Na Heri Shaaban, Timesmajira Online,Ilala
Miongoni mwa kada wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), waliojitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka kwa nafasi ya Ubunge Jimbo jipya la Kivule ni pamoja na Mhandisi Amiri Muhando.
Wengine ni Chacha Wambura Nchama mfanyabiashara maarufu jijini Dar-es-Salaam pamoja na Angelina Akilimali, Mhariri wa Radio Uhuru ,Mjumbe Mstaafu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Watia nia hao watatu wamejitokeza kuchukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi ya Ubunge katika jimbo jipya la Kivule, Wilaya ya Ilala, mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari,Mhandisi Amiri Muhando,amesema ameamua kuwania nafasi hiyo ili kusaidia kutatua changamoto za maendeleo zinazolikabili jimbo hilo jipya.
“Mimi ni mtaalamu wa miundombinu, nina uzoefu wa changamoto za eneo hili. Nikipata ridhaa ya chama, nitahakikisha huduma za kijamii na maendeleo yanawafikia wananchi kwa ukaribu zaidi,”amesema.
Kwa upande wake Chacha Wambura Nchama, mfanyabiashara maarufu, amesema ameamua kwa ridhaa yake kugombea ili kusaidia serikali kuwaletea wananchi maendeleo.
“Nimejipima nimeona natosha kupeperusha bendera ya CCM.Jimbo la Kivule lina changamoto nyingi hasa miundombinu, na mimi nipo tayari kuchapa kazi na kushirikiana na wananchi kuzitatua,”amesema.
Naye Angelina Akilimali,amesema dhamira yake ni kutumikia wananchi wa jimbo la Kivule kwa moyo mmoja, akisisitiza kuwa hajachukua fomu kwa ajili ya madaraka bali kwa lengo la kuhudumia jamii.
“Kivule kinahitaji mtu makini na ninaishukuru CCM kwa malezi niliyopata. Nikiwa mzawa wa Kivule, changamoto za eneo hili nazifahamu vyema,”amesema.

Jimbo la Kivule ni miongoni mwa majimbo mapya yaliyoanzishwa kufuatia ukubwa wa Jimbo la Ukonga ambalo awali lilikuwa na kata 13, kabla ya kugawanywa.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi