Na Esther Macha,Timesmajira Online, Mbeya
NAIBU Waziri wa Maji,Mbunge wa Vitimaalum Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Maryprisca Mahundi,kuwezesha mama lishe wa halmashauri zote za Mkoa huo mitungi ya gesi zaidi ya 700 na mchele zaidi ya kilo 3500 kupitia tamasha la Mama Ntilie (Mama Ntilie Festival).
Tamasha hilo ambalo limezinduliwa leo na linategemewa kufanyika katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya, ambapo mitungi hiyo ya gesi pamoja na mchele vitatolewa kwa mama lishe mkoani humo.
Ambapo Mhandisi Mahundi amesema kupitia tamasha la mama ntilie atatoa nafasi kwa wanawake saba watakao fanya vizuri katika mashindano ya mapishi kusoma bure mafunzo ya upishi katika chuo cha VETA Mbeya.
Mhandisi Mahundi ameeleza hayo wakati akizindua tamasha la Maryprisca Festival, Mama Ntilie wilayani Rungwe mkoani Mbeya, lililoandaliwa kwa lengo la kuwawezesha mamalishe mitungi ya gesi Ili kupunguza matumizi mkaa na kuni.
Pia katika uzinduzi huo amegawa mchele kilo tano kwa washiriki wote 100 na fedha taslimu shilingi 30,000 kwa washindi 20 wa mwanzo pamoja na mambo mengine amesema atasomesha washindi saba watakao patikana katika mashindano hayo kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya.
Sanjari na hayo Naibu Waziri huyo amesema kuwa Mama Ntilie ambao watasomeshwa bure VETA mara baada ya kuhitimu mafunzo watapatiwa vyeti ambavyo vitawasaidia kuongeza thamani ya ofisi zao.
Pia watafanyiwa utaratibu wa kusaidiwa kusajili majina ya biashara zao kwa Wakala wa Usajili wa Kampuni ya Biashara(BRELLA).
“Tunataka kuona mkibadilika mtoke namna mlivyokuwa mkihudumia watu na mhudumie katika ngazi zingine za juu ili muongeze kipato na kuchangia pato kwenye familia pamoja na kuweka heshima kwenye ndoa zenu maana mke ambaye ana mchango kwenye familia hata ndoa yake inakaa vizuri,”amesema Mhandisi Mahundi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Mbeya Edina Mwaigomole, ameshukuru mashirika mbalimbali yaliounga mkono katika kutimiza adhima ya Naibu waziri huyo hivyo ameyaomba kuendelea kumsaidia ili kuwawezesha wanawake wajasiriamali.
“Furaha ya Mhadisi Mahundi ni kubadilika kwa Mama Ntilie kwenda hatua ya pili asiwakute hapo alipowaacha na kila mtu ahakikishe kwamba anasogea na ambaye hakufanikiwa aendelee kujituma,”.
Kwa upande wake Meneja Mauzo wa kampuni ya Uuzaji Mitungi ya gesi aina ya Oryx Jastin Luaga amesema wameshiriki Maryprisca Mama Ntilie Festival lengo likiwa ni kuwatua mzigo au kuwapunguzia gharama ya maisha ikiwa na maana ya kuwashika mkono wanawake mbalimbali ambao ni mama ntilie.
Ameeleza kuwa mama Ntilie hao watapatiwa majiko ya gesi,mchele pia washindi wa kwanza 20 watapatiwa mtaji ambao utawasaidia kuongeza kipato na kuwa chachu katika maendeleo yao.
Mratibu wa mafunzo ya muda mfupi kutoka chuo cha VETA Mbeya, Rajabu Guriku,ameeleza umuhimu wa mama lishe kupata mafunzo ya upishi, huku baadhi ya mama lishe kutoka Wilaya ya Rungwe wakielezea mafunzo hayo yatakavyo wasaidia katika kukuza kipato chao.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa