Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Mbozi
NAIBU Waziri wa Majira, Mhandisi Kundo Mathew ametoa maelekezo kwa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Rukwa, kuhakikisha wanatunza na kuhifadhi rasilimali za maji na vyanzo vyake, ikiwemo kutoa elimu kwa jamii ili huduma za maji ziwe endelevu.
Ametoa maelekezo hayo Januari 13, 2025, mara baada ya kuzindua miradi ya maji katika vijiji vya Ileya na Sambewe, wilayani Mbozi, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili mkoani Songwe.
Akizungumza na viongozi na wananchi wa vijiji hivyo, Mhandisi Kundo amesema changamoto za maji katika vijiji vya Ileya na Sambewe Kata ya Itumpi sasa zimepatiwa ufumbuzi baada ya kukamilika kwa miradi hiyo iliyogharimu kiasi cha milioni 120.
Miradi hiyo, iliyoanza utekelezaji wake tangu Oktoba 11,2024, imetekelezwa kwa juhudi za Mbunge wa Jimbo la Mbozi, George Mwenisongole, kwa kushirikiana na washirika wake.
Miradi hiyo ya maji imehusisha,uchimbaji wa visima viwili vyenye uwezo wa kuzalisha lita 4,800 na 6,200 kwa saa, ujenzi wa matenki mawili kwa ajili ya usambazaji.
Pamoja na vituo vinne vya kuchotea maji (vituo viwili katika kila kijiji), ikiwemo ufungaji wa mifumo ya nishati ya jua (solar) kwenye visima vyote viwili.
Naibu Waziri Kundo, ameipongeza Mamlaka ya Maji Safi Mijini na Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mbozi ,kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo na jitihada za kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
“Sasa ni jukumu letu wote kama Serikali na jamii, kuhakikisha miundombinu ya maji inalindwa na vyanzo vya maji vinahifadhiwa,” amesema Mhandisi Kundo.
Awali katika taarifa yake,
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mbozi, Ismail Nassor,amesema miradi hiyo ya maji itahudumia wakazi 4,068 wa vijiji vya Ileya na Sambewe.
More Stories
Watatu mbaroni kwa tuhuma za mauaji wakigombania shamba
Ng’ombe 10 wamekufa kwa kupigwa na radi
Rukwa waanzisha utalii wa nyuki