ya kupikia ukiwa na lengo kuhakikisha unafikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati hiyo katika kipindi hicho.

“Takwimu zinaonesha dada,mama zetu wamekuwa wakipoteza maisha kwa sababu ya kuvuta hewa chafu inayotokana na moshi wa kuni na mkaa pia zinaonesha zaidi ya watu milioni 32 upoteza maisha kila mwaka dunia kote,kutokana na madhara ya kuvuta hewa inayotokana na moshi wa kuni na mkaa hivyo tumeshiriki katika maonesho haya ili kuwahimiza wananchi watoke katika matumizi ya nishati chafu watumie nishati safi”.

Kwa upande wake mmoja wa wananchi mkoani Mwanza Agnes Lucas,ameeleza kuwa matumizi ya gesi ya kupikia nyumbani yamemsaidia kuharakisha shughuli za upishi hata akiwa amechelewa kutoka katika shughuli zake za kumuingizia kipato.

“Najaza mtungi mdogo wa gesi kwa sh.24,000 natumia kwa mwezi wakati mwingine siku 27,ambayo imenisaidia kupunguza gharama ya mkaa ambao kwa sasa natumia mkaa kidogo kama 10000 kwa mwezi kwa ajili ya kupikia maharage tofauti na awali nilikuwa natumia zaidi ya 50000 kwa ajili ya matumizi ya mkaa wa kupikia,”.

Lidia Hugo amesema hakuna mtu asiye penda raha changamoto Watanzania kipato chetu kinatulazimisha kununua vitu vya matumizi ya siku na siyo ya jumla ya kutumia muda mrefu.

“Mimi natamani ufanyike utaratibu wa kuanzisha ujazajwi wa gesi ya kupikia kidogo kidogo kulingana na kipato cha mtu kama inavyofanyika kwenye nishati nyingine ya mkaa hata umeme,”.