November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi Kundo atoa wiki mbili,wananchi kuunganishwa maji

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew,ametoa wiki mbili kwa Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA) Kanda ya Nyakato kuhakikisha wananchi wa mtaa wa Kigala Buswelu wilayani Ilemela mkoani Mwanza wanaunganishiwa huduma ya maji.

Mhandisi Kundo ametoa kauli hiyo Julai 27,2024 wakati alipofanya ziara ya nyumba kwa nyumba katika mtaa huo ya kujionea kama huduma ya maji inawafikia wananchi wa eneo hilo.

“Hakikisha mafundi wako ata watatu wawe site mwananchi akikamilisha kupata vifaa akauganishiwe maji moja kwa moja ,nakupa wiki mbili huku sitaki kuona changamoto hii,bahati mbaya kwako nitakuwa na ziara Simiyu,Agosti 11 naenda kwa Askofu Geita,nitapita hapa kuona kama watu wa eneo hili wanapata maji,”ameeleza Mhandisi Kundo.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa mtaa huo wameeleza kufurahishwa na kauli ya Naibu Waziri wa Maji ya kutoa wiki mbili kuhakikisha mtaa huo wa Kigala ‘A’, wanapata maji kwani inaonesha dhamira ya serikali ya kumtua mama ndio kichwani.

“Tulikuwa tunapitia changamoto ya maji maeneo haya, sisi tunachota maji mpaka usiku huku umeacha watoto ndani na tunafuata maji mbali bondeni ambayo siyo salama wakati mwingine ,”.

Sanjari na hayo Naibu Waziri wa Wizara ya Maji Mhandisi Kundo Mathew Julai 26,2024 akiwa kisiwani Bezi Kata ya Kayenze wilayani Ilemela alipotembelea na kukagua maandalizi ya kuanza kwa ujenzi wa mradi wa maji unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), ameeleza kuwa mradi huo unatarajia kuwanufaisha wananchi 6,378 waishio kisiwani humo.

Mhandisi Kundo ameeleza kuwa ujenzi huo unatarajiwa kuanza Septemba 2024 na kukamilika Februari 2025 huku kazi zitakazofanyika katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa vituo 15 vya kuchotea maji, ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji la lita 250,000 pamoja na ulazaji wa mtandao wa mabomba.