January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi Mahundi azindua michuano ya Mastara Cup 2021

Na Esther Macha,TimesMajira Online, Mbeya

NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi MaryPrisca Mahundi amesema, atahakikisha anashirikiana na waandaji wa michuano ya Mastara Cup 2021 pamoja na kutafuta wadhamini wakubwa ili kukuza vipaji kwa vijana.

Mhandisi Mahundi ametoa ahadi hiyo wakati wa kuzindua michuano ya Mastara Cup 2021 katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge Jijini Mbeya inayojumuisha timu 32.

Amesema, katika dunia ya sasa michezo ina umuhimu mkubwa na inafanya vijana wasiweze kujihusisha na matukio ya ajabu hivyo anaungana na waandaji hao kuwa katika kufanikisha michuano ambayo kwa kiasi kikubwa itaibua vipaji kwa vijana.

“Michezo ina umuhimu mkubwa na ukiangalia ni moja ya sekta inayotoa ajira nyingi kwa vijana hivyo nitahakikisha nasimama bega kwa bega na waandaaji wa mashindano haya kuhakikisha tunapata wadhamini ambao wataiongezea hamasa zaidi,” amesema Mhandisi Mahundi.

Muandaaji wa michuano hiyo, Willy Mastara amesema, mpaka sasa hajaweza kupata wadhamini wa michuano hiyo lakini anaendelea kufanya za kuwasaka ili michuano hiyo iweze kufanikiwa na hatimaye kuibua vipaji kwa vijana.

Mbunge wa Mbeya Mjini na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Tulia Ackson amekubali kutoa zawadi zote za michuano hiyo baada ya kupokea ombi kutoka kwa mwandaaji hao.